
Arusha. Simanzi na maswali mazito vimetanda katika familia ya mfanyabiashara Sifaeli Mollel baada ya mwili wake kukutwa ukiwa umeharibika ndani ya nyumba inayodaiwa kutumiwa na mganga wa jadi katika eneo la Muriet jijini Arusha.
Mollel (48), mkazi wa Kijenge, Kata ya Kimandolu, alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Mei 3, 2026, kabla ya mwili wake kupatikana siku saba baadaye ndani ya nyumba hiyo.
Tukio hilo limeibua utata mkubwa baada ya ndugu wa marehemu kudai kulikuwa na viashiria vinavyoonyesha huenda aliuawa, huku mtu anayedaiwa kuendesha shughuli za uganga katika nyumba hiyo akitoweka kusikojulikana.
Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
“Upelelezi tumeshaanza ili kubaini chanzo cha tukio hilo na waliohusika. Endapo mtu yeyote atabainika kuhusika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema Masejo kwa njia ya simu.
Kaka wa marehemu, Augustino Simon, amesema familia ilianza kumtafuta ndugu yao baada ya kupotea nyumbani kwake Mei 3, ikiwemo kusambaza picha zake katika mitandao ya kijamii.
Amesema walipokuwa katika kituo cha polisi wakifuatilia taarifa za kupotea kwake, walipigiwa simu na kuambiwa kuna mwili wa mtu uliokuwa umeharibika umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Kituo cha afya Muriet.
“Tulipoelezwa kuwa mwili huo umeokotwa ndani ya nyumba ya mganga wa kienyeji, mwanzoni tuliona haiwezekani kuwa ni ndugu yetu kwa sababu hakuwa mganga wala hana makazi Muriet. Lakini baadaye tuliamua kwenda kujiridhisha,” amesema.
Amesema waliongozana na askari polisi hadi mochwari na kuukuta mwili huo ukiwa umeharibika na kuvimba vibaya, ndipo walipobaini ni ndugu yao.
“Tulipofika eneo la tukio tulikuta viatu vya ndugu yetu pamoja na vifaa vya tiba za asili ndani ya chumba hicho. Kilichotushangaza ni kwamba vitambulisho vilivyokuwapo vilikuwa na majina tofauti,” amesema.
Simon amesema leseni za biashara ya tiba za asili pamoja na taarifa za mwenye nyumba zinaonyesha mpangaji wa nyumba hiyo alikuwa mtu aitwaye Isihaka Mwitu, tofauti na jina la marehemu.
Amesema jambo lililozidi kuongeza sintofahamu ni kwamba simu ya marehemu iliendelea kuita kwa siku kadhaa hata baada ya mwili wake kupatikana, huku ikionekana katika maeneo tofauti ya jijini Arusha.
“Tunajiuliza kama alifariki ndani ya nyumba hiyo, ni nani alikuwa anatembea na simu yake? Tunaomba polisi wafanye uchunguzi wa kina kwa sababu tunahisi ndugu yetu alifika hapo kama mteja,” amesema.
Naye mkazi wa Muriet, Leonard Swai, amesema mtu aliyekuwa akiendesha shughuli za uganga katika nyumba hiyo hakuwa akifahamika vizuri mtaani kwa sababu alikuwa hafiki mara kwa mara.
“Mimi ni miongoni mwa watu waliovunja mlango baada ya kuona nzi wengi na harufu kali ikitoka ndani. Tulipochungulia dirishani ndipo tuliona mwili wa mtu ukiwa ndani,” amesema.
Amesema baada ya kutoa taarifa kwa viongozi wa eneo hilo na polisi, mlango ulivunjwa na kuukuta mwili ukiwa umeharibika vibaya, huku sehemu ya juu ya mwili ikiwa wazi na kufunikwa kwa kitenge.
“Huyu inaonekana alikuwa mteja aliyekuja kupata huduma. Huenda alikuja na fedha nyingi zilizomshawishi huyo mganga kufanya uhalifu,” amesema Swai.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Muriet, Joseph Emmanuel, amesema alipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu harufu kali na nzi wengi waliokuwa wakitoka ndani ya nyumba hiyo.
“Baada ya kufika polisi waliinua kufuli na tukakuta mwili ukiwa umevimba sana. Marehemu alikuwa amelala chali, kifua wazi na amefunikwa kwa kitenge,” amesema.
Amesema ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na mapazia mekundu pamoja na vifaa vinavyodaiwa kutumika katika shughuli za tiba za asili.
Mwenyekiti huyo amesema juhudi za kumpata mpangaji wa nyumba hiyo bado hazijafanikiwa, huku mwenye nyumba akidai hana taarifa za ndugu zake wala mahali alipo.
Kutokana na tukio hilo, amewataka wananchi kuhakikisha wapangaji wa nyumba wanajitambulisha kwa viongozi wa maeneo yao ili kusaidia usalama wa jamii na kurahisisha uchunguzi wa matukio ya uhalifu.
“Tunaamini uchunguzi wa polisi utasaidia kufichua ukweli wa tukio hili kwa sababu taarifa zilizopo zinaonyesha marehemu alikuwa amekwenda kupata huduma katika nyumba hiyo,” amesema Emmanuel.