Hospitali Cuba zasitisha upasuaji, wagonjwa zaidi ya 100,000 wasubiri matibabuHospitali Cuba zasitisha upasuaji, wagonjwa zaidi ya 100,000 wasubiri matibabu

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini New York Marekani kwa njia ya video baada ya ziara ya siku tatu nchini Cuba, Maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, Edem Wosornu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya yuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, na Altaf Musani kutoka shirika la Umoja wa Matraifa la afya ulimwenguni WHO, wamesimulia jinsi uhaba wa umeme, mafuta, dawa na vifaa tiba unavyoathiri kwa kiasi kikubwa huduma za dharura, benki za damu, maabara, mipango ya chanjo pamoja na huduma za afya kwa wajawazito na watoto.

Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa mfumo wa afya nchini Cuba uko chini ya shinikizo kubwa huku hospitali zikihangaika kutoa huduma za msingi kutokana na uhaba unaoendelea na kukatika kwa umeme.

Hali ni mbaya kiasi gani?

Katika baadhi ya maeneo, kukosekana kwa umeme kwa hadi saa 20 kumelazimisha hospitali kusitisha upasuaji usio wa dharura, huku uhaba wa mafuta ukipunguza huduma za magari ya wagonjwa na kuchelewesha huduma muhimu.

Zaidi ya wagonjwa 100,000 wakiwemo watoto 11,000 wanasubiri kufanyiwa upasuaji uliocheleweshwa kutokana na kukatika kwa umeme na uhaba wa vifaa.

Takribani watu milioni tano wenye magonjwa sugu pia wako katika hatari ya kukosa matibabu muhimu ya kuokoa maisha. Miongoni mwao ni zaidi ya watu 16,000 wanaohitaji tiba ya mionzi na zaidi ya watu 12,000 wanaopokea matibabu ya saratani kwa njia ya kemikali.

“Gharama kwa maisha ya binadamu ni kubwa na inaendelea kuongezeka,” amesema Musani, huku vituo vya afya vikikabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa tiba na huduma ya umeme isiyo ya uhakika.

© Adobe Stock/Peter Acker Havana, Cuba muuza ndizi akizipakia katika baiskeli ya magurudumu matatu

Wanawake na watoto

Huduma za afya kwa wajawazito na watoto wachanga pia zimeathirika kwa kiasi kikubwa.

Zaidi ya wajawazito 32,000 wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana na upungufu wa huduma za uchunguzi, usafiri na umeme wa uhakika unaohitajika kuendesha vifaa muhimu katika vitengo vya watoto wachanga.

“Wahudumu wa afya wanalazimika kubeba maji kwakupanda ngazi huku wanawake wakiwa wanajifungua na hii ni kwasababu pampu za maji hazifanyi kazi,” amesema Wosornu.

Ameongeza kuwa changamoto za usafiri zinazuia usambazaji wa mboga na nyama, hali inayowanyima wajawazito lishe bora.

Mifumo ya maji, usafi wa mazingira na uhifadhi wa dawa kwenye ubaridi pia imeathirika, jambo linaloongeza hatari ya magonjwa yanayoenezwa na mbu na maji kama dengue na chikungunya.

Ingawa programu za kawaida za chanjo zinaendelea, zinakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kuvurugika kwa mifumo ya ubaridi, matatizo ya usafiri na uhaba wa vifaa.

Kiujumla Wosornu ameeleza changamoto wanazokabiliana nazo wananchi wa Cuba zinazidi kuwa mgumu na madhara yake ya kibinadamu yanaenda mbali zaidi ya majanga ya kawaida ya asili.

Heko kwa wahudumu wa wafya

Licha ya hali hiyo kuwa mbaya, maafisa wa OCHA na WHO wamewasifu wahudumu wa afya na jamii kwa kuendelea kuwahudumia wagonjwa licha ya uhaba mkubwa wa vifaa na mazingira magumu ya kazi.

“Msaada wa kuokoa maisha lazima uwafikie watu bila kuchelewa. Kuchukua hatua haraka na kufanya kazi pamoja ndiyo njia pekee ya kuzuia hali hii kuwa mbaya zaidi. Hatuwezi kumudu mzozo mwingine wa kibinadamu,” amesema Wosornu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *