
Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na bila usumbufu wa kutembea umbali mrefu, mahakama ya Tanzania inatarajia kuanza ujenzi wa mahakama ya wilaya ya Momba Mkoani Songwe kwa gharama ya Sh1.8 bilioni.
Akizungumza eneo itakapojengwa mahakama hiyo wakati wa kumkabidhi mkandarasi atakaye jenga jengo hilo kutoka Kampuni ya SCORPION LIMITED Mei 4, 2026 Jaji Mkuu Mfawidhi wa mahakama kuu masijala ndogo ya Songwe Jaji Gabriel Malata amesema ujenzi wa Mahakama hiyo utasaidia kusogeza huduma kwa wananchi na kuboresha mazingira ya utoaji haki.
Malata amesema kwa sasa wilaya ya Momba haina jengo la Mahakama ya wilaya kwani wanalotumia sasa wamepanga hivyo kutumia gharama kubwa kulipa kodi ya pango kila mwezi.
Amesema licha ya wilaya ya Momba kuwa na halmashauri mbili hakuna hata Halmashauri yenye jengo la mahakama kitendo ambacho serikali imeona ni vyema kutoa fedha hizo kujenga jengo la mahakama ya wilaya ya Momba katika kata ya Chapwa eneo ambalo lilitolewa na Halmashauri ya mji wa Tunduma.
“Jengo litakalojengwa litakuwa na sehemu tofauti tofauti ikiwepo jengo la mahakama ya wilaya, mahakama ya mwanzo, mahabusu ya kike na kiume pamoja na vyoo, ambalo ni tofauti na jengo linalotumika sasa”, amesema Jaji Malata.
Amesema ujenzi wa mradi huo wilaya ya Momba litasaidia wananchi kupata haki za kimahakama karibu kwani kwa mda mrefu wilaya hiyo haikuwa na jengo la mahakama ya wilaya, walikuwa wanapanga nyumba na kuzigeuza kuanza kutumika kama mahakama.
“Sisi kama mahakama tunatarajia kuanza kutoa huduma za kimahakama Januari 2027 hivyo mkandarasi ufanye kazi usiku na mchana na kuzingatia masharti ya kimkataba ndani ya miezi minane iwe imekamilika,” amesema Jaji Malata.
Aidha amesisitiza Halmashauri kutenga maeneo ya kujenga mahakama za mwanzo katika kata za Mpemba na Kamsamba ambayo yamekuwa na wingi wa wananchi ambao wanahitaji huduma za kimahakama.
“Naishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluh Hassani kwa kuidhinisha fedha kiasi cha Sh1.8 bilioni kujengea mahakama hiyo kwani lilikuwa hitaji la wananchi wa Momba kwa mda mrefu,” amesema Jaji Malata.
Mkuu wa wilaya ya Momba Elius Mwandobo amesema licha ya ukubwa wa Wilaya hiyo haikuwa na jengo la mahakama kwani linalotumika sasa ni finyu na halina hadhi ya kimahakama kwa ajili ya kuhudumia wananchi kupata haki za kisheria.
“Mwandobo amesema ujenzi huo pindi utakapokamilika utasaidia mahakama kuondokana na adha ya kukodi jengo lisilo na sifa za kimahakama kutoa huduma kwa wananchi kwani uhitaji wa mahakama ni mkubwa wilayani humo,” amesema Mwandobo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa itakapojengwa mahakama hiyo, Mkandarasi kutoka kampuni ya SCORPION LIMITED ambaye ni mkurugenzi wa kampuni hiyo Wilson Ezekiel amesema atahakikisha anajenga jengo hilo kwa viwango kulingana na mahitaji yaliyopo kwenye makubaliano ya kimkataba.
Akizungumzia ujenzi wa mahakama hoyo Christopher Simbeye mkazi wa kata ya Chapwa amesema serikali imefanya jambo la maana ujenzi wa mahakama kwani awali walipanga jengo ambalo halikidhi kutoa huduma.
“Naishukuru sana serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za kimahakama, hivyo kama wananchi tunaomuomba mkandarasi ajenge haraka kulingana na mkataba na wao watashirikiana kulinda vifaa vya ujenzi,” amesema Simbeye.