Mwanza. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ametoa maelekezo kwa watumishi wa sekta ya afya nchini, akisisitiza umuhimu wa kuboresha huduma kwa kuzingatia utu, nidhamu, uwajibikaji na maandalizi ya utekelezaji wa sera mbalimbali katika sekta hiyo.

Ametoa maagizo hayo jana, Mei 3, 2026, wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya jijini Mwanza, akisisitiza sekta ya afya inapaswa kujengwa kwa misingi ya huduma bora kwa wananchi, si taratibu pekee.

“Tunataka kujenga Wizara ya Afya ya aina gani? Wizara ya majengo makubwa bila moyo? Au wizara yenye utu, nidhamu, weledi na uadilifu… inayomwona mgonjwa si kama faili, bali binadamu,” amehoji Mchengerwa.

Vifo vya mama na mtoto

Katika kikao hicho, Mchengerwa amesema inawezekana kupunguza na kuvimaliza kabisa vifo vya mama na mtoto, akitaja idadi ya vifo 57,000 vya vichanga kila mwaka, huku zaidi ya kinamama 2,330 wakifariki kwa mwaka.

“Hatuwezi kufurahia wala kufanya sherehe kwa namba hizo. Ukweli ni kwamba bado tunazungumzia kila mwaka, kinamama zaidi ya 2,330 wanakufa kwa uzembe au kukosa huduma karibu, au kuwepo huduma za ubabaishaji kwenye vituo vyetu, dawa hakuna au tumechelewa kuwasaidia wakati wa uzazi,” amesema.

“Zaidi ya watoto 57,000 wanakufa katika vituo vyetu kwa mwaka kwa sababu ya uzembe, kuchelewa kuwahudumia wajawazito, kukosa huduma kadhaa ikiwa ni pamoja na huduma za dharura kwa watoto wachanga,” amesema.

Akisisitiza hilo, amesema: “Lakini hasa inachangiwa na uzembe. Sehemu kubwa ni uzembe wa kutowahudumia wazazi hawa wanapokuja kwenye vituo vyetu. Wakati wangu, namba hizi jitahidi tubaki kwenye ‘single digit’ na tuamue kwa pamoja, inawezekana kabisa.”

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza na watumishi wa afya jijini Mwanza katika baraza lao kuu la wafanyakazi.

Motisha kwa watumishi

Mchengerwa amesema Serikali imeanza hatua za kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi kupitia mpango maalumu wa motisha unaolenga kuongeza ari na ufanisi katika utoaji wa huduma.

“Kama sehemu ya mkakati wa kuboresha mazingira ya kazi, wizara imewasilisha rasimu ya mwongozo wa mpango wa motisha kwa watumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa ajili ya uchambuzi na ushauri zaidi,” amesema.

Amesema pia amemuandikia Rais Samia Suluhu Hassan kumfahamisha na kumueleza kwa kinanamna mazingira ya kazi na hali ya watumishi katika ngazi mbalimbali, ikiwemo madaktari bingwa, bingwa bobezi, wauguzi na watumishi wengine wa sekta hiyo.

Amesema mpango huo utasaidia kutambua na kuwazawadia watumishi wanaojituma na wanaofanya kazi katika mazingira magumu.

“Mtumishi aliyechoka, asiye na vitendea kazi na asiyeona haki katika upandaji vyeo au anayesubiri malimbikizo yake kwa muda mrefu hawezi kutoa huduma kwa ari ileile tunayoitarajia,” amesema.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe akizungumza na watumishi wa afya jijini Mwanza katika baraza lao kuu la wafanyakazi. Picha na Saada Amir

Lugha na utu kwa wagonjwa

Amesema licha ya Serikali kuboresha miundombinu, bila lugha nzuri na utu, miundombinu hiyo yakiwemo majengo si chochote.

“Majengo mazuri bila lugha nzuri kwa wagonjwa ni kazi bure… mashine ya kisasa bila moyo wa huruma ni chuma kisicho na tiba. Hospitali inayong’ara lakini inatia hofu kwa lugha chafu, kwa rushwa, upendeleo au uzembe haijatimiza wajibu wake,” amesema.

“Hatutavumilia lugha chafu kwa wagonjwa, hatutavumilia rushwa na hatutavumilia ucheleweshaji wa huduma usiyo na sababu wala tija… lakini hatutavumilia upendeleo unaodhalilisha haki ya mwananchi.”

“Mgonjwa anapokuja kwetu, anakuwa amebeba maumivu na hofu… kauli yetu inaweza kuwa dawa ya kwanza au jeraha la pili. Twende tukachague kauli yetu kuwa dawa,” amesema.

Kurejea kazini

Amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa watumishi walionufaika na ufadhili wa Serikali katika masomo yao, akitaka warejee katika vituo vya kazi na kutoa huduma kwa wananchi.

“Waliosomeshwa na Serikali warudi kufanya kazi kwa Serikali kwa mujibu wa mkataba wa Serikali… watu wamesomeshwa na Serikali, mwingine kamaliza masters anaunganisha PhD, well and good, siyo mbaya. Lakini watu hawarudi, wanaomba likizo bila malipo wakati sheria inasema ukitoka lazima urejee ufanye kazi miaka mitatu au minne,” ameagiza.

Baadhi ya watumishi wa sekta ya afya wakiwa kwenye kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa sekta hiyo linalofanyika jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Viongozi mungu watu

Amesema kuna malalamiko kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, vitisho, unyanyasaji na udhalilishaji wa watumishi wa ngazi za chini.

“Ubabe si uongozi, udhalilishaji si nidhamu, vitisho si usimamizi… Wizara ya Afya haiwezi kuliponya Taifa kama yenyewe inaumiza watumishi wake,” amesema.

Afya ya akili, ununuzi wa dawa

Amesema Serikali itaongeza juhudi za kusogeza huduma za afya ya akili karibu na wananchi.

“Afya ya akili si anasa ya mijini… ni hitaji la kila familia, kila shule, kila kijiji na kila sehemu ya kazi,” amesema.

Pia, amesema lazima taifa lijikite katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba vya ndani ili kupunguza utegemezi wa nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *