Dar es Salaam. Katika  Bongofleva waimbaji wa kike ni wachache, na walioweza kufanya vizuri kwa muda mrefu tena kwa ubora uleule ni wachache pia, mmoja wao ni Faustina Mfinanga maarufu kama Nandy.

Akiwa na miaka 10 tangu aanze kuvuma kwa mara ya kwanza kimuziki, Nandy amefanya mengi kimuziki ikiwa ni pamoja na kutoa albamu, EP tatu, kushinda tuzo za ndani na nje. Fahamu zaidi.

1. Kabla ya Nandy kusikika kimuziki hasa chini ya Tanzania House of Talent (THT), aliwahi kuwa mmoja wa waimbaji kwenye bendi ya Banana Zoro, B Band kwa kipindi fulani.

2. Wimbo uliomtoa Nandy kimuziki, Nagusagusa (2016), uliandikwa na mtayarishaji wa wimbo huo, Ima The Boy. Awali wasanii kadhaa walipatiwa wimbo huo na kushindwa kuutendea kazi, miongoni mwa wasanii hao ni Recho wa THT.

3. Willy Paul kutoka nchini Kenya ndiye msanii wa kwanza kutoka nje ya Tanzania kumshirikisha Nandy katika wimbo wake, na hadi sasa wawili hao wamekutana katika kolabo tatu.

4. Nandy hakuwahi kushinda tuzo yoyote Tanzania hadi pale aliposhinda tuzo ya All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017, zilizotolewa Nigeria ambapo alishinda katika kipengele cha Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki.

5. Baba mzazi wa Nandy alionekana katika video ya wimbo wa mwanamuziki huyo, One Day (2017), lakini wazazi wake wote walikuja kuonekana katika video ya kolabo yake na mumewe Billnass, Bye (2022).

6. Katika video za nyimbo mbili ambazo Nandy ameshirikiana na Willy Paul, zote Nandy amecheza kama video vixen na mwimbaji pia. Nyimbo hizo ni Njiwa (2018), na Hallelujah (2019), ambazo sehemu ya Nandy iliandikwa na Jay Melody.

7. Kipindi anaanza kupata umaarufu, Nandy alipoulizwa ni nani mshindani wake katika muziki, alimtaja Maua Sama ambaye walikuwa wote katika kundi la The Butterflies. Je, ni namna gani tunaweza kupima ushindani wao? Mwishoni mwa 2017, Nandy alikuwa msanii pekee wa kike Afrika Mashariki kushinda tuzo ya AFRIMA, na mwaka uliofuata Maua Sama alikuwa msanii pekee wa kike Tanzania kuchaguliwa kuwania tuzo hizo.

8. Katika remix ya wimbo wa Ben Pol, Bado Kidogo (2018) ambayo iliwakutanisha wasanii 11, Nandy ndiye msanii pekee wa kike katika wimbo huo. Hii ni baada ya Ben Pol kutokea kama ‘King Video’ wa wimbo wa Nandy, Wasikudanganye (2017). Wasanii wengine waliokuwepo katika remix ya wimbo huo ni pamoja na Joh Makini, Jux, Fid Q, Barnaba, Roma, Billnass, Willy Paul na Wyse.

9. Aslay ndiye msanii pekee aliyeshirikishwa kwenye albamu ya kwanza yake Nandy, African Princess (2018) chini ya Epic Records, ambayo ilitoka ikiwa na nyimbo 11.

10. Baada ya mwanamuziki Papii Kocha kutoka jela kwa msamaha wa Rais John Magufuli, kwa mara kwanza alikaribishwa katika shoo aliyokuwa akifanya Nandy na Aslay. Papii Kocha na baba yake, Babu Seya walitoka jela Desemba 9, 2017 na usiku wa Februari 17, 2018, ndipo Papii Kocha alipanda jukwaani kwa mara ya kwanza, na ni katika shoo hiyo ya Nandy.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *