Fahamu mpango wa Kenya wa kukabiliana na changamoto za makaziFahamu mpango wa Kenya wa kukabiliana na changamoto za makazi

Ruto amesema hatua yao hiyo inazingatia ukweli kwamba wakenya milioni saba wanaishi kwenye makazi duni 1,100 yasiyo rasmi, hali ambayo amesema inadhoofisha uwezo wao wa kupata haki ya makazi bora kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 25 cha Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu.

Akijinasibu kuwa suala la raia kupata makazi bora kuwa ni ajenda Kabambe ya serikali na kuwa moja ya juhudi kubwa zaidi barani Afrika zinazoongozwa na serikali katika kukabiliana na changamoto ya kimataifa ya makazi mijini, Rais Ruto ametaja mkakati wa vipengele vitatu uliolenga upatikanaji wa ardhi, gharama za ujenzi na ufadhili.

UN-Habitat/Nathan Kihara Wakaazi wa mitaa ya mabanda nchini Kenya na makazi yao mapya kufuatia mradi wa serikali kuboresha makazi maeneo hayo.

Hatua zilizochukuliwa

  1. Mathalani serikali ilikabiliana na changamoto ya ardhi kwa kufanya ardhi ya umma kupatikana kwa miradi ya nyumba bila malipo, hatua ambayo amesema ilipunguza gharama za jumla za ujenzi wa nyumba kwa asilimia 30.
  2. Ili kupunguza gharama za ujenzi, Ruto amesema serikali ilikuwa na mazungumzo na wasanifu majengo, wahandisi, wapimaji wa majengo na wataalamu wengine ili kupunguza ada za usimamizi na ushauri kutoka asilimia 10 hadi asilimia 2.5 kwa kubadilishana na kandarasi kubwa za ujenzi wa nyumba.
  3. Serikali pia iliweka viwango vya pamoja vya michoro ya majengo na vifaa vya ujenzi, ikiwemo milango na madirisha yenye vipimo vinavyofanana, hatua iliyowezesha uzalishaji wa vifaa hivyo kwa wingi na kupunguza gharama za utengenezaji.

Fedha zinatoka wapi?

Kuhusu ufadhili, Ruto amesema Kenya ilianzisha mfuko maalum wa makazi unaoungwa mkono na ushuru wa nyumba baada ya kupitishwa kwa sheria husika. Amesema mpango huo unategemea kikamilifu rasilimali zilizokusanywa ndani ya nchi.

“Hatujakopa hata shilingi moja kutoka Benki ya Dunia au taasisi nyingine yoyote,” amesema Ruto akisisitiza kuwa “hizi ni rasilimali zilizokusanywa hapa nchini.”

Idadi ya nyumba

Kwa mujibu wa Rais Ruto kwa sasa Kenya inajenga nyumba 273,000, huku nyumba 8,000 tayari zikikabidhiwa wanufaika. Nyumba nyingine 55,000 zinatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu, huku nyumba zaidi ya 700,000 zikiwa katika hatua mbalimbali za maandalizi na maendeleo.

Ruto amesema mfuko wa makazi umefanikiwa kukusanya takribani dola bilioni tano kupitia ufadhili wa ndani ya nchi, akiongeza kuwa mpango huo umeifanya Kenya kuwa na “mpango mkubwa zaidi wa makazi barani Afrika.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *