Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Bahari (IMO), Arsenio Dominguez, amesema kuwa hatua ya Marekani kuanza kuzuia kabisa Mlango Bahari wa Hornuz Iran kuanzia leo saa 10 asubuhi kwa saa za Mashariki mwa Marekani (EST) haijabadilisha sana hali iliyokwisha kuwa mbaya katika Mlango Bahari muhimu wa Hormuz.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari hii leo kuhusu kuanza kwa kizuizi kwenye mlango Bahari wa Hormuz Dominguez amesema “Sioni mabadiliko makubwa kwa sasa katika hali ilivyo. Kabla ya mgogoro, wastani wa meli 130 zilikuwa zikivuka kila siku, lakini katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia meli 11 tu ndani ya siku mbili. Kizuizi cha ziada hakibadilishi ukweli kwamba hakuna biashara ya kawaida katika Mlango Bahari wa Hormuz tangu kuanza kwa mgogoro.”

Maelfu ya mabaharia wamekwama baharini

Dominguez ametanabaisha kuwa zaidi ya mabaharia 20,000 na takriban meli 1,600 bado wamekwama ndani ya Ghuba ya Uajemi, wakikabiliwa na hali ngumu zisizo na suluhisho la haraka.

“Vizuizi zaidi havileti suluhisho kwa mgogoro huu tulionao,” amesisitiza, akionya kuwa hali hiyo inaendelea kuathiri mtiririko wa biashara ya kimataifa na usalama wa baharini.

Hatari ya mashambulizi yazidi kutishia usalama wa usafiri wa baharini

Akizungumzia hali ya usalama, kiongozi huyo wa IMO ameonya kuwa vitisho vya mashambulizi bado ni vikubwa na vinazuia meli kuvuka eneo hilo muhimu la kimkakati.

“Vitisho dhidi ya meli vinabaki kuwa halisi. Ndiyo maana ujumbe wetu umekuwa wazi tangu mwanzo, hadi hali tete itakapopungua na kuwa salama, hakuna meli inayopaswa kuvuka Mlango wa Hormuz,” amesema.

Sheria za kimataifa za bahari lazima ziheshimiwe

Dominguez pia amesisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa za usafiri wa baharini, akionya dhidi ya hatua zozote zinazokiuka uhuru wa usafiri.

“Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za bahari, njia za kimataifa za usafiri lazima ziheshimiwe. Nchi zote zinapaswa kuheshimu haki ya kupita bila madhara na uhuru wa usafiri wa majini. Hakuna utaratibu wa kisheria wa kutoza ushuru wa aina yoyote,” amesema kwa msisitizo.

Madhila ya kisaikolojia kwa mabaharia yaongezeka

Akizungumzia hali ya mabaharia waliokwama, Dominguez ameelezea athari kubwa za kibinadamu wanazokumbana nazo, ikiwemo uchovu, hofu na kutengwa na familia zao.

“Fikiria kuwa umekwama ndani ya meli kwa zaidi ya mwezi bila kusafiri. Kuna hofu ya upungufu wa mahitaji muhimu na tishio la kushambuliwa,” amesema.

Ameongeza kuwa “Hali hii inaathiri vibaya afya ya akili ya mabaharia, hasa kwa kuwa hakuna mabadiliko ya wafanyakazi na wanaendelea kufanya kazi wakisubiri hali irejee kuwa ya kawaida.”

Mazungumzo yaendelea huku juhudi za uokoaji zikifanyika

Katibu Mkuu huyo amebainisha kuwa anaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Iran na Oman, ili kuweka mfumo wa kuwawezesha meli kuondoka salama katika eneo hilo.

“Nimepewa jukumu la kuratibu mfumo wa uokoaji ili kuruhusu meli kusafiri. Mazungumzo bado yanaendelea, lakini hadi tutakapothibitisha kuwa ni salama, hatuwezi kuwaweka mabaharia katika hatari zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa bado hakuna taarifa rasmi kuhusu uwepo wa mabomu ya majini, lakini amesisitiza kuwa uthibitisho kamili utahitajika kabla ya kuruhusu usafiri wa meli kuendelea katika njia rasmi zilizowekwa tangu mwaka 1968.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *