COASTAL Union ipo kambini ikiendelea kujipanga na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Black Stars, huku kocha wa Wagosi hao, Fikiri Elias, akifunguka namna anavyotaka kuwakabili wapinzani wao.

Akizungumza na Mwanaspoti, FIkiri alisema bado maandalizi yao yanaendelea kabla ya kuwakaribisha Singida Black Stars kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Fikiri alisema kwa sasa anaendelea kuimarisha namna ya timu kucheza kwa nidhamu kubwa kutokana na aina ya timu wanayokwenda kukutana nayo kuundwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa.

“Tunaendelea na maandalizi, nashukuru Mungu vijana wameendelea kuimarika, tunajipanga kukabiliana na Singida wanaokuja hapa kwetu, tunataka kuendelea kushinda lakini ni lazima tujue tutakutana na timu ngumu,” alisema Fikiri.

Fikiri aliongeza Singida ina washambuliaji wazuri ambapo hesabu itakuwa kuimarisha safu ya ulinzi isiruhusu bao huku akiridhishwa na namna maandalizi yanavyokwenda.

“Ni kweli Singida ina washambuliaji wazuri tumeona, lakini naridhishwa na namna tunavyoendelea kujipanga na mabeki wangu wanaimarika, naona kuna mwanga mzuri wa kuweza kuwadhibiti,” alisema.

Fikiri amerejea vizuri Coastal Union ambapo katika mechi mbili za kwanza ameshinda zote akiifunga Pamba Jiji kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB, lakini pia akiifunga Dodoma Jiji mabao 3-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Coastal Union ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 19 baada ya kushinda mechi nne, kutoa sare saba na kupoteza mechi nane, ikifunga mabao 16 na kuruhusu 22, wakati Singida Black Stars ni ya nne na pointi 29.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *