
KICHAPO cha mabao 3-0 ilichokipata Fountain Gate dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi ya Ligi Kuu Bara, Aprili 3, 2026 kwenye Uwanja wa Airtel Singida, kimemtisha Kocha Mohamed Ismail ‘Laizer’ katika mapambano ya kuinusuru timu hiyo msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer alisema mwenendo wa kikosi hicho sio mzuri kutokana na kutokuwa na balansi nzuri katika maeneo ya kujilinda na kushambulia, jambo linalomuweka kwenye wakati mgumu wa kuinusuru.
“Hatuko sehemu salama na ukiangalia hali tuliyonayo inaweza kututokea ya msimu uliopita. Kiukweli hatupendi kuona hilo likitokea ingawa ili tuepuke ni lazima tupambane zaidi. Kuna muda tunapoteza kwa makosa binafsi tu,” alisema.
Kocha huyo alisema malengo ni kuhakikisha timu hiyo inamaliza nafasi za juu na kuepuka kucheza mechi za mtoano kama ilivyokuwa msimu uliopita, huku jambo linalowapa ahueni ni kutopishana pointi nyingi na wapinzani wao wengi.
“Ukishinda mechi mbili unasogea juu zaidi kwa sababu hatujapishana sana na wapinzani wetu waliotuzidi. Bado tuna safari ndefu lakini kwa sasa tunahitaji kufanyia kazi kwa haraka eneo la kujilinda na ushambuliaji ili tutimize malengo hayo,” alisema kocha huyo.
Msimu uliopita Fountain ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 29 katika Ligi Kuu Bara na kukutana na Tanzania Prisons iliyomaliza nafasi ya 13 na pointi 31, ambapo kwenye mechi ya mtoano kikosi hicho kilichapwa jumla ya mabao 4-2.
Baada ya hapo Fountain ilicheza mchujo kubaki Ligi Kuu ambapo iliifumua Stand United kwa jumla ya mabao 5-1 kufuatia kikosi hicho cha ‘Chama la Wana’ kinachoshiriki Championship kuifunga Geita Gold kwa jumla ya mabao 4-2.
Katika mechi 17 ilizocheza msimu huu Fountain Gate imeshinda nne, sare nne na kupoteza tisa ikiwa nafasi ya 13 na pointi 16, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao manane huku kikiruhusu nyavu kutikiswa mara 22.