Maelfu wakimbilia Syria
Zaidi ya watu 200,000 wamevuka mpaka wa Lebanon na kuingia Syria tangu mashambulizi baina ya Israeli na Hezbollah yaanze mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya Marekani na Israeli kushambulia Iran.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema hayo leo huko Geneva, Uswisi likitanabaisha watu wengi wanakimbia mashambulizi mazito yanayofanywa na Israeli kwenye dhidi ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, na maeneo mengine ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Mwakilishi wa UNCHR nchini Syria, Asseer Al-Madaien, amesema wengi wao wanawasili wako hoi, wana kiwewe na virago vichache.
Soma kwa kina hapa.
Mabaharia hatarini – IMO
Katika hatua nyingine, shirika la Umoja wa Mataifa la Usafirishaji Baharini, IMO, limesema kumefanyika shambulio ligine dhidi ya meli kwenye lango la bahari la Hormuz.
Shambulio hili la karibuni zaidi linafanya kuweko kwa mashambulio 19 dhidi ya eneo hilo la Ghuba ambalo ni muhimu na hutegemewa na zaidi ya robo ya meli zinazosafirisha mafuta na gesi duniani.
IMO inasema shambulio hlo limesababisha moto mkubwa kwenye meli ya mafuta, kaskazini-magharibi mwa Dubai, Falme za kiarabu. “Kwa sasa wafanyakazi wako salama, ingawa uchafuzi wa baharini umeripotiwa.”
Kwa sasa shirika hilo lenye makao yake makuu limesema lina wasiwasi kuhusu usalama wa mabaharia 20,000 waliokwama ndani ya meli 2,000 huko Ghuba.
Hali ya sasa kwa mujibu wa IOM haijawahi kutokea tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Soma habari nzima hapa
Usambazaji wa chakula kwa familia za wakimbizi kaskazini mwa Lebanon.
Mgao wa chakula cha msaada mashakani- WFP
Tani 70,000 za msaada wa chakula kutoka Umoja wa Mataifa zilizokuwa zimelengwa kupatiwa watu walio hatarini katika nchi mbalimbali kwenye ukanda huo zimekwama kutokana na mapigano yanayoendelea huko Mashariki ya Kati, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Bidhaa hizo kwa sasa ziko kwenye meli kwenye eneo hilo na meli haziwezi kwenda kokote.
WFP ilikuwa ikiwasilisha kupitia Iran misaada ya chakula kwa takribani watu milioni 17 wenye uhitaji nchini Afghanistan.
Shirika hilo linasema sasa linalazimika kusafirisha msaada huo kwa malori kutoka Dubai kupitia Saudi Arabia na kisha kuelekea Afghanistan.