Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Bi. Mohammed ameeleza jinsi zana za kidijitali—kuanzia akili mnemba hadi majukwaa ya afya mtandaoni—yalivyobadilisha upatikanaji wa elimu, huduma za afya, na takwimu za idadi ya watu. “Hasa, teknolojia imepanua huduma za afya ya uzazi hadi maeneo ya mbali na yasiyofikiwa kirahisi, na hivyo kutoa fursa mpya kwa maendeleo endelevu.”
Pengo la kidijitali kimataifa na kijinsia linaloongezeka
Hata hivyo, mafanikio haya hayajasambazwa kwa usawa. “Hali inaonesha mgawanyiko mkubwa kati ya nchi zenye kipato cha juu na zile zenye kipato cha chini: wakati asilimia 93 ya watu katika nchi tajiri wanatumia intaneti, ni asilimia 39 tu katika nchi zilizo nyuma zaidi kimaendeleo wanaofanya hivyo,” amesema Naibu Katibu Mkuu.
Amesema pengo hili linaonekana zaidi ndani ya jamii, hasa kwa misingi ya kijinsia. Katika nchi zenye kipato cha chini, ni asilimia 21 tu ya wanawake walio mtandaoni, jambo linalopunguza upatikanaji wao wa taarifa, huduma, na fursa za kiuchumi.
Hatari: Upendeleo, vurugu, na kutengwa
Athari mbayá za pengo hili la teknolojia ni pana, amesema kiongozi huyo akiongeza kuwa wanawake bado hawawakilishwi ipasavyo katika sekta ya teknolojia, wakichukua takriban robo tu ya nguvu kazi, hali inayozua wasiwasi kuhusu upendeleo wa kijinsia katika mifumo ya kidijitali.
Carine. mhandisi wa programu za kompyuta akiwa nyumbani kwao Kigali nchini Rwanda akitumia kishkwambi kukamilsha programu yake iitwayo Save and Save.
Wakati huohuo, majukwaa ya mtandaoni yanazidi kuhusishwa na unyanyasaji, upotoshaji wa taarifa, na vurugu za kijinsia, ikiwemo vitisho vipya kama picha zilizohaririwa na akili mnemba au AI, kwa lugha ya kiingereza “deepfakes”. “Changamoto hizi sio tu zinadhoofisha usawa, bali pia zinahatarisha afya na haki za wanawake.”
Zaidi ya upatikanaji: Nguvu,ushiriki, na ulinzi
Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa pengo la kidijitali halihusu tu upatikanaji wa vifaa au intaneti—linahusu pia nguvu, ushiriki, na ulinzi. Bila upatikanaji jumuishi, makundi yaliyotengwa yako katika hatari ya kuachwa nje ya mchakato wa kuunda teknolojia zinazogusa maisha yao moja kwa moja.
Kinachopaswa kufanywa |
|
Kuziba Pengo: Ili kukabiliana na changamoto hizi, Umoja wa Mataifa umetoa wito wa hatua za haraka na zilizoratibiwa kimataifa. Kipaumbele cha kwanza ni kuziba pengo la kidijitali kwa kupanua upatikanaji wa intaneti nafuu, kuwekeza katika elimu ya kidijitali, na kuhakikisha fursa sawa kwa wanawake na jamii zilizotengwa kushiriki katika uchumi wa kidijitali. Kusimamia teknolojia kwa uwajibikaji: Kuanzisha mifumo madhubuti ya usimamizi wa teknolojia inayozingatia haki za binadamu. Hii inajumuisha kudhibiti matumizi ya akili bandia, kushughulikia madhara ya mtandaoni, na kuhakikisha mifumo ya kidijitali ni wazi, ya haki, na jumuishi. Umuhimu wa Uwekezaji katika Utafiti: Kuwekeza katika utafiti, ikibainisha kuwa asilimia 90 ya fedha za utafiti duniani zinatumika katika nchi za G20. Kupunguzwa kwa bajeti za utafiti katika nchi zinazoendelea kunaweza kudhoofisha upatikanaji wa takwimu muhimu kwa ajili ya kupanga sera, hasa katika masuala ya idadi ya watu na maendeleo. |
Bi. Mohammed amekumbusha kuwa “teknolojia inaweza kuwa chombo chenye nguvu kwa manufaa ya wote, lakini tu ikiwa upatikanaji, usimamizi, na uwekezaji vitasimamiwa kwa usawa. Bila hatua madhubuti, mapinduzi ya kidijitali yanaweza kupanua zaidi pengo ambalo yana uwezo wa kulifunga.”
Tuhakikishe uendelezaji wa teknolojia unazingatia haki na usawa – Mwenyekiti CPD59
Mwenyekiti wa mkutano huo, Balozi Zéphyrin Maniratanga, amepazia sauti suala la pengo la teknolojia akisema mafanikio katika akili mnemba au AI, mifumo ya kidijitali, na teknolojia ya kibayolojia bado hayajafikia watu wote.
Akioanisha maudhui ya mwaka huu ya mkutano huo ambayo ni Idadi ya watu, teknolojia na utafiti kwa ajili ya maendeleo endelevu, Balozi Maniratanga ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Burundi kwenye Umoja wa Mataifa amesema, “ingawa maendeleo hayo yanabadilisha jinsi serikali zinavyoelewa na kukabiliana na mwenendo wa idadi ya watu na kuwa na uwezo wa kuboresha huduma za afya, elimu, na mipango ya kiuchumi huku ukiharakisha maendeleo endelevu bado hayajasambazwa kwa usawa.”
Balozi Maniratanga ameona pengo la kidijitali linaloongezeka kama changamoto kubwa, akibainisha kuwa “tofauti za upatikanaji wa teknolojia zinaakisi ukosefu mpana wa usawa katika uwekezaji wa utafiti na uwezo wa kisayansi. Bila msaada maalum, ubunifu unaweza kupanua badala ya kupunguza pengo hili.”
Amehimiza serikali na washirika wa kimataifa kuwekeza katika mifumo ya takwimu, kuimarisha miundombinu ya kidijitali, na kuhakikisha ushiriki jumuishi katika uchumi wa kidijitali. Halikadhalika, umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa faragha, usalama wa data, na matumizi ya kimaadili ya teknolojia.
“Ahadi ya teknolojia ni jambo kubwa sana,” amesema Balozi Maniratanga, “lakini tu ikiwa itaongozwa na usawa, haki za binadamu, na uwajibikaji wa pamoja.”