
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameipongeza Tunisia kwa mafanikio hayo na kusema,“Kutokomeza ugonjwa huu wa vikope kunaonesha jinsi gani nia thabiti ya muda mrefu ya serikali, huduma nzuri za afya kuanzia ngazi ya jamii na ushirikiano wa pamoja zinavyoweza kuleta matokeo makubwa. Tunisia imethibitisha kuwa hata ugonjwa unaoongoza duniani kwa kuambukiza watu upofu unaweza kudhibitiwa.”
Ugonjwa wa Trakoma unahusishwa kwa karibu sana na upatikanaji mdogo wa maji safi, usafi wa mazingira, pamoja na usafi wa mwilii, na huathiri zaidi makundi ya watu walio katika mazingira magumu.
Katika nusu ya kwanza ya karne ya 20, ugonjwa huu ulikuwa janga kubwa nchini Tunisia ambapo uliathiri takribani nusu ya idadi ya watu wote nchini humo, hasa katika maeneo ya kusini.
Naye, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Mashariki mwa Bahari ya Mediterania, Dkt. Hanan Balkhy, amepongeza juhudi hizo akisema, “Haya ni mafanikio makubwa yanayoonesha ahadi endelevu na thabiti ya kitaifa kwa miaka mingi na yanaonesha kile kinachowezekana nchi inapoweka msisitizo katika kushughulikia visababishi vya upofu vinavyozuilika.”
Mkakati wa SAFE na mafanikio ya Tunisia
Kwa miongo kadhaa, Tunisia imetekeleza mpango kabambe wa kupambana na ugonjwa huo kwa kutumia mkakati unaopendekezwa na WHO unaojulikana kama SAFE. Mkakati huu unajumuisha upasuaji kwa wagonjwa walifikia hatua za juu za ugonjwa, utoaji wa dawa za kutibu maambukizi ya bakteria (Antibiotics), ili kuondoa maambukizi, kunawa uso ili kupunguza maambukizi, na uboreshaji wa mazingira, hasa upatikanaji wa maji safi na vyoo.
Waziri wa Afya wa Tunisia, Dkt. Mustapha Ferjani, amebainisha, “Uthibitisho huu unaonesha mafanikio ya kihistoria kwa Tunisia na unaonesha ahadi ya muda mrefu ya nchi yetu katika afya ya jamii, kinga na usawa.”
Hadi kufikia sasa, mafanikio hayo yametokana na kampeni ya muda mrefu iliyoongozwa na Wizara ya Afya kwa ushirikiano wa karibu na WHO pamoja na wadau wengine wa maendeleo. Mifumo imara ya afya ya jamii na uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya maji na usafi vimesaidia sana kushusha viwango vya maambukizi ya ugonjwa huo nchini kote na kufanya Trakoma kuwa janga la kwanza la kitropiki lililopuuzwa, kutokomezwa kabisa nchini Tunisia.
Mwakilishi wa WHO nchini Tunisia, Dkt. Ahmed Zouiten, amesema, “Uthibitisho wa kutokomezwa kwa Trakoma kama tatizo la afya ya jamii nchini Tunisia unaonesha matokeo ya ushirikiano endelevu kati ya Wizara ya Afya na WHO katika kufikia mafanikio ya afya ya jamii nchini kote.”
Mipango endelevu kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele
Katika kuhakikisha uendelevu wa hatua hiyo, Tunisia imeweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji ili kubaini mapema ikiwa ugonjwa huo utajitokeza tena mahali popote. Mfumo huo unajumuisha mafunzo endelevu kwa wataalamu wa afya na usimamizi wa wagonjwa wapya watakaogundulika ili kulinda mafanikio hayo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa hatua hii, Tunisia inaungana na mataifa mengine duniani yanayopiga hatua kutokomeza magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa, ambayo ni sehemu muhimu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanayohusu afya, ikiwa ni nchi ya 14 katika ukanda wa Mashariki mwa Bahari ya Mediterania kulingana na mapendekezo ya WHO kufanikiwa kutokomeza angalau ugonjwa mmoja kati ya magonjwa yaliyopuuzwa. Pia, inakuwa nchi ya 31 duniani kote kuthibitishwa kuwa imetokomeza ugonjwa huo wa vikope kama tatizo la afya ya jamii.
Nchi nyingine ambazo tayari zimethibitishwa na WHO, kwamba zimetokomeza ugonjwa huu wa vikope ni pamoja na Algeria, Australia, Benin, Burundi, Cambodia, China, Misri, Fiji, Gambia, Ghana, India, Iraq, Iran, Laos, Libya, Malawi, Mali, Mauritania, Mexico, Morocco, Myanmar, Nepal, Oman, Pakistan, Papua New Guinea, Saudi Arabia, Senegal, Togo, Vanuatu pamoja na Vietnam.