Dar es Salaam. Rais wa Yanga, Hersi Said amesema mradi wa ujenzi wa Uwanja mpya wa klabu hiyo, utawafanya kumiliki asilimia 50 huku mwekezaji akimiliki kiasi hicho.
Akizungumza leo Ijumaa Mei 15, 2026 kwenye hafla ya utiaji saini ya mradi huo Hersi amesema, kampuni ya GSM imeonyesha kutotaka tamaa katika umiliki wa uwanja huo kwa kutaka asilimia 50 pekee za umiliki wa uwanja huo.
Hersi amesema maamuzi hayo yamewapa faraja uongozi wa klabu hiyo, akisema hatua hiyo imeipunguzia mzigo klabu kwa kuwa na nguvu katika mradi huo.
“Wakati tunajadiliana juu ya ujenzi wa uwanja nilishangaa sana kwa nini Ghalib Said Mohammed haukutumia akili yako ya majadiliano ya umiliki wa mradi.
“Wakati tunajadiliana ukasema unataka kumilikia asilimia 50 pekee za mradi huu hatua ambayo itaifanya klabu yetu nayo kumiliki asilimia 50, hii ni hatua kubwa,” amesema Hersi.
Aidha Hersi ameongeza kuwa Yanga katika mradi huo mchango wake mkubwa ni ardhi wakati GSM ikifanikisha jukumu la uwezeshaji wa kifedha katika kufanikisha Uwanja huo.
“Hapa Jangwani tuna eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 35,000. Jukumu letu litakuwa kuwezesha eneo la ujenzi na GSM itafanikisha jukumu la kifedha,” amesema.
Uwanja huo unaatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18 hadi 24, baada ya kutangazwa rasmi kwa kuanza kwa mradi huo.
“Ndugu Wanayanga, hivi karibuni klabu yenu itakuwa na uwanja hapa katika eneo hili (Jangwani). Mungu akijaalia ‘maximum’ miezi 18 mpaka 24 tutasimama hapa kuzindua uwanja huu wa kisasa,” amesema Hersi.
Yanga imesaini makubaliano na kampuni hiyo kwenye ujenzi wa uwanja huo mpya ambao utajengwa eneo la Jangwani, Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo katika Makao Makuu ya Yanga na hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na TFF.
Wakati hafla hiyo ikiendelea, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amempaisha mfadhili wa klabu hiyo Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ akisema hana tamaa katika uwekezaji wa uwanja wa klabu hiyo kutokana na kuwa tayari kugharamia ujenzi wa uwanja huo.
Kamwe amesema kama GSM angekuwa na tamaa kwenye umiliki wa uwanja huo angeweza kuhitaji asilimia 80 kwake na 20 kwa klabu hiyo.
Kamwe amesema GSM amekuwa hana maneno mengi ambapo sasa baada ya maneno yake ya Yanga bingwa watamuongezea maneno mengine hana tamaa.
“Unajua Kuna wakati unaweza kuwa na tamaa lakini GSM ni tofauti sana hebu angalia anataka asilimia 50 tu lakini ingekuwa mwingine angehitaji hata asilimia 80 ziwe kwake na klabu tubaki na 20,” amesema Kamwe huku akishangiliwa na wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.
“Sisi Yanga tunakushukuru kwa moyo wako unatupa somo kwamba tuache tamaa kwenye maisha yetu na nadhani GSM amekuwa hataki mambo mengi kuna Ile kauli yake ya Yanga bingwa lakini sasa tumuongezee maneno haya hana tamaa.”