BAADA ya kupigwa mechi sita za raundi 15 ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), ligi hiyo imesimama kwa siku takribani 18 hadi Mei 14 mwaka huu itakapoendelea.
Sababu ya kusimamishwa tena ligi hiyo ni kutokana na ratiba ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwenye kuwania kushiriki Fainali za Kombe la Dunia chini ya miaka 20 itakayoanza kupigwa Mei 2 hadi Mei 10, mwaka huu.
Ikumbukwe timu ya wasichana ya Tanzania, Tanzanite Queens ni miongoni mwa nchi zinazosaka nafasi ya kushiriki fainali hizo zitakazopigwa Poland mwaka huu.
Baada ya ratiba hiyo, WPL ikirejea zitapigwa mechi sita ikiwemo Dabi ya Kariakoo kati ya Simba Queens dhidi ya Yanga Princess, iliyopangwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, Mei 15.
Matokeo ya raundi ya 15, Simba Queens iliitandika Ceasiaa Queens bao 1-0, Fountain iliambulia kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya JKT Queens, Yanga Princess iliichapa Geita Queens mabao 2-1.
Alliance Girls iliambulia kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Mashujaa Queens, Tausi ikiwa nyumbani ilichapwa mabao 2-1 na Bunda huku Ruangwa Queens ikishindwa kufurukuta mbele ya na Bilo baada ya kutoka suluhu. Kwa matokeo ya mechi hizo, yanaifanya Simba Queens iendelee kusalia kileleni na pointi 43, Yanga Princess imebaki nafasi ya pili na pointi 39, huku JKT Queens ikisalia nafasi ya tatu na pointi 38.
Mashujaa Queens imesogea hadi nafasi ya nne ikikusanya pointi 26, Fountain baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya JKT Queens na Simba Queens, imeshuka hadi nafasi ya tano na pointi 20.