Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imefafanua mapendekezo yake kuhusu uwajibikaji, huku ikifichua wajumbe wake kupokea zaidi ya jumbe 300 za matusi baada ya kuwasilisha ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Pia, imependekeza kuwepo mkakati maalumu ili kukabili matukio ya kutekwa na kupotea kwa watu.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam leo Jumanne Aprili 28, 2026 Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman amesema ripoti yao imependekeza safu tatu za uwajibikaji;  uwajibikaji binafsi kwa aliyefanya kosa, uwajibikaji wa kiongozi au kamanda aliyekuwa anajua au alipaswa kujua kosa lililotendwa na aliye chini yake, pamoja na uwajibikaji wa taasisi.

Amesema hakuna aliyepinga suala la uwajibikaji na kwamba hilo ni mojawapo ya mapendekezo ya tume hiyo.

Uwajibikaji wa haki

Jaji Chande amesema wanachotaka wananchi ni uwajibikaji wa haki, hivyo walishauriana na baadhi ya viongozi waathirika waliowahoji na waliwapa maoni kuwa, anayestahili kuwajibika awajibishwe kwa mujibu wa sheria na asiyestahili asiwajibishwe.

“Wengine wakaenda mbali zaidi kwamba asitolewe mtu kafara kwenye kuwajibishana. Ushauri huo tuliupokea na ilibidi tusikilize pia maoni ya watu,” amesema Jaji Chande.

Safu tatu za uwajibikaji

Katika ripoti yao hiyo, amesema wamependekeza safu tatu za uwajibikaji, ikiwamo ya kuwajibika binafsi kwa mtu aliyehusika kutenda kosa la jinai au madai.

“Kwa polisi hili si jambo geni. Kwanza sheria inasema hivyo, kwamba askari polisi atakayesababisha kifo kwa kutumia silaha atawajibika yeye mwenyewe,” amesema.

Ameitaja safu ya pili ni kiongozi au kamanda kuwajibika, akifafanua kuhusu kiongozi kwa upande wa raia na kamanda kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.

“Hii ina vigezo vitatu. Huyo kiongozi au kamanda kwanza awe na uwezo wa kumuamuru au kumuamrisha au kumsimamia huyo wa chini yake aliyetenda kosa.

“Kwa sababu unamtuhumu kwa kosa sio aliyefanya yeye bali mtu wa chini yake, lakini yeye anabeba lawama na tuhuma sio lazima afanye yeye,” amesema.

Pia, amesema lazima kiongozi au kamanda huyo awe amejua kitendo kile alichofanya mtu wa chini yake au alipaswa ajue.

“Huwezi tu kumtuhumu kamanda au kiongozi, je alijua au alipaswa kujua kwa mazingira yale. Tatu, lazima ujue kuwa ameshindwa kuchukua hatua zote ambazo zinaweza kuchukuliwa ili kukinga,” amesema.

Safu nyingine ya uwajibikaji waliyoipendekeza ndani ya ripoti hiyo ni kwa taasisi.

“Sisi tunaongozwa na hadidu za rejea kubaini hoja kwa ngazi hii. Tume si jukumu lake kumtia mtu hatiani au kutamka kijinai,” amesema.

Jaji Chande amesema ushahidi wa tume pekee hautoshi kumtia mtu hatiani, lakini unafaa kuanzia upelelezi.

Kutekwa, kupotea watu

Akizungumzia kutekwa na kupotea kwa watu, amesema tume imebaini na imependekeza suala hilo kupewa kipaumbele na kuundiwa mkakati maalumu wa uchunguzi, kutokana na kubaini kesi nyingi huishia katika hatua ya upelelezi.

Hata hivyo, tume hiyo imeweka wazi kuwa, baada ya kuwasilisha ripoti Aprili 23, mwaka huu kwa Rais Samia baadhi ya wajumbe wake walipokea zaidi ya jumbe 300 za matusi, hali aliyosema ni hatari ya kuzima maoni yao.

Ufafanuzi wa tume hiyo, unakuja siku chache baada ya kuibuka baadhi ya vyama vya siasa ikiwamo ACT- Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vikiipinga ripoti hiyo kwa msisitizo wa umuhimu wa uwajibikaji kama njia ya kuponya majeraha.

Matukio ya utekaji

Katika ufafanuzi wake, Jaji Chande, amesema tume imebaini na kupendekeza suala la kutekwa na kupotea kwa watu lipewe kipaumbele na kuundiwa mkakati maalumu wa uchunguzi wa polisi, licha ya ukweli kwamba, jeshi hilo lina kazi nyingi.

Amesema ripoti yao imependekeza uchunguzi huo ufanywe kwa kina kwa kuanzia kwenye mizizi ya tatizo hilo ili kupata utatuzi sahihi.

“Tumeona kwamba, katika upelelezi unaoendelea wa kesi za kutekwa na kupotea kwa watu, pamoja na mafanikio ya kuwapata wenzetu waliopotea, waliojipoteza au waliotekwa, kuna umuhimu wa kuwa na mkakati maalumu wa kutatua,” amesema.

Pia, amesema tume hiyo imependekeza mamlaka kama itaridhia imtake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa ufanisi katika eneo la upelelezi wa kesi hizo.

Maelezo yake hayo, yametokana na rejea yake kuhusu taarifa ya kupotea na kutekwa kwa watu kama miongoni mwa vyanzo vya ghasia zilizotokea.

Akirejea ripoti ya polisi, amesema katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025 watu 758 walibainika kupotea kati yao asilimia 34 hadi sasa hawajapatikana.

Amesema katika idadi hiyo ya waliopotea 503 sawa na asilimia 66 wamepatikana, huku 265 sawa na asilimia 34 hawajapatikana.

