Kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini D’Njamena na Geneva WFP imesema mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 28 anatarajiwa kutumia ushawishi wake miongoni mwa vijana, mashabiki wa michezo na jamii mbalimbali barani Afrika kuhamasisha kuhusu athari za njaa kali pamoja na umuhimu wa usalama wa chakula na lishe.

Betel aahidi kusaidia lishe ya vijana

Akizungumza baada ya uteuzi huo kutangazwa mjini N’Djamena, Betel amesema lishe bora na maisha yenye afya ni mambo muhimu katika kuwasaidia vijana kufikia mafanikio katika michezo, elimu na maisha kwa ujumla. 

Ameipongeza WFP kwa programu zake zinazosaidia watoto na familia zinazokabiliwa na uhaba wa chakula na migogoro ya kibinadamu.

“Chakula, lishe na maisha yenye afya ni muhimu kuwasaidia vijana kufikia uwezo wao kamili katika michezo, elimu na kila nyanja ya maisha,” amesema Casimir Betel. “Programu za chakula shuleni na lishe zinazowasaidia vijana tangu utotoni hadi kipindi cha shule zinanigusa sana, pamoja na programu za dharura na za muda mrefu zinazohakikisha familia zinapata chakula wakati wa migogoro na baadaye kujitegemea. Ninafurahi kufanya kazi na WFP nchini Chad.”

Mafanikio ya kimataifa yaongeza umaarufu wa Betel

Kati ya mwaka 2019 na 2025, Betel alishinda medali 18 za kimataifa, zikiwemo medali 12 za dhahabu na sita za shaba katika mashindano ya Afrika na kimataifa ya taekwondo.

Ushindi wake wa hivi karibuni katika Kombe la Rais wa Ethiopia na mashindano ya Slovenia Open mwaka 2025 umeimarisha hadhi yake kama mmoja wa wanamichezo bora wa Chad. Kwa sasa mwanataekwondo huyo anajiandaa kwa mashinadano ya 2028 ya Olympiki ya majira ya joto yatakazofanyika Los Angeles Marekani.

Maafisa wa WFP wanasema mafanikio na umaarufu wake vinamfanya kuwa balozi mwenye ushawishi mkubwa kwa vijana huku akihamasisha kuhusu changamoto za njaa na lishe zinazoathiri jamii zilizo hatarini.

WFP Yasema Ushirikiano Utawavutia Vijana

“Tuna furaha kufanya kazi na Casimir Betel, na ninaamini kuwa utetezi wake wa kuboresha uhakika wa chakula na lishe utawagusa maelfu ya vijana na mashabiki wa michezo wanaomchukulia kama mfano wa kuigwa,” amesema Sarah Gordon-Gibson, Mkurugenzi wa WFP nchini Chad. “Ana dhamira ya kweli na shauku ya kuhamasisha kuhusu kazi ya WFP, na atasaidia kwa kiasi kikubwa kueleza umuhimu wa chakula na lishe katika kuandaa kizazi kijacho cha mabingwa wa Chad.”

Ushirikiano huo unakuja wakati WFP ikiendelea kutoa msaada wa dharura wa chakula kwa watu walio katika mazingira magumu nchini Chad huku pia ikifanya kazi na serikali pamoja na washirika wa maendeleo kuimarisha suluhisho endelevu la uhakika wa chakula na maendeleo ya rasilimali watu.

WFP yaendelea kutumia michezo kuongeza uhamasishaji

WFP imesema kushirikisha wanamichezo mashuhuri na watu maarufu ni sehemu ya juhudi kubwa za kuongeza uelewa kuhusu njaa, utapiamlo na umuhimu wa kuwekeza kwa vijana. Kupitia programu za chakula mashuleni, msaada wa lishe na miradi ya kujenga mnepo, WFP inalenga kusaidia jamii kujikwamua kutokana na migogoro huku ikijenga njia endelevu kuelekea utulivu na ustawi. WFP inaendelea kuwa shirika kubwa zaidi duniani la misaada ya kibinadamu linalookoa maisha wakati wa dharura na kusaidia jamii zilizoathiriwa na migogoro, majanga ya tabianchi na majanga mengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *