Dar es Salaam. Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la Mwananchi umebaini kuwepo kwa mchezo wa ‘watu wa kati’ wanaolipia idadi kubwa ya fremu za maduka katika Stendi ya Daladala ya Mwenge, kisha kuzipangisha kwa gharama kubwa.

Mradi huo uliopo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ulianza kujengwa mwaka 2019 ukiwa na jumla ya fremu za maduka 138. Fremu hizo zilichukuliwa na wanunuzi tangu Novemba 2023 kwa njia ya mnada wa mtandaoni, kwenye mfumo unaojulikana kwa jina la Tausi.

Tausi ni mfumo wa kidijitali unaotumiwa nchini kwa ajili ya kusimamia na kurahisisha utoaji wa huduma za umma kwa njia ya mtandao.

Uchunguzi umebaini kuwa ‘watu wa kati’ wananufaika kwa kupata faida ya kila mwezi inayofikia Sh1,623,400 kwa kila fremu ya chini na Sh779,400 kwa ghorofani.

Mwandishi wa gazeti hili alifika katika soko hilo akijifanya mfanyabiashara anayehitaji fremu. Hata hivyo, alielekezwa kwa mmoja wa madalali maarufu, ambaye naye alimpeleka kwa mtu mwingine anayeelezwa ndiye anasimamia fremu zinazopangishwa.

Msimamizi huyo, aliyekuwa akiratibu ukarabati wa baadhi ya fremu, alimwonyesha mwandishi zile zilizobaki na kumtaka awahi kuzilipia, akieleza kuwa kuna watu tayari wameonyesha nia ya kuzikodi. Alisisitiza kuwa atakayelipia kwanza ndiye atakayepata.

Aidha, alimpa mwandishi namba ya akaunti ya kutuma fedha atakapokuwa tayari, huku akimfafanulia tofauti ya bei kati ya ile ya halmashauri na ile ya mmiliki wa kwanza.

Kwa mujibu wa msimamizi huyo, gharama rasmi za halmashauri ni Sh200,000 kwa mwezi kwa fremu za ghorofani na Sh300,000 kwa zile za chini. Hata hivyo, alieleza kuwa fremu zote zilishachukuliwa.

Aliongeza kuwa mmiliki aliyekwishazilipia fremu hizo kwa halmashauri, ndiye anazipangisha kwa Sh1,923,400 kwa kila moja ya chini na Sh979,400 kwa zile za ghorofani kila moja, ikiwa na ukubwa wa mita za mraba 26.

Mmoja wa madalali hao (jina linahifadhiwa) alisema licha ya gharama kuwa kubwa, upatikanaji wa fremu hizo bila kupitia kwa madalali, ambao hulipwa ada ya udalali sawa na kodi ya mwezi mmoja, si jambo rahisi.

“Fremu hizi unazoziona hapa zimechukuliwa na mtu mmoja. Ili kuzipata, ni lazima upitie kwa madalali kwa sababu huwezi kumpata mmiliki moja kwa moja,” alisema dalali huyo.

Kuhusu utaratibu wa malipo, mmoja wa wasimamizi alisema mpangaji anatakiwa kulipia miezi sita ya kodi mapema, kupitia akaunti atakayoelekezwa.

Alipoulizwa kwa nini malipo yanafanywa kwenye akaunti ya mtu binafsi ilhali fremu hizo ni za Serikali, alieleza mmiliki huyo tayari alishazilipia kwa halmashauri, hivyo ana haki ya kuziendesha kadri anavyoona inafaa, ikiwemo kuzipangisha.

“Mpaka sasa, kati ya zaidi ya fremu 40 anazomiliki, tayari nyingi zimeshachukuliwa na kulipiwa. Zilizobaki ni chache, na huenda zikachukuliwa ndani ya siku chache zijazo,” aliongeza msimamizi huyo.

Alipoulizwa kuhusu madai ya wapangaji kuwapangisha watu wengine kwa gharama kubwa, Mwanasheria wa Manispaa ya Kinondoni, Charles Lawisso amesema hana taarifa za kuwepo kwa wapangaji wanaowapangisha watu wengine kwa gharama kubwa Zaidi ya ile iliyowekwa na Serikali.

“Hatuna taarifa kama kuna wapangaji wanaowapangisha wengine kwa bei kubwa, isipokuwa tunaendelea kufuatilia ili kubaini ukweli wa suala hilo.”

Amefafanua kuwa mpangaji haruhusiwi kumpangisha mtu mwingine bila kupata kibali kutoka manispaa inayomiliki mradi huo.

Akizungumzia suala la baadhi ya wapangaji kutokuwa na mikataba kama ilivyobainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2024/25, inayobainisha kuwa wanaoshikilia fremu hizo hawana mikataba halali, Lawisso amesema kwa sasa tatizo hilo halipo kwani wote wana mikataba halali.

CAG kwenye ripoti yake anasema halmashauri hiyo ilipangisha fremu 88 kwa kipindi kuanzia  Oktoba 4, 2023 hadi Septemba 30, 2024, hata hivyo kuanzia Oktoba 1, 2024, mpangaji ameendelea kushikilia fremu hizo bila kuwa na mkataba halali.