Jaji Chande amesema kwa mwaka 2022 ripoti ya Chama cha Msalaba Mwekundu ilieleza waliopotea ni 216, waliopatikana ni 160 na ambao hawajapatikana ni 57.

Aidha, mwaka 2025 alisema waliopotea ni 237, waliopatikana ni 176, ambao bado hawajapatikana ni 61.

Jaji Chande amesema kuna makundi saba ya watu kupotea, ambayo ni kulipizana kisasi, uhalifu, kukwepa sheria, masuala ya kishirikina, kuondoka bila kutoa taarifa na masuala ya usafirishani haramu wa binadamu.

Pia, amesema duniani watu waliopotea kwa mwaka 2024 ni 288,000 na kwamba dunia nzima ina jumla ya viashiria 74 vya watu kupotea.

‘Kazi yetu kubaini hoja’

Jaji Chande amesema tume hiyo kazi yake ilikuwa kubaini hoja kutokana na ushahidi uliowasilishwa.

“Tume kazi yake ya msingi ilikuwa ni kubaini hoja na kubaini hoja ni ‘fact finding’ kutokana na ushahidi uliowasilishwa mbele ya tume. Kujibu zile hadidu za rejea tulizopewa,” amesema Jaji Chande.

Pia, amesema hadidu hizo za rejea ziliwataka kubaini chanzo, lengo la wahusika, nani wahusika, madhara ya kibinadamu kiuchumi, kijamii yaliyotokana na ghasia hizo na kubaini, kuzuia na kudhibiti kilichotokea.

Aidha, mwenyekiti huyo wa tume amesema ndani ya siku 153 ilizopewa kufanya kazi, kila siku ilikutana ana kwa ana na mashahidi 40.

Idadi hiyo ya watu iliyokutana nao kwa siku, alisema imefanya tume hiyo kwa siku zote 153 iwe imekutana na jumla ya watu 6,205 ana kwa ana.

“Tume hii, imekutana ana kwa ana na watu 6,205. Sasa jiulize tume gani kwa siku 153 imekutana ana kwa ana na watu 6,205; hakuna duniani. Sisi tumesikiliza mashahidi na kuhojiana na watu 40 kwa siku moja,” amesema.

Kwa nini hawakutajwa watu

Akifafanua kuhusu tume hiyo kutotaja majina ya watu hadharani, mjumbe wa tume hiyo, Profesa Ibrahim Juma amesema kutaja watu ni uvunjaji sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.

Amesema kwa sababu hiyo, tume ilishindwa kuruhusu ushahidi utolewe hadharani, ndiyo maana baadhi ya mashahidi walisikilizwa kwa faragha kwa kuwa walikuwa wanataja majina ya watu.

“Ukiruhusu majina ya watu yatajwe hadharani na humpi muhusika nafasi ya kusikilizwa, tayari kuna uamuzi wa Mahakama Kuu, kwenye nchi nyingine inakataza jambo kama hilo,” amesema Profesa Juma.

Wapokea jumbe za matusi

Profesa Juma amesema baada ya kuwasilisha ripoti kwa Rais Samia, baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wamepokea jumbe zaidi ya 300 za matusi.

Amesema kitendo hicho, kinaashiria kwamba, Tanzania kwa sasa kumezuka tabia aliyoiita hatari ya watu kuzima maoni ya wengine, huku wakitaka ya kwao pekee ndio yasikilizwe.

Tabia hiyo, amesema imedhihirika hata baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya tume hiyo, baadhi ya wajumbe wamepokea jumbe za matusi katika simu zao ili kuzima maoni yaliyowasilishwa kupitia ripoti.

“Baada ya taarifa kutoka tumepokea matusi zaidi ya 300 kwa sababu kuna mtu hataki maoni yetu yaliyopatikana kwa njia ya methodolojia ya kusikiliza watu yasiwafikie watu,” amesema.

Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, ambaye pia ni mjumbe wa tume hiyo, Said Mwema amesema katika watu zaidi ya 63,000 waliokutana nao, baadhi walikiri kushawishiwa kushiriki kwa ahadi ya maisha mazuri baadaye.

Amesema hiyo ndiyo sababu inayoifanya tume hiyo, ione kuwa, ghasia hizo ziliratibiwa na kupangwa.

Mwema amesema kuna wafanyabiashara walioulizwa kipato chao kwa siku, wakaahidiwa kupewa zaidi lakini wafanye kazi maalumu na jambo likifanikiwa mambo yatakuwa mazuri zaidi.

“Pia, matukio, picha na ushahidi mwingine ulituonesha kabisa zilipangwa mbinu zaidi ya 16 ili jambo hili lifanikiwe. Kuna maeneo 202 yalitokea kwenye kadhia hii, polisi wakazidiwa,” amesema.

Kwa nini JWTZ

Akifafanua kuhusu kuwepo kwa askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi (JWTZ) siku hiyo mtaani, mjumbe wa tume hiyo, Luteni Jenerali Balozi Paul Mella amesema jeshi hilo lilikuwa likifanya kazi kwa kushirikiana na vyombo vingine kudhibiti vurugu.

Hata hivyo, amesema hilo ni takwa la kisheria linaloliruhusu JWTZ kwenda kusaidia mamlaka na wanapokwenda wanafanya kazi kwa kushirikiana na inayofanana na polisi.

Balozi Mella amesema kanuni za majeshi ya ulinzi pia, zinafafanua namna jeshi hilo linavyopaswa kufanya kazi yanapotokea matukio kama hayo.

“Kama mnasikia maswali kwamba ilikuwaje wanajeshi wakawepo basi sababu ni hiyo. Na sheria hizi sio Tanzania pekee hata huko duniani zipo,” amesema Balozi Mella.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *