“Kwa majina ni Dkt. Rukia Nzobo. Nimekuja hapa kuwakilisha shirika la Center for the Study of Adolescence jijini Nairobi, linalojulikana kwa kifupi kama CSA. Kazi yetu ni kuwatetea vijana, hasa katika masuala ya afya ya uzazi na jinsia, na pia kuwasaidia kupata elimu sahihi kuhusu afya yao. Tunafanya kazi na vijana, hususan wasichana, wanawake, na watoto.”

Mwanamke amesimama kando ya nembo kubwa ya Umoja wa Mataifa katika ukumbi wa mikutano.

Dkt. Rukia Nzobo kutoka Kenya, ambaye amewakilisha shirika la Center for the Study of Adolescence jijini Nairobi, CSA katika mkutano wa CSW70.

Nikataka kufahamu kile ambacho wanafanya?

“Kazi yetu kwa ujumla ni kuwatetea vijana, hasa wanawake na wasichana, ili wapate huduma za afya ya uzazi na elimu sahihi kuhusu afya yao. Nimekuja kuwasilisha maoni yao na kuelezea changamoto wanazokumbana nazo, hususan wasichana na wanawake wa Nairobi. Pia nimekuja kuzungumzia ukosefu wa huduma za afya. Vijana wengi nchini Kenya, hasa Nairobi na kaunti nyingine, hawapati huduma hizi kwa urahisi. Hivyo basi, jukumu langu ni kujifunza jinsi nchi nyingine zinafanya na tunawezaje kuboresha hali yetu ili kuhakikisha vijana wanapata huduma na elimu wanayohitaji. Aidha, nimekuja kuwapazia sauti na kuelewa serikali mbalimbali zinakubaliana na ahadi zipi za kisera na namna zinavyopanga kuzitekeleza. Maarifa haya nitarudi nayo nyumbani ili kuwasaidia vijana kujitetea na kudai haki zao, hasa katika kupata huduma muhimu.”

Ni ujumbe gani ungependa kutoa kwa wasichana na wanawake kote duniani?

“Ujumbe wangu ni kwamba kuwa mwanamke hakumaanishi huna haki ya kupata huduma au elimu. Kwa hakika, wanawake wanahitaji huduma na elimu zaidi ili waweze kujitegemea na kusonga mbele. Wanawake wanapaswa kusimama imara na kudai haki zao sawa na wanaume.”

Tunapozungumzia mshikamano wa wanaume katika kusongesha lengo namba tano la Maendeleo Endelevu, SDGs la usawa wa kijinsia una ujumbe gani kwa wanaume?

“Ni muhimu kwa wavulana na wanaume kuacha vitendo vya dhuluma dhidi ya wanawake. Wanawake ni binadamu sawa na wanaume, na ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha wanapata haki zao. Wanawake wanachangia pakubwa katika kuimarisha familia na jamii kwa ujumla. Kwa hivyo, wanaume wanapaswa kushirikiana na wanawake katika kusukuma mbele usawa wa kijinsia. Ukimsaidia mwanamke, unasaidia familia nzima. Sote ni binadamu na tuna mahitaji sawa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *