
Mashirika hayo ni lile la Chakula na Kilimo FAO, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, na lile la Mpango wa Chakula Duniani, WFP.
Taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo mjini Mogadishu, nchini Somalia, imeonesha kuwa ongezeko hilo limesababisha athari mbaya zaidi za utapiamlo duniani unaowaathiri takribani watoto milioni 1.9, ambapo kati yao watoto 493,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali wa ghafla, hali inayowaweka kwenye hatari ya kufariki, mara 12 zaidi ikilinganishwa na watoto wenye lishe bora.
Uchambuzi mpya wa Ripoti ya hali ya uhakika wa chakula (IPC), umeonesha kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na hali ya dharura imeongezeka mara tatu ndani ya mwaka mmoja, huku kukiwa na hatari kubwa ya njaa kali katika maeneo ya kilimo na ufugaji hususan wilaya ya Burhakaba, iwapo mvua za msimu wa Aprili hadi Juni hazitanyesha na bei za vyakula zitaendelea kupanda kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati.
Hali hii ya dharura imejiri wakati athari za mizozo ya kikanda na matatizo ya usafirishaji wa bidhaa baharini zikipandisha bei za vyakula kwa asilimia 20 na kudhoofisha uwezo wa ununuzi wa kaya maskini.
George Conway, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu nchini Somalia, ametoa wito wa dharura kwa jamii ya kimataifa akisema, “Uchambuzi wa IPC unachora taswira ya wazi na ya dharura, kukiwa na ongezeko la idadi ya watoto wenye utapiamlo na uthibitisho wa hatari ya janga la njaa kali katika eneo la Burhakaba. Bila msaada wa haraka na endelevu kutoka kwa wafadhili, watu waishio ughaibuni na sekta binafsi, tuna hatari ya kushuhudia janga linalozuilika likitokea mbele ya macho yetu.”
Naye Mwakilishi wa FAO nchini Somalia, Etienne Peterschmitt, amefafanua ukubwa wa madhara ya majanga hayo akisema “Nchi ipo kwenye hatua mbaya sana. Ukame mkali na wa muda mrefu ambao umeharibu njia za kujikimu kimaisha, ukiongezeka na mzozo wa Mashariki ya Kati ambao umepandisha bei za chakula na mafuta, pamoja na ongezeko la hatari ya mafuriko makubwa yanayohusiana na El Niño, ina maana kwamba nchi ipo ukingoni mwa hatari ya njaa kali kwa mara nyingine tena.”
Kufungwa kwa huduma za afya na hatari kwa watoto
Kutokana na upungufu mkubwa wa fedha za ufadhili, vituo vya afya na lishe zaidi ya 500 vimefungwa kote nchini Somalia, jambo lililosababisha milipuko wa magonjwa kama surua kuongezeka mara mbili katika robo ya kwanza ya mwaka huu yakiwaathiti watoto ambao tayari wana utapiamlo.
Mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia, Sandra Lattouf, amesisitiza uzito wa janga hili kwa watoto na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka.
“Kote nchini Somalia, watoto wanakabiliwa na mzozo unaozidi kuwa mbaya kwa kasi na muda unaisha. Wakati jamii na wafanyakazi walio mstari wa mbele wakiendelea kuwa wavumilivu, hawawezi kufanya hivyo peke yao. UNICEF inaongeza msaada wa kuokoa maisha kwa dharura. Kwa kuchukua hatua za haraka, bado tunaweza kuokoa maisha na kulinda haki ya kila mtoto ya kuishi na kustawi,” ameeleza Sandra Lattouf.
Mpango wa mwitikio na mahitaji ya kibinadamu wa mwaka 2026 nchini Somalia umepata asilimia 15.2 tu ya fedha zinazohitajika, huku takribani asilimia 90 ya wananchi wakisalia bila msaada wowote wakati utabiri wa El Niño ukionesha hatari ya mafuriko kwa siku za usoni.
Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Somalia, Hameed Nuru, amekumbusha jinsi muda unavyoisha kuokoa maisha ya familia zilizomaliza nguvu zote za kujikimu. “Tunafikia hatua ambayo kuchelewa kwingine kokote kunaweza kugharimu maisha ya watu. Familia zimefuta kabisa njia zao zote za kujikimu, huduma na misaada ya dharura ni midogo mno, na watoto wanatumbukia katika utapiamlo mkali nchini kote.”
Wito wa pamoja wa kuongeza misaada ya dharura
Mashirika hayo yamekamilisha ripoti yao kwa kutoa mwongozo wa pamoja unaotaka kuongezwa kwa misaada ya dharura ya chakula, afya, na maji safi ili kuzuia maafa makubwa ya kibinadamu kabla ya mwisho wa mwaka huu. Habari hii imetoa picha halisi ya changamoto zinazoikabili nchi hiyo huku kukiwa na shinikizo kubwa kwa wafadhili kutoa usaidizi unaohitajika kwa haraka.