Dar es Salaam. Kwa sasa D Voice kutokea WCB Wasafi, ni kati ya waimbaji wanaofanya vizuri katika muziki nchini akichanganya Bongofleva na Singeli, kitu kinachoonyesha ukubwa wa kipaji chake.
Akiwa na miaka miwili ndani ya lebo hiyo, tayari nyimbo zake zimepata mamilioni ya wasikilizaji katika majukwaa ya kidijitali na hivyo kuwa miongoni mwa wasanii wanaokua kwa kasi. Fahamu zaidi.
1. D Voice ni msanii wa nane kusainiwa na WCB Wasafi baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018) na Zuchu (2020).
2. Hata hivyo, tayari alikuwa ameshavuma katika singeli kupitia wimbo wake maarufu, Kuachana Shingapi (2021), na hata kushirikiana na wasanii wakubwa kama Barnaba na Nay wa Mitego.
3. Takribani mwaka mmoja na nusu baadaye, ndipo WCB Wasafi wakamtambulisha kupitia albamu yake, Swahili Kid (2023) yenye nyimbo 10, akiwa ni msanii wa kwanza wa lebo hiyo kutambulishwa kwa albamu.
4. Wasanii walioshirikishwa katika albamu hiyo ni wa WCB Wasafi pekee ambao ni Diamond Platnumz, Zuchu pamoja na Mbosso na Lava Lava ambao kwa sasa hawapo katika lebo hiyo baada ya kuondoka.
5. Ila Zuchu alipata upendeleo kwa sababu alishirikishwa katika nyimbo mbili – Nimezama na BamBam ambao ndio hasa uliofanya vizuri na kuibeba albamu hiyo, na hadi sasa video yake imeshatazamwa YouTube mara milioni 23.
6. Swahili Kid ni albamu inayojumuisha aina mbalimbali za muziki ikiwemo Singeli, Bongofleva, Amapiano, Afro Pop na Zouk, huku ikizungumzia kwa kina masuala ya kijamii, mapenzi na changamoto za maisha.
Huku D Voice alionyesha kipaji chake katika uandishi wa nyimbo na uimbaji akiwasilisha ladha mpya na ya kuvutia katika muziki wa Kiswahili, ladha inayoweza kuwagusa na kuwavutia mashabiki wengi.
7. D Voice ni msanii wa kwanza anayeimba miondoko ya Singeli kusainiwa na WCB Wasafi, rekodo lebo yake Diamond ambayo ndani ya miaka 10 tayari imewasimamia wasanii nane tena kwa mafanikio.
8. Tayari nyimbo zake zimesikilizwa (streams) mara milioni 100 katika mtandao wa Boomplay Music akiwa ni msanii wa 14 Tanzania kufanya hivyo, na wa kwanza kufikia rekodi hiyo akiwa na umri chini ya miaka 25.
9. Kolabo ya D Voice na Mbosso, Tunapendana (2024), ndio wimbo wa mwimbaji huyo uliofanya vizuri zaidi YouTube ambapo hadi sasa video yake imeshatazamwa zaidi ya mara milioni 30.4.
10. Hadi sasa ndani ya Bongofleva, msanii ambaye D Voice ameshirikiana naye mara nyingi zaidi ni Zuchu, mshindi mara sita wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), tena kwa misimu miwili pekee.
Wawili hao wametoa nyimbo sita; BamBam (2023), Nimezama (2023), Nani (2024), Hujanizidi (2024), Baby Mpya (2025) na Baridi (2026). Hapo nyimbo za D Voice ni tano, na wa Zuchu ni mmoja (Hujanizidi) kutoka katika albamu yake, Peace and Money (2024).