
Nchini Nigeria, waendesha mashtaka wamewashtaki wanaume sita, akiwemo meja jenerali mstaafu, siku ya Jumanne, Aprili 21, kwa kujaribu kupanga mapinduzi mnamo mwezi Oktoba 2025. Hapo awali mamlaka ilikana madai hayo, huku jeshi likitangaza kuwakamata maafisa 16 kwa “masuala ya nidhamu.” Baadaye, Rais Bola Tinubu alifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa jeshi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Nigeria, njama hiyo inayodaiwa ilihusisha washukiwa zaidi ya 40, wakiwemo maafisa wa ngazi za juu. Lengo lilikuwa kushambulia na kuchukuwa udhibiti wa Aso Rock, ikulu ya rais, na kumkamata, au hata kumuua, rais Bola Tinubu na makamu wake wa rais, Kashim Shettima. Rais wa Baraza la Seneti na Spika wa Baraza la Wawakilishi pia wangililengwa. Kufuatia jaribio hili la mapinduzi, Rais Bola Tinubu alifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa jeshi.
Wanaume sita walishtakiwa rasmi mnamo Aprili 21 na mwendesha mashtaka wa umma. Wanatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama Kuu ya Abuja mapema leo Jumatano, Aprili 22. Miongoni mwa walioshtakiwa ni jenerali mstaafu, mkaguzi wa polisi, na raia.
Watu hao sita wanakabiliwa na mashtaka 13 kuanzia uhaini na ugaidi hadi kuficha taarifa na utakatishaji fedha. Wanashutumiwa, haswa, kwa kuwa na ufahamu wa njama iliyopangwa na Kanali Mohammed Alhassan Ma’aji, aliyetambuliwa kama kiongozi mkuu wa jaribio hili la mapinduzi.
Inadaiwa walikula njama “miongoni mwao kufanya kitendo cha ugaidi” na “kwa njia isiyo ya moja kwa moja, lakini kwa kujua” walitoa “msaada” kwa Kanali Ma’aji, kulingana na hati ya mashtaka. Watu wengine wanahusishwa katika kesi hiyo, akiwemo gavana wa zamani wa Jimbo la Bayelsa, ambaye kwa sasa hajulikani aliko, anayeshukiwa kufadhili njama hiyo.
Angalau maafisa wakuu 16, akiwemo Mohammed Alhassan Ma’aji, pia wamekamatwa. Kumi na wanne ni wa Jeshi la Nigeria, wengine ni wa Jeshi la Wanamaji na Jeshi la Anga. Wanajeshi hawa wanaweza kukabiliwa na mahakama ya kijeshi kwa kuhusika kwao katika njama hiyo inayodaiwa ya mapinduzi.
Inasemekana kwamba watu hao walipanga kuvamia ikulu ya rais ya Aso Rock na kumuua rais wa Nigeria, makamu wake, na rais wa Baraza la Seneti na spika wa Baraza la Wawakilishi.