KMC imeendelea kujiweka karibu zaidi na hatari ya kushuka daraja baada ya kupoteza kwa mabao 4-3 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, uliopigwa leo Mei 14, 2026.

Mtibwa Sugar ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 30 kupitia kwa Fredrick Magata, kabla ya Oscar Masai kuongeza la pili dakika ya 45. Hadi mapumziko wenyeji walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa presha kubwa kutoka kwa Mtibwa Sugar na dakika ya 49, Said Mkopi alipachika bao la tatu kwa mpira wa adhabu uliomshinda kipa wa KMC, Ismail Mpanki.

Dakika ya 51, KMC ikapata bao kupitia Daruweshi Saliboko kwa mkwaju wa penalti na kupunguza pengo la mabao kuwa 3-1, kisha dakika ya 53, Kassimu Shaibu aliiongezea  Mtibwa Sugar bao la nne.

Licha ya kuwa nyuma kwa tofauti ya mabao matatu, KMC haikukata tamaa na iliendelea kushambulia. Rashid Chambo aliifungia timu hiyo bao la pili dakika ya 57 na kurejesha matumaini ya kupata matokeo chanya.

Dakika ya 85, Adam Uledi aliandika bao la tatu kwa KMC katika tukio lililoibua mabishano makubwa, baada ya mwamuzi msaidizi wa kwanza, kuinua kibendera akidai kulikuwa na kuotea (Offside). Hata hivyo, baada ya benchi la ufundi la KMC kuonyesha kutoridhika, waamuzi walijadiliana na bao likakubaliwa.

Pamoja na kurejea kwa nguvu katika dakika za mwisho, KMC ilishindwa kupata bao la kusawazisha na kujikuta ikipoteza mchezo huo uliofanya kuwa ni wa kumi mfululizo kumaliza dakika tisini bila ya ushindi.

Kwa matokeo hayo, KMC imezidi kujiweka kwenye hatari zaidi ya kushuka daraja, ikisalia mkiani mwa msimamo na pointi tisa ikicheza mechi 23.

KMC sasa imepoteza mechi ya 18 katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ikishinda mbili na sare tatu, imebakiwa na saba kuhitimisha msimu ambapo hali inaonekana kuwa ngumu kujiokoa na aibu ya kushuka daraja.

Kwa upande wa Mtibwa Sugar, ushindi huo unawasogeza hadi nafasi ya kumi kutoka ya 13, ikifikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi 23.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *