
KUNA dakika 90 ngumu kesho kati ya Azam dhidi ya Simba pale Azam Complex, huku kocha wa matajiri hao wa Chamazi, Florent Ibenge, akishusha mkwara mzito kwa wapinzani wao.
Ikumbukwe kuwa, kwenye mchezo wa kwanza Azam ilishinda kwa mabao 2-0 mbele ya Simba ikiwa nyumbani, ambapo timu hizo zitakutana tena kwenye mechi ya marudiano hata hivyo huu utakuwa mchezo wa tatu Simba inakutana na Ibenge baada pia ya kuiongoza timu yake kuwachapa vijana hao wa Msimbazi kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi bao 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu mchezo huo, Ibenge ambaye ni kocha wa zamani wa Al Hilal ya Sudan amesema kuwa amewaambia wachezaji wake kwamba wanatakiwa kusahau matokeo ya mchezo wa kwanza wa ushindi.
Ibenge ambaye ameiongoza Azam kwenye michezo 16, wametoka sare michezo nane na kushinda michezo nane, amesema kikosi cha Simba ambacho walicheza nacho mchezo wa mzunguko wa kwanza kina utofauti mkubwa, ambapo wataingia na hesabu tofauti ya kutafuta matokeo mazuri.
“Hii ni mechi mpya kabisa. Ni kweli tulishinda mchezo wa kwanza, lakini haina maana kwamba tuna uhakika wa kushinda na huu. Nimewaambia wachezaji wangu tusahau kila kitu kuhusu ushindi wa kwanza na sasa tutambue tutakwenda kucheza mchezo mgumu zaidi,” amesema Ibenge.
“Simba ina timu tofauti kabisa na ile ambayo tulikutana nayo kwenye mchezo wa kwanza kuanzia benchi lao la ufundi na hata baadhi ya wachezaji. Kuna wachezaji wameongezwa, wazuri wenye kasi.” Aliongeza licha ya mabadiliko ya Simba, kikosi chake kipo kwenye maandalizi ya kutafuta ushindi kwenye mchezo huo, akifurahishwa na namna walivyocheza mchezo wa mwisho ugenini dhidi ya Singida Black Stars waliposhinda kwa mabao 2-1.
“Azam tunaendelea na maandalizi. Tunafahamu ugumu wa mchezo, lakini maandalizi yetu yanalenga kutafuta ushindi; kama si pointi tatu, basi tupate moja.
“Ninajivunia vijana wangu wanajituma sana. Tumetoka kucheza mechi ngumu dhidi ya Singida ambayo nilisema awali ilikuwa ni kama mechi ya mashindano ya Afrika, hususan Kombe la Shirikisho, lakini sasa tunakwenda kucheza mechi nyingine kubwa ya kiwango kama hicho.
“Nilisema awali kazi yetu kubwa sasa ni kuendelea kupunguza pointi kati ya timu hizi kubwa tofauti na msimu uliopita, bado tupo kwenye malengo hayohayo wakati tukienda kukutana na Simba.”
Ibenge ni miongoni mwa makocha wachache wa Ligi Kuu Bara ambao wameanza msimu na timu zao bila kuondolewa, huku matajiri hao wakimpa mkataba wa mwaka mmoja kukinoa kikosi hicho.