
Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Manga kilichopo wilayani Ludewa, Oliva Mgina (24), aliyekuwa akitafutwa kwa kosa la mauaji ya kaka yake, Lasenus Mgina (27), ambaye inadaiwa alimpiga kwa kitu chenye ncha kali.
Aidha, katika oparesheni ya Aprili hadi mwanzoni mwa Mei 2026, jumla ya watuhumiwa 52 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali, yakiwemo mauaji, wizi wa pikipiki, uvunjaji na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.
Hayo yamesemwa leo Mei 15, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, alipozungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.
Amesema tukio hilo la mauaji lilitokea Novemba 26, 2025 katika kijiji hicho cha Lusitu, na mtuhumiwa alitoroka kusikojulikana, na amekuwa akitafutwa hadi alipokamatwa na Jeshi la Polisi.
Amesema mtuhumiwa alichelewa kurudi nyumbani, ndipo kaka yake ambaye ni marehemu kwa sasa akamuuliza kwa nini amechelewa, swali ambalo lilimkera, na kuchukua kitu chenye ncha kali na kumpiga nacho.
Amesema upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea, na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili.
“Huyu alimuua kaka yake siku za nyuma. Binti alirudi nyumbani, hakulala nyumbani, kaka yake alipoanza kumgombeza akampiga na kitu kizito, ndipo akapoteza maisha,” amesema Banga.
Amesema Jeshi hilo pia linamshikilia Thomas Haule, mkazi wa Ngalawale wilayani Ludewa, kwa kujifanya mfanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi ya Yas na kuingilia mifumo ya simu na kupora fedha Sh82,992.
Kamanda Banga amesema upelelezi wa kesi hiyo utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Aidha, katika wilaya hiyo ya Ludewa, watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, ambao ni Gerald Matei (25) na Elisha Kayombo (23), wakiwa na pikipiki mbili ambazo hazina usajili, mali zinazodaiwa kuwa za wizi.
Kwa upande wa usalama barabarani, Kamanda Banga amesema katika kipindi cha Aprili, jumla ya makosa 5,427 yalikamatwa; kati ya hayo, 5,426 yalitozwa faini, lakini kosa moja dereva alifungiwa leseni.
Ametoa wito kwa wananchi mkoani Njombe kuacha kujichukulia sheria mkononi au kufanya uharibifu wa mali, kwani Jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayebainika kutenda vitendo vya kihalifu.
Mkazi wa Njombe, Andrew Haule, amesema sababu kubwa ya wananchi mkoani humo kutenda matukio ya mauaji ni migogoro ya ardhi ndani ya familia au imani za kishirikina.