
Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimtaifa ya Kukuza Uelewa kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini na Usaidizi wa kuyategua, ambayo huadhimishwa kila tarehe 4 Aprili 2026, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema silaha hizo zinaendelea kusababisha madhara makubwa kwa raia, hasa watoto, wakati migogoro ikiendelea kuongezeka na matumizi ya kijeshi duniani yakipaa.
Guterres, amebainisha kuwa mabomu ya ardhini, vilipuzi vilivyosalia bila kulipuka na vilipuzi vilivyotengenezwa kienyeji vinaendelea kuwa hatari hata baada ya vita kumalizika, vikisalia katika nchi kama Colombia, Ethiopia, Lebanon na Myanmar, pamoja na maeneo yaliyoathiriwa na migogoro kama Ukanda wa Gaza na kote nchini Syria. Hatari hizi zilizojificha huua maelfu ya watu kila mwaka na kujeruhi wengine wengi, mara nyingi miaka mingi baada ya mapigano kumalizika.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa hatua za kuondoa mabomu zina umuhimu mkubwa katika maeneo yenye amani dhaifu na yaliyoathiriwa na migogoro, kwani huruhusu shughuli za kibinadamu kufanyika kwa usalama zaidi na kusaidia jamii zilizoathirika kupona na kujijenga upya.
Mshikamano
Akitoa wito wa mshikamano wa kimataifa, amewahimiza wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kupitisha na kuheshimu mifumo muhimu ya kisheria, ikiwemo ‘Anti-Personnel Mine Ban Convention’ amba oni mkataba wa kudhibiti kwa namna yoyote ile vilipuzi vinavyolenga wanadamu, na kuzitaka nchi zilizojiondoa kurejea tena. Ameonya kuwa kudhoofisha mikataba hiyo kutawaweka raia katika hatari zaidi, huku takribani watu milioni 100 tayari wakiwa hatarini duniani.
Akirejelea kaulimbiu ya mwaka huu, “Wekeza katika amani, wekeza katika hatua za kuondoa mabomu,” Katibu Mkuu mesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika kusafisha maeneo yaliyochafuliwa na mabomu, kuimarisha elimu ya tahadhari, kusaidia waathirika, na kupunguza akiba ya silaha.
“Lazima tuondoe kabisa tishio linalotokana na silaha hizi,” Guterres amesema akisisitiza lengo la kuhakikisha watu wote duniani wanaishi kwa usalama na matumaini.
Maadhimisho haya ya kila mwaka yanakumbusha mafanikio yaliyopatikana pamoja na kazi kubwa inayohitajika bado kufikia dunia isiyo na hatari ya mabomu ya ardhini.