Lawisso amesema aliyekuwa hajatia saini mkataba ni mwekezaji wa awali aliyeyaacha maduka hayo, lakini tayari amepatikana mwekezaji mwingine ambaye ana mkataba rasmi. Hivyo, suala la wapangaji kutokuwa na mikataba halipo tena.

Kuhusu mwekezaji kujenga upya katika eneo alilolichukua, Lawisso amekiri kulifahamu hilo, akieleza mwekezaji huyo alieleza tangu awali kuwa atajenga eneo hilo kulingana na mahitaji yake.

Kukaa bila wateja

Hata hivyo, kutokana na kupangishwa kwa bei kubwa, hali hiyo inaelezwa kuchangia fremu kukaa muda mrefu bila  watu na hivyo kuathiri mzunguko wa biashara katika eneo hilo.

“Baadhi tumeanza biashara hapa tangu tulivyoambiwa tufungue, lakini wenzetu hasa hao waliochukua fremu nyingi, hawazifungui, hivyo tunajikuta tupo wachache na kuathiri mzunguko wa biashara hapa,” amesema mmoja wa wafanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina moja la Doreen.

Wakati Doreen akisema hayo, Aprili 24, 2026 Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, alitoa tangazo akiwataka wafanyabiashara wote waliopanga fremu katika stendi hiyo, wawe wamezifungua ifikapo Aprili 30, 2026.

Tangazo hilo lililosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Halmashauri hiyo, Jamadi Omari, limeandikwa:

“Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni anawatangazia wafanyabiashara wote waliopanga katika fremu za biashara zilizopo kituo kipya cha mabasi cha Mwenge (ambao hawajalipa kodi za fremu au wamelipia na hawajazifungua) kuwa, wanatakiwa kuzilipia na kuzifungua kabla au ifikapo tarehe 30. 04.2026.

“Kushindwa kufanya hivyo, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni itazichukua fremu hizo na kuzitangaza upya kwenye mfumo wa Tausi kuanzia tarehe 01.05.2026, ili kuwapa fursa wafanyabiashara wengine wenye uhitaJi wa kufanya biashara katika eneo hilo.”

‘Tumeshapata chetu’

Ofisa Biashara, Philipo Mwakibete alisema walimiliki wa fremu hizo walizipata kupitia mnada wa wazi ulioendeshwa kwa mfumo wa Tausi, walizilipia na Serikali tayari imepata mapato yake.

 “Dhamira ya Serikali ni kukusanya kodi kwa ajili ya maendeleo, ndiyo maana ilikuja na mifumo hii. Mtu aliingia kwenye mfumo akaomba hata fremu zaidi ya mbili na akaingiza fedha za umma; hakuna kosa,” amesema Mwakibete.

“Stendi ya Mwenge kuna walioomba fremu zaidi ya mbili na wapo wanaofanya shughuli za biashara. Wenye fremu wote waliomba kupitia mfumo ambao hata watumishi hatuwezi kuingilia, kwani kuomba kunahitaji mtu aingize nywila yake,” amesema.

Hata hivyo, amekiri baadhi ya fremu ziko wazi baada ya kukubaliana na waliochukua kupisha kufanyika kwa maboresho ya ndani katika stendi hiyo, ikiwemo miundombinu ya lifti ambayo haikuwa inafanya kazi.

“Niwaondoe hofu wote waliopata fremu; haziwezi kuchukuliwa na yeyote na hakuna atakayenyang’anywa. Hali imebakia vilevile kwa walioshinda kwenye mnada wa Tausi, na kwa sasa wanapitia mikataba; kuna waliomaliza kulipa pango na wengine bado.”

Amesema kufungwa kwa fremu hizo hakumaanishi zimekosa wateja, bali ni kwa lengo jema la kupisha maboresho yanayoendelea kufanyika, ambayo yatadumu kwa muda mfupi kabla ya shughuli kuendelea.

“Wengi wamelipa pango; kuna waliolipa mwaka mzima, miezi sita na miezi mitatu. Mathalan, ghorofa ya kwanza imeshalipiwa yote, na waliochukua fremu moja moja kwa asilimia kubwa wamelipa. Wale ambao bado, tunaendelea kuwatengenezea control number,” amesema.

Utaratibu unaotumika kupangisha licha ya kukusanya mapato kwa usahihi, umelalamikiwa kuwa unaumiza wananchi wa kadaiwa.

 Rita Chacha amesema suala la watu wa kati linaumiza kwani Watanzania walio na vipato vya chini ni ngumu kupata fursa katika miradi hiyo ya Serikali ambayo inajengwa kwa kodi zao.

“Hata kama eneo awali lilichukuliwa na mtu kwa ajili ya kuweka maduka makubwa akashindwa, kwa nini lisigawanywe wakapewa wananchi wa kawaida wenye mahitaji na badala yake imemwachia mtu mmoja ambaye anapangisha kwa fedha anayotaka ambayo haiingii serikalini,” amesema Rita.

Alphonce Lema, amesema fremu zilizo  jirani na mradi huo zinazomilikiwa na watu binafsi gharama yake ni Sh500,000 na bado watu wa kawaida wana uwezo wa kuzikodisha licha ya kuwa ni ndogo ukilinganisha  na hizo za halmashauri.

Lema amesema ana imani nao pia wanaweza kupangisha hizo za Serikali, na fedha zikaingia humo badala ya mtu mmoja kujinufaisha nazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *