
Iran imelaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea katika eneo la Sayyida Zainab mjini Damascus, ambalo limepelekea kuuawa shahidi Sayyid Farhan Hassan Al‑Mansour, mmoja wa wanazuoni wa Kiislamu na khatibu wa Ijumaa katika Haram ya Bibi Zainab (AS).
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baqaei, ameeleza kusikitishwa sana na uhalifu huo na kusema: “Mashambulio ya kigaidi dhidi ya maeneo matakatifu na wanazuoni wa dini nchini Syria na katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa ujumla ni sehemu ya njama mbaya za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinazolenga kuchochea fitina na kuibua mgawanyiko. Ni muhimu kwa pande zote kuwa macho dhidi ya njama hizi na kuchukua hatua madhubuti katika kupambana na ugaidi na itikadi kali.”
Akituma salamu za rambirambi kwa familia ya mwanazuoni huyo aliyeuawa shahidi, pamoja na wananchi na jamii ya wanazuoni nchini Syria, Baqaei amesisitiza umuhimu wa kuwatambua na kuwaadhibu wahusika wa shambulio hilo na kuimarisha ushirikiano wa nchi za eneo hilo ili kung’oa mizizi ya ugaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amesisitiza wajibu wa serikali ya mpito ya Syria katika kuhakikisha usalama wa raia, wanazuoni na makundi yote ya kikabila na kidini nchini humo.
Vyombo vya habari vya Syria viliripoti Jumamosi, kwamba Sayyid Farhan Hassan Al-Mansour alifariki dunia kutokana na majeraha aliyopata katika shambulio la guruneti baada ya kukimbizwa hospitalini katika eneo la Sayyidah Zainab (SA) mjini Damascus.
Alikuwa Imamu wa Swala za Ijumaa katika haram hiyo yenye kaburi la mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Sayyidah Zainab binti Ali bin Abi Twalib (AS).