
Kwa mujibu wa Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF iliyotolewa leo jijini New York, Marekani, takwimu zinaonesha kuwa nchi ya Iran ndiyo iliyoathirika vibaya zaidi ikiwa na vifo vya watoto 216 na waliojeruhiwa 1,767, ikifuatiwa na Lebanon yenye vifo 124, majeruhi 413.
Nchini Israel watoto wanne wamepoteza maisha huku 862 wakijeruhiwa, na Kuwait kifo kimoja. Maeneo mengine yenye majeruhi ni Bahrain watoto wanne, na Jordan mtoto mmoja.
“Tukio la kusikitisha zaidi limetajwa kuwa ni shambulio la kombora katika shule ya Shajareh Tayyebeh nchini Iran lililouwa watoto 168 kwa siku moja, jambo linaloashiria uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu,” imesema taarifa hiyo.
Mashambulizi yasiyokoma ya pande zinazozozana katika nchi nyingi yanaharibu vifaa na miundombinu ambayo watoto wanategemea, ikijumuisha hospitali, shule, na mifumo ya maji na usafi wa mazingira. Ghasia zinazoendelea katika Jimbo la Palestina, ikiwa ni pamoja na Gaza na Ukingo wa Magharibi, katika kipindi hicho zimeua watoto 16 wa Palestina na kujeruhi zaidi ya 50.
Kauli ya Mkuu wa UNICEF
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell, amelaani mashambulizi hayo yanayolenga miundombinu ya kijamii.
“Watoto katika eneo hili wanapitia ukatili wa kutisha, huku mifumo na huduma ambazo zinapaswa kuwaweka salama zikishambuliwa. Hatua za haraka zinahitajika kutoka kwa pande zote zinazopigana ili kulinda maisha ya raia na kuheshimu haki za Watoto,” amesema Russell.
Athari mbaya za ongezeko la gharama ya mafuta kwa lishe na dawa
Mbali na vifo na majeraha nchini, vita hivi vimesababisha usumbufu mkubwa wa usafirishaji katika Mlango Bahari wa Hormuz na kanda nzima, jambo ambalo UNICEF inakadiria linaweza kusababisha ucheleweshaji wa hadi miezi sita kwa bidhaa muhimu kufika duniani kote.
Ongezeko la bei ya mafuta linalotabiriwa kufikia asilimia 20 linaongeza gharama za utengenezaji wa bidhaa muhimu kama chanjo na lishe, huku njia ndefu za baharini zikiongeza hadi wiki nne za safari kwa meli za mizigo. Ili kuhakikisha huduma hazisimami kwa watoto duniani, UNICEF imeanza kutumia njia mbadala za anga, ardhi, na bahari, huku ikifanya mazungumzo na wasafirishaji ili kupunguza tozo za ziada na kutoa kipaumbele kwa mizigo ya kibinadamu.
Usaidizi wa dharura nchini Lebanon na Iran
Nchini Lebanon, UNICEF imeongeza operesheni zake na kufanikiwa kukarabati mifumo 20 ya maji na usafi inayohudumia watu milioni 1.2, huku ikipanua huduma za afya zilizounganishwa ikiwemo chanjo na huduma za dharura kwa watoto wachanga katika vituo zaidi ya 290 vya wakimbizi na kwa watu 480,000 katika jamii zinazohifadhi wakimbizi.
Huko Iran, kufuatia ombi la Wizara ya Afya, shirika hilo limeweka vituo vya afya vinavyotembea na mahema ya huduma ya kwanza ili kurejesha huduma kwa watu takriban 226,000 katika maeneo yaliyoathirika vibaya. Msaada huu unajumuisha utoaji wa chanjo na msaada wa kisaikolojia (MHPSS) kwa watoto na vijana waliokumbwa na kiwewe cha milipuko na kupoteza makazi zaidi ya milioni 1.2.
UNICEF imerejea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutaka usitishwaji wa haraka wa mapigano na pande zote kujizuia kutumia nguvu kupita kiasi. Chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu, raia hususan watoto na miundombinu ya kijamii kama shule na hospitali lazima vilindwe wakati wote wa vita.