Dar es Salaam. Kwa wanamuziki wa zamani wa muziki wa bendi, sikukuu za kidini zilikuwa ni siku za mapato makubwa.
Katika miaka ya mwanzoni ya 1990, nilikuwa mwanamuziki wa Vijana Jazz Band, miaka hiyo bendi zilikuwa zikitegemea mapato kutokana na viingilio vya wapenzi wa muziki.

Ukumbi wetu kwa siku za Jumapili na sikukuu ulikuwa ukumbi wa Vijana Social Hall Kinondoni.  Siku za sikukuu kama vile Idd el Haji, Idd el Fitri, Pasaka, Krismas na mwaka Mpya zilikuwa siku ambazo ukumbi ulifurika.

Watu walikuwa wengi kiasi cha kulazimika kuweka milango mitatu tofauti ya kuingilia. Dansi letu lilianza sa tisa mchana na kwa kweli kufikia saa kumi na moja kulikuwa hakuna hata nafasi ya kutema mate. Uwingi ule wa watu kwa zama hizi ungechukuliwa kama tamasha lililofanikiwa.

Watu walikuwa wengi ukumbini kiasi cha watoto kupoteana na walezi au wazazi wao, na ilikuwa kawaida kutangaza mtoto kuonekana ukumbini hana wazazi au walezi  hivyo alipandishwa jukwaani na tangazo likatolewa kuwasaka walezi au wazazi wa mtoto huyo.  

Kutokana na uwingi wa wahudhuriaji wa maonyesho ya sikukuu, bendi nyingi zilitumia nafasi hiyo kutambulisha nyimbo zao mpya. Kwa vile bendi nyingi zilipunguza au kuacha kabisa kufanya maonesho katika kumbi mbalimbali.

Mwezi wa Ramadhani ulitumika kwa bendi kufanya mazoezi ya nyimbo mpya,  nyimbo mpya ambazo zilikuja kupigwa hadharani kwa mara ya kwanza siku ya Idd Mosi. Katika matangazo ya maonyesho ya Idd Mosi ,  matangazo yaligusia kuweko na nyimbo mpya.

Lakini siku za sikukuu ndipo pia bendi mpya zilipozinduliwa na kuna nyingine zilikufa mara baada ya onyesho moja au mawili yaliyofanyika wakati wa sikukuu.

Sikukuu ya Idd baada ya mwezi wa Ramadhan ilikuwa na changamoto yake, kwani  kuna bendi zilijikuta zinashindwa kufanya maonesho kwa kujikuta wanamuziki wake wamehamia bendi mpya wakati wa mwezi wa Ramadhani, au hata kuhamia bendi nyingine kongwe.

Ili kuepuka hali hiyo, Vijana Jazz Band tulikuwa tunakutana kama wiki moja kabla ya sikukuu, kujua hali halisi. Nakumbuka kuna wakati mmoja tulipokutana ikagundulika waimbaji wetu wawili walikuwa wamehamia bendi nyingine.Ikalazimika mazoezi ya kuziba pengo yafanyike haraka.

Nyakati hizo bendi kama ilikuwa ikimtaka mwanamuziki kulikuwa na vishawishi vingi, vikiwemo fedha taslim, au kupangiwa nyumba iliyo na samani, na mara nyingine kupewa mshahara mkubwa kuliko bendi uliyotoka na kulipa madeni yote kama alikuwa anadaiwa na bendi yake ya awali.

Mambo yako tofauti sana zama hizi. Kwanza maonyesho hayategemei kiingilio, iwe siku ya kawaida au siku ya sikukuu,  bendi zinalipwa na wafanyabiashara hasa ya pombe ili waweze kufanya maonyesho yao katika klabu zao.

Hivyo kupatikana au kukosekana umati wa  watu haiathiri pato la bendi lililokwishapangwa, japokuwa bahati mbaya mapato haya yako chini sana.
Kiongozi mmoja wa bendi ameniambia sikukuu hii bendi yake haitakuwa na maonyesho.

Tatizo kubwa ni kuwa bendi nyingi siku hizi hazina wanamuziki wa kudumu, wanakuwa vibarua tu ambao hulipwa siku bendi inapopanda jukwaani tu, hivyo mpigaji mmoja anaweza akapanda hata majukwaa ya bendi tatu tofauti kwa wiki.

Katika mfumo huo wapigaji wa vyombo hupandisha gharama zao za kukodishwa siku za sikukuu. Na mara nyingine  mwanamuziki anaweza kukubaliana na bendi moja lakini dakika za mwisho akiahidiwa fedha zaidi na bendi nyingine huacha kupokea simu za bendi ambayo makubaliano yalikuwa tayari.

Bendi inajikuta imeshapokea fedha za onyesho, wanamuziki wote wako jukwaani lakini mpiga solo hapokei simu. Bendi nyingi siku hizi  hazina mazoezi ya pamoja, na nyingi hazina nyimbo zake ambazo imetunga.

Hali hii imefanya bendi ziko nyingi lakini zote zinapiga fungu la nyimbo ambazo zote ni za bendi za zamani, na siku hizi si ajabu kukuta bendi ikipiga nyimbo maarufu za Bongofleva au hata nyimbo za Injili kwenye maonyesho yake.

Nikikumbuka viongozi wa bendi kubwa za zamani ambao waliweza kuendesha bendi zao na kutengeza nyimbo nzuri na kurekodi japo mara moja kila miezi sita, hakika najiuliza kwanini wanamuziki hawa wenye uwezo mkubwa wakishindwa kuja na nyimbo mpya miaka nenda miaka rudi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *