Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva, Gift Stanford, maarufu Gigy Money, kwa sasa unaweza kumuita Rawya kwani ameanza ukurasa mpya wa maisha baada ya kufunga ndoa na Licky ‘Tarick’, Machi 13, 2026, jijini Dar es Salaam.

Ndoa hiyo imekuja na mabadiliko makubwa, ikiwemo kubadili dini na sasa anaitwa Raway.

Katika mahojiano na Mwananchi, Gigy Money amezungumzia kuhusu maisha mapya ya ndoa na mambo ambayo ameamua kuachana nayo ili kulinda heshima ya familia yake.

GIG 01

Maisha baada ya ndoa 
Gigy anasema ndoa imeleta utulivu mkubwa katika maisha yake na kumfanya awe mtu mwenye mipango zaidi tofauti na ilivyokuwa zamani. Anakiri kuwa maisha ya awali ya usanii yalikuwa na pilikapilika nyingi ambazo wakati mwingine zilimfanya ashindwe kuwa na mwelekeo sahihi.

“Kwa sasa nimekuwa mtu wa kupanga maisha yangu vizuri zaidi, ndoa imenipa mwelekeo mpya kabisa, imenifanya nijitambue na kujua nini hasa nataka kwenye maisha yangu,” anasema Gigy.

‘Show off’
Moja ya mambo makubwa aliyosisitiza ni kuachana na maisha ya kujionesha kupita kiasi (show off), tofauti na ilivyozoeleka kwa baadhi ya mastaa.

“Zamani nilikuwa naishi maisha ya ‘show off’ sana, kila kitu lazima watu wajue. Lakini sasa nimejifunza kuwa si kila jambo linahitaji kuwekwa wazi, ndoa yangu imenifundisha kuheshimu faragha yangu na ya mwenza wangu,” anasema.

GIG 04

Misele sasa basi 
Gigy pia anasema amepunguza sana mizunguko ya hapa na pale ambayo haikuwa na faida kubwa kwenye maisha yake.
“Siwezi kusema nimeacha kazi, hapana, muziki bado ni maisha yangu, lakini sasa nachagua sehemu za kwenda, siendi kila mahali kama zamani, naangalia heshima yangu na ya familia yangu kwanza,” anasema.

GIG 03

Ndoa si kikwazo
Akizungumzia hofu iliyopo kwa baadhi ya wasanii kuwa ndoa inaweza kuua ndoto zao za muziki, Gigy anakanusha mtazamo huo.

“Watu wengi wanaamini ukioa au kuolewa basi unaanza kushuka kisanii, lakini si kweli, kila kitu kinategemea namna unavyopanga maisha yako. Mimi bado nitafanya muziki mkubwa zaidi, lakini kwa nidhamu na mipaka,” anasema.

Anasema: “Naweza kusema wazi kabisa, ndoa imenibadilisha kwa asilimia kubwa, sio tu kwenye maisha ya nje bali hata ndani yangu. Nimeacha baadhi ya mambo ambayo hayakuwa na tija, nimepunguza marafiki wasiokuwa na mchango wa faida kwangu na zaidi nimejifunza kumheshimu mwenza wangu pamoja na familia kwa ujumla. 

“Watu wanapaswa kuelewa kuwa ndoa si gereza, bali ni sehemu ya kujifunza na kukua. Kama utaiingia kwa nia njema, inakujenga na kukufanya uwe bora zaidi kuliko ulivyokuwa awali.”

GIG 02

Ushauri kwa mastaa 
Mwisho, Gigy ametoa ushauri kwa wasanii wenzake wanaoogopa kuingia kwenye ndoa.

“Wasanii wenzangu wale wenye kuogopa kuingia kwenye ndoa, waache kuogopa ndoa. Kama umeipata kwa mtu sahihi, ni baraka kubwa sana, inaweza kukusaidia hata kufika mbali zaidi kimafanikio kuliko unavyofikiria,” anasema.

Kwa sasa, Gigy Money anaonekana kuanza safari mpya yenye nidhamu, heshima na mtazamo tofauti, jambo linaloonyesha wazi kuwa maisha ya ndoa yanaweza kuwa chachu ya mafanikio badala ya kikwazo kwake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *