Mfumo wa stakabadhi za ghala umeendelea kuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima, ukionyesha wazi kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa Katika msimu wa mwaka 2025/2026, mfumo huo umeingiza mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 90 kwa Mkoa wa Morogoro, hatua inayodhihirisha kuwa juhudi zikitiwa nguvu, matunda yake huwa ni ya kuridhisha.

Mafanikio hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima, wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mfumo huo ambapo amesema mapato hayo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 71 katika msimu uliopita hadi kufikia zaidi ya bilioni 90 na kusisitiza kuwa Mkoa umejipanga kuongeza uzalishaji zaidi ili kufikia mafanikio makubwa zaidi.

Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Cessilia Sostenes, ameeleza namna mfumo huo ulivyoimarisha ushirika na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima, hali inayowawezesha kunufaika zaidi na jasho lao pamoja na kukuza uchumi wa Morogoro kwa ujumla.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Denis Londo, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima na wafanyabiashara, huku ikihamasisha uwepo wa viwanda vyenye ushindani, akibainisha kuwa maendeleo hayaji kwa bahati bali kwa mipango thabiti.

Kwa upande wake, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amesisitiza juu ya usimamizi bora wa vyama vya ushirika ili kuendeleza mfumo huo kwa tija zaidi ili kuleta mabadiliko chanya kwa wakulima na uchumi wa taifa kwa ujumla.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *