Meli nyingi hazijaweza kupita kwenye mkondo huo muhimu wa kimkakati huku Iran ikiendelea na vita vyake na Marekani, Israel na nchi nyingine katika eneo hilo.

Ufunguzi wa Hormuz unasalia kuwa lengo kuu la Jumuiya ya Kimataifa kutokana na umuhimu mkubwa kiuchumi katika usambazaji wa mafuta na mbolea duniani.

Katika mahojiano na Nathalie Minard wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa (UN NEWS) kuelekea Siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu mabomuya kutegwa ardhini na Msaada wa Hatua Dhidi ya Mabomu hayo, inayoadhimishwa kila tarehe 4 Aprili, Mtaalamu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya msaada wa kutegua mabomu UNMAS, Paul Heslop ameeleza kuwa uteguaji mabomu ya baharini ni kazi hatari na ngumu mno kulinganisha na mabomu ya nchi kavu.

media:entermedia_image:fb597e86-3ce3-463c-b38a-cbb0655c2e3c

UN News/Daniel Johnson

Paul Heslop, UNMAS

UN NEWS: Je, una taarifa zozote kuhusu vilipuzi vya majini vilivyomo katika Mlango Bahari wa Hormuz?

Ingawa bado hakuna ripoti rasmi zilizothibitisha idadi kamili ya mabomu yaliyotegwa, ukweli kwamba jeshi la maji la Iran lilikuwa na akiba kubwa ya silaha hizi kabla ya kuanza kwa vita dhidi ya Marekani na Israel, hii imezidisha wasiwasi wa kiusalama kwa usafirishaji wa mafuta na mbolea duniani.

Utegaji wa mabomu hayo unaweza kufanyika hata kwa kutumia boti ndogo za uvuvi, au meli maalumu za kutega mabomu.

UN NEWS: Ni aina gani za mabomu ya baharini zinazoweza kutegwa?

Tofauti na mabomu ya ardhini ambayo hubaki sehemu moja baada ya kutegwa, mabomu ya baharini yana changamoto ya kipekee kwa sababu yanaweza kutegwa katika aina tatu tofauti: yanayoelea juu ya maji, yanayoelea ndani ya maji, au yaliyotulia chini kabisa ya sakafu ya bahari.

Yanaweza kutengenezwa kwa plastiki au chuma. Mifumo yake ya milipuko inajumuisha kuguswa na boti, nguvu za usumaku wa baharini, au yanaweza kulipuliwa kwa rimoti, au kupangwa muda maalumu wa kulipuka.

UN NEWS: Kwa nini mabomu ya baharini ni changamoto zaidi kuyategua?

Mbali na kutumia vipimo vitatu vya urefu, upana, na kwenda chini, kuna kipimo cha nne ambacho tunatazama muda, kwani mikondo ya maji, mawimbi makali, na mabadiliko ya maji kupwa na kujaa husababisha mabomu haya kuhama sehemu moja kwenda nyingine kila wakati. Hali hii inafanya eneo la Mlango Bahari wa Hormuz ambalo endapo likisafishwa leo huweza kuchafuliwa tena kesho na bomu lililosukumwa na maji kutoka sehemu nyingine, jambo linalofanya kazi ya wataalamu wa kutegua mabomu kuwa ya hatari na inayobadilika kila saa huku wakifanya kazi katika mazingira yenye mienendo isiyotabirika.

UN NEWS: Je, yanawezaje kugunduliwa?

Teknolojia inayotumika kugundua mabomu hayo inajumuisha vifaa maalum, ‘sonar’ vinavyotumia mawimbi ya sauti na sumaku kwa ajili ya kutambua chuma, lakini hata vifaa hivi hukumbwa na vikwazo vya kimuundo na mfumo kama vile maeneo yenye joto kali la maji, ambayo yanaweza kuzuia, kudhoofisha, au kupotosha mawimbi ya sonar, hali inayofanya mabomu yaliyojificha chini ya tabaka hilo kutokuonekana kwa urahisi kwenye mitambo ya meli za uokoaji.

Picha ya satelaiti ya Mlango-Bahari wa Hormuz, unaounganisha Ghuba ya Oman na Ghuba ya Uajemi, na kutenganisha Iran na Oman, UAE, na Qatar.

Njia ya meli muhimu ya kimkakati ya Mlango-Bahari wa Hormuz imeoneshwa ikitenganisha mataifa ya Falme za Kiarabu na Iran.

UN NEWS: Ni nchi gani zenye meli za kutegua mabomu na uwezo wa kiufundi wa kuingilia kati katika eneo hilo mahususi la mabomu ya baharini?

Haya yanajiri wakati ambao tunashuhudia mabadiliko. Kwa sasa mataifa mengi yanahamia kwenye teknolojia mpya inayotumia ndege zisizo na rubani yaani droni na roboti za chini ya maji ili kulinda maisha ya binadamu wakati wa kazi hiyo hatari ya uteguaji inayohitaji umakini mkubwa.

UN NEWS: Ikiwa mabomu ya baharini yatathibitika kuwa tishio kwa usafirishaji, ni suluhisho gani litakaloruhusu usafiri kuanza tena mara tu amani itakaporejeshwa?

Ili kurejesha usafirishaji wa bidhaa muhimu katika Mlango Bahari wa Hormuz pindi amani itakapopatikana, suluhisho la muda mrefu litahitaji mifumo ya doria ya kila siku, inayofanana na ile inayotumika kwenye shughuli za kulinda amani nchi kavu ambapo gari la ulinzi hukagua barabara kila asubuhi. Mpango unaopendekezwa ni kutengeneza njia maalumu zenye upana wa kilomita kadhaa ambazo zitasafishwa kila siku na meli za ulinzi au droni zinazotangulia mbele ya msafara wa meli za kibiashara ili kuhakikisha usalama wa njia hiyo. Hii ni kwa sababu haiwezekani kusafisha kila mita ya mraba ya Mlango Bahari wa Hormuz kila siku, hivyo njia hizo maalumu zitalindwa kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha kuwa hakuna bomu jipya lililotegwa usiku au kusukumwa na maji kuingia kwenye njia hiyo ya usafiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *