
Morogoro. Ni asubuhi na mapema Kijiji cha Iwemba Kata ya Kidodi, sauti ya mtoto mchanga inasikika ndani ya familia ya Kyambike.
Napokewa na mjamzito na mwenyeji katika nyumba niliyofikia, japo jina lake ni Furaha lakini uso wake hauoneshi kama mwenye furaha.
Sababu ya furaha yake kutoweka usoni, mwanaye ni mgonjwa na hana fedha za matibabu wala nauli ya kumfikisha hospitali japo ana umri chini ya miaka mitano.
Namdokeza kuhusu agizo la Serikali kwamba wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hupata matibabu bure, anasema jambo hilo halipo akisimulia zaidi namna alivyosubiri miezi miwili apate fedha kuanza kliniki.
“Nilipoanza kliniki nilitakiwa kwenda na fedha; na kiwango inategemea na mtu na mtu, mimi nilitakiwa kutoa Sh30,000 na hii niliambiwa ni kwa ajili ya vipimo,
“Ukishalipa fedha hizo, unaambiwa ukifika nyumbani andaa glovu, vifaa vingine ambavyo nitapaswa kuviwasilisha kliniki,” anasema.
Furaha anasema hakuwa na uwezo wa kulipa kiwango hicho cha fedha, hivyo alihangaika kuuza kuku wake ili kuanza kliniki japo kwa kuchelewa.
Anasema ni vyema Serikali kutekeleza agizo lake kwa kuwa wajawazito ni lazima kulipia huduma hospitali na kama asipotoa hela anapoumwa hupewa dawa za maumivu pekee.
Kisa hicho kinafanana na kile alichotozwa mkazi wa Kidodi wilayani Kilosa, Mariam Kiwembo (25) ambaye anakiri yeye alitozwa Sh15,000 ili kupata huduma.
“Nilijua matibabu ni bure, nilifika hospitali kuanza kliniki, nikaambiwa nikalipe sikuwa na fedha hivyo nilirudi nyumbani hadi nilipopata fedha hizo na kwenda kulipa,” anasema.
Anasema baada ya kufanyiwa uchunguzi hupaswa kwenda na kurudi, kwa mara nyingine na vifaa vya kujifungulia ikiwamo glovu, sinano, beseni na vitenge mambo ambayo anasimulia kuwa vinawakwaza.
Suala hilo la gharama kwa wajawazito huwa na madhara kwa kundi husika, Septemba 2024, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka alitoa siku tatu vyombo vya usalama kuchunguza tukio la mjamzito aliyepoteza maisha.
Mume wa marehemu Suleiman Makuani aliwasilisha malalamiko hayo kwa mkuu huyo wa wilaya akisema mkewe alicheleweshewa kupata huduma wakati akitaka kujifungua akitakiwa kulipia mafuta Sh180,000 gari la wagonjwa.
Baada ya kupambana kutafuta fedha hizo na kupata Sh100,000 na mkewe kuanza kusafirishwa tayari alishachelewa kupata huduma.
Mtoa huduma wa afya ngazi ya jamii Kata ya Biro, Wilaya ya Malinyi jina limehifadhiwa, anasema tangu 1994 amekuwa akitoa huduma kwa jamii bila kulipwa.
Miongoni mwa majukumu yake ni kuwashawishi wajawazito kuhudhuria kliniki ili wakajifungue salama lakini akikumbuka tukio lililobaki kichwani mwake hadi sasa.
“Alikuwepo mjamzito hakuwa na uwezo wa kumudu hata mlo wake wa siku, alitakiwa kwenda hospitali kuhudhuria kliniki, lakini kwa sababu hakuwa na fedha Sh20,000 ambazo zilihitajika alikaa nyumbani.
“Kwa kuwa wataalamu wanavyoshauri mama anapaswa kuanza kliniki mapema yeye alichelewa na alijifungua bila kupata msaada wa wataalamu, siku nakwenda kumsalimia namkuta ndani alitokwa na damu nyingi, katika kupiga kelele kuomba msaada muda haukuwa rafiki na mama alifariki,” anasema.
Mtoa huduma ya afya ngazi ya msingi Kata ya Biro, Jackline Paul anasema wakati wa Sikukuu ya Krismasi miaka ya nyuma, dada mmoja ambaye hakuwa vyema kiuchumi, alijifungulia nyumbani kutokana na kukosa fedha za kwenda hospitali.
“Nilipata taarifa hizo, nilikwenda nyumbani kwake asubuhi, nilikuta mazingira aliyojifungulia hayakuwa salama, nilimkagua kitovu cha mtoto jinsi ambavyo kilifungwa hakikuwa sawa,”anasema.
Mtoa huduma huyo anasema kwa kuwa hakukuwa na wakunga wa jadi wamepigwa marufuku kutoa huduma, alihangaika na mama huyo kumkimbiza hospitali kupatiwa huduma ya kwanza ili kumuepusha na maambukizi.
Anasema ni muhimu Serikali iangalie ni namna gani huduma za afya bure zitatolewa kama inavyoelekeza kuliko ilivyo sasa, wajawazito wanapofika hospitali hukumbana na changamoto na huacha kuhudhuria kliniki.
Mtaalamu wilayani Malinyi jina limehifadhiwa, anasema katika kukabiliana na kuwaepusha na changamoto za gharama wajawazito huwashawishi kujiunga na bima ya afya.
“Tulikuwa na bima CHF ambayo wanalipia Sh30,000, sasa walikuwa wakituambia tumeambiwa huduma za afya ni bure hawataki ila wengine wanakubali, sasa bima mpya inakuja ambayo watapaswa kulipia Sh150,000 sijui itakuaje kwa huku vijijini matibabu bure ni changamoto kwa sababu haiwezi kutekelezeka,” anasema.
Anasema kutokana na ugumu wa maisha wapo kina mama wakati mwingine hufika hospitali kusaka huduma za afya wakiwa wamebeba mayai au kuku kumpatia mtoa huduma ili apatiwe matibabu.
Kinachofanyika
Diwani wa Kidodi, Juma Nassoro anasema kwa kuwa sera ya afya inaelekeza matibabu bure, wanalisimamia hilo.
“Kwa kuwa sera imetekeleza matibabu bure kwa wajawazito sisi madiwani kupitia vikao vya Serikali za mitaa, tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi kutolipia huduma kwa wajawazito kwa kuwa ni maelekezo ya Serikali kupata matibabu bure,”anasema.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Betuel Joseph anasema katika kuwasogezea wananchi huduma za afya, Serikali ndani ya wilaya hiyo imejenga zahanati 59, vituo vya afya 13 na hospitali moja ya wilaya.
Sera ya afya inayoelekeza wajawazito kutibiwa bure tunaitekeleza ipasavyo, tunazingatia maelekezo hayo kwa kuhakikisha akina mama wanaipata haki hiyo bure,” anasema.
Anasema utekeelezaji wa sera hiyo ni rahisi kwasababu Serikali kuu imetenga fedha kugharamia wajawazito.
Pia, Serikali za mitaa kupitia idara ya afya, mkurugenzi huyo anasema wametenga fedha ambazo hupatikana kupitia makusanyo ya ndani ya halmashauri na hutumika kutoa huduma kwa kundi hilo.
“Mahitaji anayohitaji mjamzito ikiwamo vidonge vya kuongeza damu hivyo hutolewa bure, vingine vya kuwakinga na malari pia tunatoa bure, sasa dawa hizi tunazipata kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD),” anasema.
Anasema wakati mwingine baadhi ya vituo huelemewa na watu zikiwamo Kata ya Ruaha, Dumila huwa na idadi kubwa ya wakazi, hivyo wakati mwingine dawa hupungua kutokana na wingi lakini dawa huchukuliwa kwingine na kuwapatia.
Kuhusu wajawazito kutozwa fedha, anasema hawajapokea malalamiko yoyote na maelekezo yao kwa watumishi wa afya ni kutekeleza sera hiyo bure na endapo ikibanika mjamzito kutozwa fedha, hurejeshwa.
Hali mikoa mingine
Siyo Mkoa wa Morogoro pekee hata Dar es Salaam, mwaka jana wakati mkuu wa mkoa huo, Albert Chalamila akizungumza na wananchi wa Temeke alisimulia tukio la mjamzito aliyempigia simu akilalamika kutozwa fedha hospitali.
Chalamila alimuelezea mama huyo aliyempigia simu akilalamika kuambiwa na daktari atoe Sh50,000 ili inunulie vifaa vya kumsaidia kujifungua ikiwamo gloves; lakini Chalamila alimwambia asitoe fedha aende nyumbani akajifungue.
“Mama mmoja amenipigia simu eti baba nimeambiwa hapa hospitali wameishiwa gloves, wameishiwa vifaa vitakavyonisaidia mimi kujifungua wamesema nilipe 50,000 ili nichangie kwenda kununua vitu vitakavyonisaidia kujifungua,” anasema.
Chalamila anasema baada ya mama huyo kutokuwa tayari kununua vifaa akamwambia aende akajifungue nyumbani.
“Nikamwambia mama pole kwanza hiyo siyo haki toka nje chukua bajaji nenda zako nyumbani kamwambie mumeo achukue kisu na mikasi akusaidie kujifungua,” anasema.
Aidha anafafanua kuwa, lengo la kumwambia hivyo ni kwa sababu siyo nyakati zote vifaa vipo na pia kuna nyakati inabidi mgonjwa aangalie hali yake kwanza na namna ya kujisaidia kabla ya kulalamika.
Novemba 2023 mkoani Tanga iliripotiwa tukio la mjamzito kufia Kituo cha Afya Kabuku, wilayani Handeni kutokana na kile kilichodaiwa ni uzembe wa watumishi wa kituo hicho.
Ndugu wa mjamzito huyo walidai walitakiwa kulipa Sh150,000 fedha ambazo hawakuwa nazo na kusababisha ndugu yao kupoteza maisha hatua ambayo Waziri wa Afya wakati huo, alitoa amko la kuwataka watumishi wa afya kuzingatia maadili ya taaluma zao
Sera na miongozo
Wakati hali ikiwa hivyo, Sera ya Afya ya mwaka 2007, sehemu ya 5.3.4 kifungu (c) (i) Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inayotoa huduma bila faida, na mashirika ya kimataifa, itaendelea kutoa huduma bila malipo kwa; wanawake wajawazito, watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Pamoja na hayo, mkataba huu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni ambao Tanzania iliuridhia kuutekeleza 1976 unaeleza kwamba, nchi zilizoridhia mkataba huo zinawajibika kulinda haki ya kila mtu kupata viwango vya huduma za afya vinavyozingatia utu na ubora.
Mbali na hivyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 14, inaelekeza kuwa, kila mtu ana haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.
Pia, makubaliano ya viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika yaliyofikiwa Aprili 27,2001 mjini Abuja, Nigeria (Abuja Declaration, 2001) yakilenga kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika nchi wanachama ikiwamo Tanzania
Nchi hizo zimeahidi kutenga angalau asilimia 15 ya bajeti ya Taifa kwa sekta ya afya, kipaumbele kikiwekwa kuwa ni afya ya mamanamtoto.
Hata hivyo, Tanzania hutumia takribani kati ya asilimia 5 hadi chini ya asilimia 6 ya bajeti ya Taifa kwenye sekta ya afya jambo ambalo ni kinyume na azimio hilo.
Watetezi haki za binadamu
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga anasema suala la afya ya mama na mtoto linapaswa kupewa kipaumbele ya hali ya juu.
Anasema japo sera inaelekeza matibabu bure, lakini bado kuna changamoto
“Changamoto ni kwamba mafungu ya fedha hayafki kwa wakati katika hospitali zinazopaswa, hivyo kumesababisha kina mama kuambiwa wakanunue vifaa na kweli unakuta hospitali husika haina vifaa.
“Mwaka juzi kulitokea tukio la mama kuambiwa akanunue vifaa na ikashindikana na kupoteza maisha, huyo ni mfano tu lakini wapo wengi wanaopoteza maisha kwa sababu vifaa vinavyopasa kuwepo hospitali hazipo,” anasema.
Dk Henga anasema wataalamu wa afya wanaweza kulaumiwa, lakini kama hawana vifaa hawana jinsi ya kufanya.
“Vifaa vinavyopaswa kwenda hospitali za umma vinapaswa kwenda kwa wakati, yapo mambo mengi yanafanyika nchini ambayo sio kipaumbele.
Bajeti ya afya inapaswa kuongezeka kila mwaka ili kutatua changamoto hii na matumizi mengine yasiyo na msaada kwa maisha ya watu yanapaswa kupungua,” amesema.
Kilio cha watunga sera
Mei 16, 2025, aliyekuwa Mbunge wa Mbozi (CCM), George Mwenisongole, aliyehoji bungeni iwapo bado kuna utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007, inayotamka kuwa huduma za kujifungua kwa kina ma wajawazito zinapaswa kutolewa bure.
Katika swali lake la nyongeza, Mwenisongole pia aliuliza kuhusu hatma ya vifaa tiba vinavyoagizwa au kununuliwa kwa ajili ya huduma hizo, akitaka kujua vinakwenda baada ya wanawake kujifungua wa huduma za afya nchini.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya kipindi hicho, Dk Godwin Mollel akijibu swali hilo alisema Wizara ya Afya iko katika hatua za mwisho za kupitia upya sera hiyo kwa lengo la kufanya maboresho yatakayoiwezesha kuendana na mahitaji ya sasa na changamoto zilizopo katika sekta ya afya.
“Hata hivyo, kuanza kutumika kwa Bima ya Afya kwa Wote itakuwa suluhisho la kudumu la tatizo hili na kumaliza malalamiko ya wananchi,” alisema Dk Mollel.
Hatua za sasa
Akizungumza na Mwananchi Januari 10, 2026 juu ya hatua za Serikali kuhusu wajawazito kutozwa fedha, Waziri wa Afya, Omary Mchengerwa anasema Rais Samia Suluhu Hassan atatoa maelekezo wakati akizindua Bima ya Afya kwa Wote.
“Tunakwenda kwenye Bima ya Afya kwa Wote na itazinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni na kupitia uzinduzi huo atazungumza mengi, kwasasa tunachofanya ni kuhakiisha mifumo inasomana
“Ukiangalia sababu ya bima ya afya kushindwa kufanya kazi ni mifumo kutosomana na utegemezi wa sekta binafsi na sisi, kama Serikali tumedhamiria kuboresha, kusomana kwa mifumo sekta binafsi kutaondoa udanganyifu.
“Hili la wajawazito kutibiwa bure, linakwenda sambamba na sheria na tutahakikisha tunakwenda kutekeleza hivi karibuni, maelekezo atakayotoa Rais wakati akizindua Bima ya Afya kwa Wote itatoa mwanya sekta ya afya inakwenda wapi,” anasema.
Inaendelea kesho