
Dar es Salaam. Wakati katika mtandao wa kijamii wa Tiktok ikiibuka biashara ya uuzaji wa dola za Marekani bandia kwa wale wanaotaka kujionyesha, Serikali imesema ukikamatwa nazo adhabu yake ni miaka 20 jela au faini ya Sh10 milioni.
Hayo yamesemwa wakati ambao wafanyabiashara hao wameendelea kunadi biashara hiyo huku wakiwataka watu wanaokwenda kwenye sherehe kuchangamka ili wasikae kinyonge wakati wa kutunza.
Kibunda cha dola za Marekani 1,000 kinauzwa kati ya Sh20,000 hadi Sh50,000 kulingana na muuzaji huku wengine wakiuza kibunda hicho pamoja na shotgun (kifaa maalumu cha kumwaga pesa) kwa Sh50,000.
Kwa mujibu wa mmoja wa wauzaji, fedha hizo pia hutumiwa na watu wanaotengeneza picha mjongeo (video) au wanaotaka kuonyesha ufahari katika shughuli mbalimbali.
“Njoo nunua hizi usikae kizembe, urushe watu roho, pesa kidogo unakuwa na fedha nyingi ambazo ukiwaonyesha watu mtandaoni wanachanganyikiwa,” amesema muuzaji huyo huku akisema unaweza kufikishiwa mzigo popote ulipo.
Bidhaa hizo zilionekana kuuliziwa zaidi ya wafuatiliaji wake mtandaoni ambapo baadhi walikuwa wakiuliza wanapataje wakiwa katika mikoa mbalimbali, jambo linalotia shaka iwapo fedha hizo ikiwa zitaingia mtaani na kutumika vibaya na watu wasiojua kutofautisha halali na bandia.
Wakati biashara hiyo ikiendelea, tayari baadhi ya watengenezaji wa maudhui mtandaoni (content creators) wameanza kuzitumia katika baadhi ya machapisho yao wakionyesha uwezo wao wa kumwaga hela.
Kauli ya BoT
Akizungumzia suala hilo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema taarifa zozote zinazohusisha fedha za nchi nyingine kama dola ya Marekani (USD), Euro, Paund, Rand zinapaswa kudhibitiwa na nchi husika kwa kuwa ndiyo yenye dhamana ya kusimamia matumizi sahihi ya fedha yake.
“Kwa upande wa Tanzania, tunasimamia matumizi ya Shilingi ya Tanzania pamoja na pale inapobadilishwa kwa kutumia fedha nyingine za kigeni,” amesema Gavana.
Pamoja na hayo amesema BoT imeendelea kuelimisha umma kupitia njia mbalimbali ili kuwatahadharisha wananchi kujiepusha na vitendo viovu na kuchukua tahadhari dhidi ya matapeli au wahalifu wa mitandaoni.
Amesema wameendelea kutoa elimu kwa wananchi ikiwemo kutumia vipindi mbalimbali ya luninga kuutahadharisha umma na kuelimisha jamii kuhusu udanganyifu wa aina mbalimbali unaofanywa mitandaoni.
“Hadi baadhi wanaambiwa na wawekezaji matapeli kwamba wametumiwa fedha BoT wakati hawana akaunti huko. Wanatumiwa swift message feki na kudanganywa kuwa fedha zao zimetumwa kwenye benki za nchini ambazo zimeiba fedha hizo ili kuzifanyia biashara ya kukopesha watu wengine,” amesema na kuongeza:
“Hivyo, tutaendelea kuelimisha wananchi na kuchukua hatua kwa watu wa ndani ambao watatumia Shilingi ya Tanzania kufanya utapeli wa mitandaoni.”
Athari kiuchumi
Akizungumzia suala hilo, Oscar Mkude amesema kuenea kwa biashara ya dola bandia kunaweza kupunguza imani ya wananchi kwa fedha husika na kuongeza gharama za miamala, kwani watu hulazimika kujiridhisha zaidi kabla ya kufanya ubadilishaji wa fedha.
“Fedha bandia inapokuwa nyingi sokoni, watu wanapoteza uaminifu na kila muamala unahitaji tahadhari zaidi,” amesema Mkude.
Amesema uchumi hufanya kazi vizuri pale ambapo kuna uaminifu katika matumizi ya fedha taslimu lakini endapo fedha bandia zinaongezeka, huibua hatari kubwa kwa wananchi kupoteza fedha zao kwa watu wasio waaminifu.
“Uchumi unategemea uaminifu wa fedha inayotumika. Ukiwa na fedha bandia nyingi, wananchi wanaweza kupoteza fedha zao kirahisi,” amesema.
Kwa mujibu wa Mkude, uwepo wa zuio la matumizi ya fedha za kigeni katika kulipia huduma na bidhaa ndani ya nchi inaweza kusaidia kudhibiti baadhi ya mianya ya utakatishaji fedha hizo ikiwemo watu wenye fedha hizo kutafuta njia za kuzitumia au kuzichanganya na fedha bandia.
“Mtu akiwa na fedha za kigeni anaweza kutafuta njia ya kuzitakatisha au kuzichanganya hizi za bandia na fedha halisi, hivyo udhibiti ni muhimu,” amesema.
Ameeleza kuwa hata wamiliki wa maduka ya kubadilisha fedha wanaweza kuathirika endapo hawatakuwa makini, kwani wanaweza kupokea fedha bandia bila kujua.
Mkude ameonya watu wanaonunua dola sehemu zisizo rasmi kuwa kwenye hatari ya kupigwa, kwa sababu wakipata hasara hawana sehemu ya kulalamikia kutokana na kukosa risiti au ushahidi wa muamala.
Kutokana na hali hiyo, amewashauri wananchi wanaohitaji kununua dola kwenda kwenye maeneo rasmi yaliyopangwa na kusimamiwa, ili kuhakikisha wanapata fedha sahihi na salama.
“Kwa sasa tatizo hilo haliwezi kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Taifa kwa ujumla kwani bado wanauza kwa kiwango kidogo, bali linaweza kuwaumiza zaidi watu mmoja mmoja. Lakini yakiongezeka yanaweza kuwa tishio kwa uchumi mpana,” amesema Mkude.
Mchambuzi wa uchumi na fedha, Dk Goodhope Mkaro amesema mbali na umiliki wa fedha bandia kuwa kinyume na sheria lakini pia uwepo wake unaweza kuathiri mahusiano kati ya nchi na nchi.
“Kuwa na fedha za kigeni bandia kama za Marekani zinaweza kuathiri mahusiano yetu kwani wahusika wakiona wanaweza kudhani hakuna kitu kimefanyika kudhibiti hilo, jambo hili si zuri na wanaolifanya waache mara moja,” amesema Mkaro.
Mfanyabiashara katika soko la Kariakoo, Ramadhan Issa amesema, “kusingekuwa na usimamizi huu, hizi dola tunazoona zinauzwa kwa bei rahisi zingelipia huduma huku kwenye biashara zetu, ukizingatia siyo wote wanajua alama za usalama katika fedha za kigeni kama ilivyo kwa zile za Tanzania.
Lakini bado, alionyesha hofu ya kutaka jambo hilo kudhibitiwa kwani anaamini kuna baadhi ya watu wanaweza kujikuta katika hatari ya kuchanganyiwa fedha halali na bandia jambo linaloweza kuwafanya wapate hasara.
