
Ripoti hiyo iitwayo “Nani anayelipa gharama? Ukosefu wa usawa wa Kijinsia na Taifa kutokuwa na deni” imechambua takwimu kutoka nchi 85 zinazoendelea na kubaini kuwa wanawake wanaathirika zaidi kupitia kupoteza ajira, kushuka kwa kipato na kuongezeka kwa majukumu yasiyolipwa ya malezi na huduma nyumbani.
Kwa nini hali hii inatokea?
Uchunguzi imebainisha kuwa serikali zinapoongeza fedha kwa ajili ya kulipa madeni, hupunguza matumizi kwenye sekta muhimu kama afya na ustawi wa jamii, jambo linalopunguza fursa za ajira rasmi na huduma za msingi.
“Madeni ya taifa si suala la hesabu pekee, bali ni suala la kibinadamu. Malipo makubwa ya madeni yanapunguza uwezo wa serikali kuwekeza kwenye huduma muhimu, na mzigo mkubwa unaangukia wanawake,” alisema Alexander De Croo ambaye ni Mkuu wa utawala wa UNDP.
Ripoti hiyo pia inaonya hatari ya muda mrefu kuwa, hadi ajira milioni 92.5 za wanawake zinaweza kuwa hatarini. Aidha, vifo vya akina mama vinaweza kuongezeka kwa asilimia 32.5 hii ni sawa na vifo 67 zaidi kwa kila vizazi 100,000.
Nani anaathirika zaidi?
Wanawake, hasa wale wanaobeba jukumu kubwa la malezi na huduma za nyumbani, wanapoteza fursa za kiuchumi wakati huduma za kijamii zinapopunguzwa.
Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo Mkurugenzi wa Usawa wa Jinsia wa UNDP Raquel Lagunas amesema “Wanawake ndio wa kwanza kupoteza ajira, huduma na usalama wa kiuchumi pindi matumizi ya umma yanapobanwa na madeni.”
Ripoti hiyo inatoa wito kwa serikali na taasisi za kifedha duniani kuweka kipaumbele katika ajira, maendeleo ya binadamu na usawa wa kijinsia, badala ya sera za kubana matumizi zinazoongeza pengo la kipato.
Kwa ujumla, wataalamu wanaonya kuwa mafanikio ya maendeleo yanaweza kurudi nyuma ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa kudhibiti mzigo wa madeni bila kuathiri huduma za kijamii.