
Dar es Salaam. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imewasilisha bungeni bajeti yake ya Sh525.327 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27 huku ikibainisha vipaumbele tisa itakavyovifanyia kazi.
Kati ya fedha hizo, Sh39.071 bilioni ni kwa ajili ya mishahara, Sh28.065 bilioni ni matumizi mengineyo huku miradi ya maendeleo ikitengewa Sh458.19 bilioni.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Mei 4, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda wakati akiwasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha mbele ya Bunge.
Miongoni mwa vipaumbele alivyovibainisha ni kukamilisha maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027 yatakayofanyika Juni hadi Julai 2027 nchini kwa kushirikiana na nchi nyingine za Kenya na Uganda.
Makonda amesema wizara inalenga kukamilisha kukarabati, kuboresha, kujenga na kuendelea kutunza miundombinu katika sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo.
Kipaumbele kingine, amesema ni Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya 74 ya Urembo ya Dunia (Miss World).
Mbali na sekta hiyo ya burudani, wizara pia inakudia kukamilisha kutunga na kuhuisha sera, sheria, mikakati, miongozo na kanuni mbalimbali katika kuimarisha usimamizi na utekelezaji katika sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo.
Pia, amesema vipaumbele vingine ni kuimarisha na kustawisha Kiswahili kikanda na kimataifa, kuimarisha, kuziwezesha na kufanikisha ushiriki wa timu za Taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na kuboresha elimu na mafunzo katika tasnia za utamaduni, sanaa na michezo.
Vipaumbele vingine amesema ni kuweka na kuboresha mazingira wezeshi na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza na kuendeleza sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo; na kuratibu, kuendesha na kusimamia matamasha, shughuli na matukio ya habari, utamaduni, sanaa na michezo.
“Maeneo mahsusi yatakayopewa kipaumbele katika mwaka 2026/27 ni pamoja na: kuhakikisha upatikanaji wa maudhui ya redio (TBC) Taifa, Bongo FM na TBC International), Televisheni (TBC1, TBC2, Tanzania Safari Chaneli na Televisheni ya Kiingeraza), TBC mtandao.
“Kuendelea kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha kwa kutangaza utekelezaji wa shughuli za kimkakati za Serikali; kuchapa na kusambaza nakala 1,909,752 za magazeti ya Daily News na Habari Leo; kuimarisha usimamizi wa uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kuboresha mifumo ya kupokea, kuchakata na kushughulikia malalamiko,” amesema.
Makonda amesema wizara itaendelea kutoa elimu kwa watoa huduma za kwa kuzingatia kanuni, miongozo, masharti ya leseni na maadili ya uandishi na utangazaji wa habari; kuratibu kampeni ya kitaifa ya kukabiliana na changamoto za mmomonyoko wa maadili nchini; kuratibu maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani katika ngazi ya kitaifa na kikanda, ikiwamo kufanya kongamano la kimataifa la Kiswahili jijini Paris, Ufaransa.
“Tutasimamia uzingatiaji wa maadili katika shughuli za sanaa; na kutoa mikopo yenye thamani ya Sh20 bilioni kwa wadau 8,000 wa tasnia za habari, utamaduni na sanaa na ajira zinazotarajiwa kuzalishwa ni 105,000,” amesema Makonda.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Cornel Magembe amesema makadirio ya bajeti hiyo katika miradi ya maendeleo hayajaongezeka kwa mwaka 2026/27 ikilinganishwa na mwaka 2025/26.
Magembe amesema kamati imebaini kuwa wizara hiyo haina miradi mipya na ratiba ya utekelezaji wa miradi ya awali haiongezi bajeti ya maendeleo.
“Kwa jumla bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeongezeka kwa asilimia 1.09 bila ongezeko lolote katika bajeti ya miradi ya maendeleo. Kwa takwimu hizi uendeshaji wa wizara umeongezewa bajeti kiasi na miradi ya maendeleo itaendelea kama ilivyokuwa,” amesema.
Amesema kamati ina maoni kuwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kutasaidia kukamilisha ujenzi wa miundombinu bora ya michezo Tanzania.
Amesema imetoa maoni kuwa, kuendelea kutenga bajeti na kutoa fedha kwa wakati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa viwanja vitatu vya mazoezi katika Mkoa wa Dar es Salaam na viwanja vitano vilivyopo mkoani Arusha ni jambo linaloweza kufanikisha maandalizi madhubuti ya AFCON 2027.
“Serikali ifufue na kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa vazi la Taifa ili kuimarisha utambulisho wa Taifa, kukuza umoja wa kitaifa, kukuza uchumi, ajira pamoja na kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania,” amesema.