Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amezindua mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa akisema kila Mtanzania anaona faida za Mwenge katika kuchochea maendeleo, kuhamasisha amani, umoja, mshikamano wa kitaifa na kuimarisha muungano.
Uzinduzi wa mbio hizo imefanyika leo Aprili 2, 2026, katika Uwanja wa Gombani, Wilaya ya Chake-Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, na utakimbizwa katika halmashauri 195 na mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mwinyi amesema falsafa ya Mwenge wa Uhuru inatokana na maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliyetamka mwaka 1959 kwamba Watanganyika walikusudia kuwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili uangaze ndani na nje ya mipaka yao, ukileta matumaini, upendo na heshima.
Amesema azma hiyo ilitimia mwaka 1961 wakati wa Uhuru wa Tanganyika, ambapo Mwenge uliwashwa kama ishara ya mwanzo wa safari ya taifa huru lenye umoja, mshikamano na uzalendo.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akimkabidhi mkimbiza mwenge kitaifa, Wazo Mwangonda baada ya kuuwasha katika uwnaja wa Gombani Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba
Dk Mwinyi amebainisha kuwa mwaka 1964, viongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar, wakiongozwa na hayati Abeid Amani Karume, waliendeleza dhana hiyo kwa kuutumia Mwenge kama chombo cha kuhimiza haki, usawa na maendeleo ya wananchi.
Kwa mwaka huu, mbio za Mwenge wa Uhuru zinaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”
Dk Mwinyi amesema ujumbe huo unalenga kuhamasisha wananchi kuendelea kulinda amani, kuimarisha mshikamano na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amesisitiza kuwa amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kijamii ni msingi wa maendeleo endelevu, kwani huwezesha Serikali kupanga na kutekeleza sera za maendeleo kwa ufanisi.
Aidha, ameeleza kuwa matumizi ya lugha ya Kiswahili yamekuwa nyenzo muhimu ya kuwaunganisha Watanzania na kuondoa tofauti za kikabila, kidini na kiuchumi.
Kuhusu mapambano dhidi ya changamoto mbalimbali za kijamii, Dk Mwinyi amesema Mwenge wa Uhuru mwaka huu utaendelea kuhimiza vita dhidi ya rushwa kupitia kaulimbiu isemayo: “Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu.”
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua wahusika wa vitendo hivyo.
Dk Mwinyi pia amezungumzia dawa za kulevya, akisema kuwa Serikali imeongeza juhudi za kupambana na biashara na matumizi yake, ambapo kati ya mwaka 2023 na 2025, tani kubwa za dawa hizo zilikamatwa na wahusika kuchukuliwa hatua.
Wakimbiza mwenge kitaifa wakienda kutoa heshima kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kabla ya kuwakabidhi ulipowashwa katika uwnaja wa Gombano Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba
Awali, akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid, amesema mkoa huo una vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na fukwe nzuri na kilimo cha viungo.
Amesema sekta kuu za uchumi ni biashara, ujasiriamali, uvuvi na kilimo cha mwani, ambapo wananchi wameendelea kunufaika na shughuli hizo za kiuchumi.
“Mkoa wa Kusini Pemba umejipanga kuhakikisha miradi yote itakayopitiwa na kutembelewa na Mwenge huo ipo katika hali nzuri,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amewataja wakimbiza Mwenge kitaifa wakiongozwa na Wazo Magonda kutoka Mkoa wa Ruvuma.
Wengine ni Nyasi Stanslaus kutoka Mkoa wa Manyara, Peter John wa Mkoa wa Singida, Rahyan Mohamed Rashid wa Kusini Pemba, Mbula Kuyela kutoka Rukwa na Mussa Othman Ali wa Kusini Unguja.