Arusha. Serikali ya Tanzania imezihamasisha kampuni na wawekezaji kutoka Urusi kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zinazojitokeza nchini, hususan katika maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, pamoja na sekta za kimkakati zikiwemo madini, nishati, kilimo, viwanda na utalii.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa AFCON 2027 kwa pamoja na Kenya na Uganda, hatua inayotarajiwa kufungua fursa kubwa katika miundombinu ya michezo, hoteli, usafiri, majengo, Tehama, usafiri wa anga na huduma za utangazaji.
Akizungumza leo Ijumaa Mei 15, 2026 katika kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya, amesema Tanzania imejipanga kutumia mashindano hayo kama kichocheo cha uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
“Tanzania pamoja na Kenya na Uganda zitakuwa wenyeji wa AFCON 2027, jambo ambalo linafungua fursa kubwa za uwekezaji katika miundombinu ya michezo, hoteli, usafiri, Tehama, anga na utalii. Tunawakaribisha wawekezaji wa Urusi kushirikiana na sekta binafsi ya Tanzania,” amesema Dk Chaya.
Amebainisha kuwa mbali na AFCON, Tanzania inaendelea kuwa na fursa nyingi katika sekta za madini na uongezaji thamani, uzalishaji wa mbolea, elimu ya ufundi, viwanda, nishati, kilimo cha kisasa, dawa na uhamishaji wa teknolojia.
Amesema Tanzania imeendelea kuvutia wawekezaji kutokana na nafasi yake ya kimkakati kama lango la biashara la ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini kupitia EAC na SADC, zenye zaidi ya watu milioni 300.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TISEZA, Dk Aziz Mlima, amesema kongamano hilo linadhihirisha kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi, ambapo zaidi ya kampuni 120 za Urusi na 200 za Tanzania zilishiriki.
Amesema katika kipindi cha 2020 hadi Machi 2026, miradi 13 yenye ushiriki wa wawekezaji wa Urusi yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 401 imetekelezwa nchini, ikiongozwa na sekta za madini, mafuta na viwanda.
Naye Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, alisema ushirikiano kati ya nchi hizo mbili una nafasi kubwa ya kuleta mageuzi kupitia uhamishaji wa teknolojia, ubia na uwekezaji wa muda mrefu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Tanzania ina takribani hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo, lakini ni asilimia 33 pekee inayotumika, akibainisha kuwa bado kuna fursa kubwa ya uwekezaji katika kilimo na usindikaji wa mazao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya kiserikali nchini Urusi mwezi ujao, hatua inayolenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.