
Wanakikundi ni watoto na vijana wanane wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 19 kutoka Bolivia, Guatemala, Indonesia, Wales, Zambia na Zimbabwe, wakilenga kuhakikisha sauti za watoto na vijana zinazingatiwa katika maamuzi yanayowahusu.
Msingi wa kuunda kundi
Kwa mujibu wa kikosi kazi hicho, watoto na vijana mara nyingi hawawakilishwi ipasavyo katika mikutano ya kimataifa licha ya maamuzi hayo kuathiri maisha yao moja kwa moja.
Katika kipindi cha miezi 15 iliyopita, kundi hilo lilifanya kazi kwa pamoja kutafuta suluhisho la changamoto zinazokwamisha ushiriki wa watoto katika matukio ya kimataifa.
Kupitia tafiti mbili za kimataifa pamoja na mkutano wa mtandaoni uliowakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali duniani, walibaini kuwa hata pale watoto wanaposhirikishwa, ushiriki huo mara nyingi hauwi wa maana wala jumuishi vya kutosha.
Kundi hilo linaeleza kuwa ushiriki wa watoto unaweza kusaidia:
· Kuboresha maamuzi yanayohusu watoto na vijana
· Kuimarisha ujumuishaji katika mikutano ya kimataifa
· Kuwezesha watoto kueleza changamoto wanazokutana nazo
Changamoto katika ushiriki wa watoto
Pamoja na juhudi hizo, kundi hilo limebainisha changamoto mbalimbali zinazowazuia watoto kushiriki kikamilifu katika mikutano ya kimataifa, zikiwemo:
· Kukosekana kwa uwakilishi wa kweli wa watoto na vijana
· Kutokuwepo kwa mazingira salama na jumuishi
· Kushirikishwa katika hatua za mwisho badala ya mwanzo wa maamuzi
· Kukosekana kwa mrejesho baada ya mikutano kumalizika
Changamoto hizo zimeelezwa kuwa zinadhoofisha uwezo wa watoto kutoa mchango wenye matokeo katika maamuzi yanayowahusu.
Viwango vya ushiriki wa maana vyaanzishwa
Baada ya kuunda Kikosi Kazi cha Watoto na Vijana, wanachama hao walikutana mara kwa mara kuandaa viwango vya ushiriki wa maana wa watoto katika matukio ya kimataifa.
Viwango hivyo vinaongozwa na haki ya watoto kusikilizwa katika masuala yanayowahusu kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 12 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (CRC) uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1989.
Mwaka 2024, watoto na vijana wenye umri wa miaka 8 hadi 24 kutoka nchi 125 walishiriki katika utafiti wa kimataifa uliosaidia kuandaa viwango hivyo. Zaidi ya nusu yao walieleza kuwa wamewahi kushiriki angalau tukio moja la kimataifa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Mwongozo wa “Tujumuisheni!” wazinduliwa
Katika uzinduzi wa viwango hivyo uliofanyika mtandaoni Aprili 2026, Amanda ambaye ni mwanachama mwenye umri mdogo zaidi wa kikosi kazi hicho amesema lengo lao ni kuhakikisha sauti za watoto na vijana hazisikiki tu bali pia zinaheshimiwa.
Kundi hilo lilitengeneza mwongozo uitwao “Tujumuisheni!” ukiwa na maelekezo kuhusu mambo yanayopaswa kufanywa kabla, wakati na baada ya matukio ya kimataifa ili kuhakikisha ushiriki wa watoto unakuwa salama, jumuishi na wenye matokeo.
Mwanachama kutoka Wales, Arthur, amesema wametumia Mfano wa Ushiriki wa Lundy unaozingatia vipengele vinne vya ushiriki ambavyo ni nafasi, sauti, wasikilizaji na ushawishi. Aidha, viwango hivyo vinahimiza watoto kushirikishwa kuanzia hatua za mwanzo za kupanga mikutano hadi utekelezaji wa maamuzi baada ya mikutano kumalizika.
Wito wa hatua za pamoja
Francine kutoka Zambia alisema jina “Tujumuisheni!” lina maana ya kuwataka watoto kuwa sehemu ya maamuzi yanayoathiri maisha yao nyumbani, shuleni, katika jamii na katika mikutano ya kimataifa. Amesisitiza kuwa watoto si wapokeaji wa maamuzi pekee bali ni washiriki muhimu katika kuyaunda.
Afisa wa Kitengo cha Haki za Watoto na Vijana wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, Helen Griffiths, amesema ushiriki salama na wa maana wa watoto katika michakato ya kimataifa ni muhimu kwa maamuzi bora ya haki za binadamu.
Ameeleza kuwa watoto wana uzoefu wa moja kwa moja wa changamoto wanazokutana nazo, hivyo ushiriki wao unaweza kusaidia kuboresha sheria, sera na mipango inayowahusu pamoja na jamii kwa ujumla.
Wito wa kuimarisha ushiriki wa watoto
Kikosi kazi hicho kimetoa wito kwa mashirika yote duniani yanayofanya kazi na watoto na vijana kuhakikisha viwango hivyo vinatumika katika hatua zote za kupanga, kutekeleza na kufuatilia matukio ya kimataifa.
Kimesisitiza kuwa ushiriki wa watoto unapaswa kuwa wa kweli, salama, jumuishi na wenye matokeo ili kuhakikisha sauti zao zinachangia katika maamuzi ya sasa na ya baadaye.
