WAKATI matumaini ya mashabiki wa Simba kwa sasa yakiwa kwa Seleman Mwalimu, mabosi wa timu hiyo wanaweza kuwa na wakati mgumu kumbakisha mshambuliaji huyo anayewatumikia kwa mkopo kutoka Wydad Casablanca ya Morocco.
Mara baada ya msimu huu 2025-2026 kumalizika, Mwalimu ambaye ni mfungaji bora wa Kombe la Muungano 2026 akiwa na mabao matatu huku afunga sita Ligi Kuu Bara, anatakiwa kurejea zake Morocco kutumikia mkataba uliosalia hadi Juni 30, 2029.
Ili Simba kusalia na mshambuliaji huyo mzawa, rais wa heshima na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ anatakiwa kumwaga mkwanja mrefu kulingana na thamani ya mchezaji huyo.
Ikumbukwe kuwa, Mwalimu ambaye Mtandao wa Transfermarket unahusika na takwimu za mpira wa miguu, uhamisho, tetesi, thamani za wachezaji, makocha na klabu unaonesha amezaliwa Januari 19, 2006 akiwa na miaka 20 hivi sasa, alijiunga na Wydad Casablanca kwa uhamisho wa Euro 288,000 (Sh881.8 milioni) akitokea Singida Black Stars.
Uhamisho huo ulimfanya mshambuliaji huyo kuvunja rekodi ya Simon Msuva wakati akiondoka Yanga na kujiunga na Difaa El Jadida mwaka 2017 ambaye alisajiliwa kwa Dola 150,000 (Sh337 milioni), ambapo wakati huo kiungo huyo alikuwa akishikilia rekodi ya mchezaji wa Kitanzania aliyesajiliwa kwa mkwanja mrefu zaidi Morocco.
Ili Simba au timu nyingine ambayo itahitaji huduma ya mshambuliaji huyo itabidi ijipange kutokana na ada kubwa ya uhamisho ambayo vigogo hao wamekuwa wakitoza.
Taarifa kutoka Morocco zinabainisha, wakati Simba inamchukua Mwalimu kwa mkopo, ilitoa kiasi cha Euro 50,000 (Sh153 milioni), hali inayoonesha Wydad imekuwa ikiwatoa wachezaji wake kwa gharama kubwa iwe kumuuza au mkopo.
Kabla ya kuanza msimu huu, Wydad ilipiga bei baadhi ya nyota wake akiwemo Thembinkosi Lorch kwenda Al-Ittihad (Libya) kwa Euro 1.10m ambazo ni zaidi ya Sh3.08 bilioni.
Nassim Chadli kwenda Al-Ain ya Falme za Kiarabu kwa Euro 875,000 zaidi ya Sh2.45 bilioni, Jamal Harkass kwenda Damac FC ya Saudia kwa Euro 600,000 zaidi ya Sh1.68 bilioni na Stephane Aziz Ki kwenda Al-Ittihad (Libya) kwa Euro 340,000 zaidi ya Sh952 milioni.
Katika kipindi kifupi ambacho ameichezea Wydad Casablanca kabla ya kurejea Bongo mwanzoni mwa msimu huu 2025-2026 kwa mkopo, Mwalimu ni kati ya mastaa ambao waliweka rekodi mwaka jana 2025 kwa kucheza fainali za Kombe la Dunia la Klabu ambapo Chelsea ilitwaa ubingwa huo kwa kuichapa PSG mabao 3-0 huko Marekani.
Mwalimu alicheza kwa jumla ya dakika 73, katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo mikubwa zaidi duniani katika ngazi ya klabu, alikuwa benchi dhidi ya Manchester City na walipoteza kwa mabao 2-0, akapata nafasi dhidi Juventus na kucheza kwa dakika 45, mechi ambayo ilimpa umaarufu huku wakipoteza kwa mabao 4-1.
Kocha wa Wydad, Mohamed Amine Benhachem kwa wakati huo, alimpa tena nafasi Mwalimu katika mechi ya mwisho dhidi ya AI Ain, aliingia dakika ya 62 akichukua nafasi ya Al Somah na kupiga mashuti mawili wakati wakipoteza kwa mabao 2-1.
Licha ya Simba kuonyesha kuvutiwa na huduma ya mshambuliaji huyo, inaelezwa kuwa Mwalimu atakuwa na nafasi ya kuonyesha pia mbele ya Patrice Carteron huko Wydad pindi atakaporejea kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao kutokana na mabadiliko ya benchi la ufundi la timu hiyo ambayo yamefanyika.
Carteron aliteuliwa kuwa kocha wa Wydad Machi 24, 2026 akichukua mikoba ya Benhachem ambaye alimpa fursa kwa mara ya kwanza Mwalimu huko Morocco na kushauri kumtoa kwa mkopo ili kujijenga zaidi kutokana na ufinyu wa nafasi kwenye kikosi hicho ambacho kwa sasa kinamastaa kama vile, Hakim Ziyech.
MWENYEWE AFUNGUKA
Akizungumzia ukubwa wa jukumu alilonalo katika safu ya ushambuliaji ya Simba, Mwalimu amesema:
“Binafsi sina presha kwa sababu yapo ambayo nimejifunza wakati nikiwa Wydad Casablanca kiasi cha kupata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia la klabu msimu uliopita, nina furaha kuwa hapa na shabaha yangu ni kufanya vizuri kwa ajili ya Simba.”
Ameongezakwa kusema: “Kuhusu nini kitatokea hilo ni suala la kusubiri hadi mwisho wa msimu, kwa sasa fokasi yangu ni kusaidia timu, tumemaliza kazi nzuri na kubwa Zanzibar (katika michuano ya Muungano ambapo Simba ilibeba ubingwa) sasa ni upande wa Ligi Kuu Bara.”
Wakati huohuo, Kiungo wa Singida Black Stars, Lamine Jarjou raia wa Gambia, amesema: “Katika Ligi ya Tanzania mshambuliaji ninayemuona ana vitu vingi uwanjani na talenti kubwa ni Mwalimu.”
Kauli yake iliungwa mkono na staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel aliyesema: “Namfahamu Mwalimu tangu akiwa mdogo, ana kipaji kikubwa ni suala la muda kukiona kwa ukubwa na uwazi wake.”