Unguja. Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeteketeza tani 4.8 za maziwa ya watoto aina ya S.M.A namba moja, baada ya kubainika kuwa yamechafuliwa na kemikali ya Cereulide inayotokana na bakteria aina ya Bacillus cereus.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la kulinda afya za watoto na jamii kwa ujumla dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya bidhaa hizo zisizo salama.
Akizungumza wakati wa uteketezaji huo uliofanyika Jumamosi, Mei 2, 2026, Ofisa Uhusiano wa ZFDA, Fatuma Makame Juma, amesema hatua hiyo imekuja kutokana na taarifa iliyotolewa na kampuni ya Nestlé kuhusu uwepo wa uchafuzi katika baadhi ya bidhaa za maziwa hayo.
Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo, ZFDA ilifanya ukaguzi wa haraka katika maeneo mbalimbali ya biashara na kufanikiwa kuyatoa sokoni maziwa hayo kabla hayajasababisha madhara kwa watumiaji.
“Bidhaa hizi zingeweza kusababisha madhara mbalimbali kwa watoto na watumiaji wengine, ikiwemo kichefuchefu, kutapika, maumivu ya tumbo pamoja na kuharisha, hivyo ilikuwa lazima kuchukua hatua za haraka,” amesema.
Maziwa ya watoto aina ya S.M.A namba moja yaliyoteketezwa na Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA).
Amefafanua kuwa maziwa yaliyoteketezwa ni S.M.A namba moja pekee, huku akiwahakikishia wananchi kuwa maziwa ya S.M.A namba mbili na namba tatu yaliyopo sokoni ni salama na yanafaa kwa matumizi ya binadamu.
Fatma amewataka wafanyabiashara pamoja na wananchi kushirikiana na ZFDA kwa kutoa taarifa mapema wanapobaini bidhaa zilizoharibika, zilizokwisha muda wake au zinazotia shaka ili hatua stahiki zichukuliwe kwa haraka.
Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni ya Bopar Enterprises Ltd, Abdul Hussen Mohamed, amesema ushirikiano wao na ZFDA umewezesha kuyaondoa maziwa hayo sokoni kwa wakati na kuzuia madhara yaliyoweza kujitokeza kwa watoto.
Amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na mamlaka husika katika kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zinapitia ukaguzi na kupata vibali rasmi kabla ya kuingizwa sokoni.
“Tumekuwa tukihakikisha kila bidhaa inayokuja nchini inapita kibali cha uingizaji kutoka ZFDA ili kuzuia bidhaa zisizo salama kuwafikia wananchi,” amesema.
Juma Hamdani, mkazi wa Kibele, amesema udhibiti wa bidhaa zisizo salama ni muhimu katika kuhakikisha watoto na jamii kwa ujumla zinapata bidhaa bora na salama kwa matumizi ya kila siku.
Aidha, ameipongeza ZFDA kwa jitihada zake katika kulinda afya za wananchi na kuwataka waendelee kuchukua hatua stahiki kwa bidhaa zisizo salama kwa matumizi ya binadamu.