
Katika chapisho jipya liitwalo “Kuimarisha Uadilifu wa Taarifa: Matangazo, Akili Mnemba na Janga la Taarifa Duniani”, Idara ya Umoja wa Mataifa ya Mawasiliano ya Kimataifa na Mtandao wa Matangazo uitwao Conscious Advertising Network wanaonya kuwa matumizi ya AI bila udhibiti katika sekta ya matangazo yanaongeza hatari katika mfumo mzima wa taarifa za kidijitali.
Nguvu ya fedha kwenye mustakabali wa matangazo
Muhtasari huo wenye kurasa 32, unaeleza kuwa sekta ya matangazo ipo katikati ya namna taarifa zinavyosambaa mtandaoni, huku maamuzi ya matumizi ya fedha yakiamua ni maudhui yapi yanazalishwa, kusambazwa na kuingiza mapato.
Kadri zana za AI zinavyozidi kutumika katika ununuzi wa nafasi za matangazo na utengenezaji wa maudhui, hali hiyo inaendelea kuongezeka.
“Mfumo wa matangazo unafadhili mifumo inayounda kile watu wanaona, kuamini na kukubali,” amesema Mshauri Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uadilifu wa Taarifa, Charlotte Scaddan.
“Bila hatua za haraka na mifumo ya udhibiti, AI inaweza kuharakisha kudorora kwa uadilifu wa mfumo wa taarifa. Watangazaji wana uwezo wa kusaidia kurekebisha hali hiyo,” amesema Afisa huyo.
Muhtasari huo unaonesha hatari kadhaa zinazoongezeka, ikiwemo kuenea kwa taarifa potofu, hotuba za chuki na maudhui yanayogawanya jamii, huku mapato ya matangazo yakiendelea kufadhili maudhui hayo bila kujali ubora au usahihi wake.
Halikadhalika, ukosefu wa uwazi katika mifumo ya matangazo inayoendeshwa na AI unazua wasiwasi kuhusu udanganyifu na matumizi yasiyo na ufanisi.
Aidha, kuongezeka kwa maudhui yanayotengenezwa na AI kunatishia uhai wa vyombo huru vya habari, huku kupungua kwa imani ya watumiaji katika mazingira ya kidijitali kukidhoofisha ufanisi wa kampeni za matangazo.
Ni jambo gani la kufanya?
Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa watunga sera kuoanisha mifumo ya usimamizi wa AI na matangazo na viwango vya kimataifa vinavyozingatia maadili ya wa taarifa, pamoja na kushirikiana na sekta binafsi na asasi za kiraia kuongeza uwazi.
Kwa upande wa kampuni za matangazo ya biashara, wanahimizwa kudai uwazi zaidi katika mnyororo wa AI, kuipa kipaumbele mazingira ya maudhui yenye ubora, na kutumia nguvu ya kifedha kushinikiza majukwaa ya kidijitali kuweka ulinzi madhubuti kwa watumiaji.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa uwazi zaidi unaweza pia kuongeza ufanisi wa matangazo, ikithibitisha kuwa uwajibikaji unaweza kwenda sambamba na mafanikio ya biashara.