Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limekutana na kufanya kikao na wadau wa ujenzi wa meli jijini Mwanza kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa meli na vyombo vingine vya majini nchini ili kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na wadau hao, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ya Usafiri Majini Wakili Leticia Mtaki, amesema TASAC itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa meli na vyombo vya majini nchini ili kupunguza utegemezi wa kuagiza vyombo hivyo kutoka nje ya nchi, hatua ambayo pia itasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

Naye, Meneja wa ukaguzi na usajili wa meli TASAC Mhandisi Said Kaheneko amewahimiza wajenzi wa meli kuwasilisha michoro kama inavyotakiwa na Sheria ili kusaidia kupunguza makosa ya kiufundi yanayoweza kusababisha ajali.

Kwa upande wao, wadau wa ujenzi wa meli wameeleza kuwa kikao hicho kimewapa fursa ya kutambua maeneo mbalimbali ya uwekezaji katika sekta ya usafiri majini pamoja na umuhimu wa kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.

Kikao hicho cha kwanza na cha kipekee Tanzania kuwahi kufanyika kimekuja wakati mwafaka kutokana na umuhimu wa sekta ya usafiri majini katika maendeleo ya Ukanda wa Ziwa Victoria na Taifa kwa ujumla, kwani kuwa na meli bora kutasaidia kuimarisha usalama wa usafiri majini.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *