
Nchini Sudan mwanamke mmoja anatekeleza kwa vitendo maudhui ya siku hii mwaka huu ambayo ni Wekeza kwenye amani, wekeza kwenye hatua dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini.
Mwanamke huyo si mwingine bali ni Sadia Yahya, yeye ni kutoka shirika la kiraia la usalama liitwalo Jasmar. Kupitia video ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya msaada wa kutegua mabomu, UNMAS, anaelezea kilichochagiza yeye kuingia kwenye jukumu hilo ambalo mara nyingi huonekana ni la wanaume.
Anasema, “kile kilichonihamasisha kuingia katika operesheni za kutegua mabomu ni mzozo nchini Sudan, hasa kuzingatia ninatoka jimbo lililoathirika vibaya na mapigano ambalo ni Khordofan Kusini. Nilitaka kusaidia watu waendelee kuishi maisha ya kawaida.”
Licha ya changamoto ninajvunia kazi hii
Akiwa ndani ya jengo akikagua iwapo kuna bomu huku amevalia sare maalum ya uteguaji mabomu ambayo ni kofia ngumu ya manjano na kizibau kirefu cha buluu.
Sadia anasema, “changamoto ninazokutana nazo wanawake wa Sudan hawazikubali. Wanafikiri kuwa iwapo nikiingia kwenye kazi hii nitakumbana na hatari nyingi. Lakini ukweli ni kwamba baada ya kuingia kwenye kazi hii, ingawa ni hatari, ninajivunia na nina furaha sana.”
Ndoto ni idadi kubwa ya wanawake katika operesheni
Elnour Babiker Mohamed ni kiongozi wa timu ya shirika la kiraia la Jasmar. Yeye anazungumzia mustakabali wao akisema, “matumaini ya siku za usoni ni ni kuwa na viongozi wanawake wa Masuala ya kiufundi. Hawa ni wanawake wa nchi yangu, na ninafahamu kuwa ni thabiti, na wanavyoweza kuwajibika kuondoa mabomu ya kutegwa ardhini Sudan.”
UNMAS ilianzishwa mwaka 1997, kuongoza, kuratibu na kutekeleza shughuli za kupunguza vitisho vinavyotokana na mabomu ya kutegwa ardhini, masalia ya vilipuzi vya vita na vingine vinavyotengenezwa.