London, England. Klabu ya Chelsea FC imemfuta kazi kocha wake mkuu, Liam Rosenior, kufuatia mwenendo mbaya wa matokeo ndani ya klabu hiyo.

Uamuzi huo umechukuliwa leo Jumatano Aprili 22, 2026 baada ya Chelsea kupoteza michezo mitano mfululizo ya ligi bila kufunga hata bao moja, hali iliyozua shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki.

Rosenior anaondoka darajani hapo baada ya kudumu kwa chini ya miezi minne tangu alipoteuliwa kuchukua mikoba ya Enzo Maresca, licha ya kusaini mkataba wa miaka sita na nusu.

Aliyekuwa kocha wa Chelsea, Liam Rosenior akiwashukuru mashabiki uwanjani jana Aprili 21, 2026 baada ya kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Brighton.

Katika kipindi chake kifupi, Chelsea ilishindwa kuonyesha makali uwanjani, ikikosa ubunifu safu ya ushambuliaji na kuonekana kupoteza mwelekeo katika mbio za kuwania nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

Chanzo cha karibu ndani ya klabu kimeeleza kuwa uongozi haukuwa tayari kuvumilia mwenendo huo, hasa baada ya timu kushindwa kabisa kufunga katika mechi tano mfululizo, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa tangu 1912.

Aliyekuwa kocha wa Chelsea, Liam Rosenior akitoa maelekezo uwanjani katika moja ya mechi za timu hiyo.

Hali hiyo imeongeza presha kwa uongozi kuchukua hatua hiyo mapema ili kujaribu kuokoa mpango wa kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao. Pamoja na uamuzi huo, Chelsea imetoa shukrani kwa Rosenior na benchi lake la ufundi kwa mchango wao ndani ya kipindi walichokaa klabuni hapo.

Uongozi umeeleza kuwa Rosenior ameonyesha uadilifu, nidhamu na weledi mkubwa tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo. Baada ya kuondoka kwake, Chelsea imemtangaza Calum McFarlane kuwa kocha wa muda hadi mwisho wa msimu.

Kocha wa muda wa Chelsea, Calum McFarlane.

McFarlane atasaidiwa na benchi la ufundi lililopo huku jukumu lake likiwa kuiongoza timu katika kipindi hiki kigumu.

Kocha huyo anaondoka Darajani huku akiiacha timu hiyo ikiwa nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 48 baada yay a mechi 34.

Mbali na changamoto za ligi, chini ya kocha Rosenior, Chelsea pia ilishindwa kufanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiondolewa hatua ya 16 bora, na pia kuondolewa kwenye nusu fainali ya Carabao Cup.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *