
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inatarajia kutumia Sh1 trilioni kuimarisha huduma za afya kisiwani humo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2026/30.
Kiwango hicho cha fedha kinachopangwa kutumika kwa miaka mitano ijayo ni ongezeko la zaidi ya mara sita ya Sh130 bilioni zilizotengwa miaka mitano iliyopita.
Hayo yameelezwa jana Jumapili, Mei 17, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mngereza Mzee Miraji wakati wa kufanya tathmini ya mradi wa ‘ZHSF Mothers’ unaotekelezwa na taasisi binafsi ya Pharm Access kwa kushirikiana na Wizara ya Afya chini ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF).
“Fedha hizo zitakwenda kuongeza ukarabati na miundombinu mbalimbali na kuimarisha afya ya msingi, Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya na kuwekeza zaidi katika sekta hiyo,” amesema.
Amesema kuimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto ni moja ya vipaumbele vya SMZ na ujenzi wa hospitali za wilaya na mkoa na kuunganisha mifumo na kuongeza wataalamu wa afya.
Amesema bado wajawazito wanapata changamoto ya kupata huduma kwa wakati hivyo mradi huo una umuhimu mkubwa kuhakikisha unamaliza changamoto hiyo.
“Wanawake hawa wapo katika hofu ya kutopata huduma kwa wakati, lakini kupitia mradi huu ZHSF Mothers, wamewezeshwa kuhudhuria kliniki mapema na kupata huduma kwa wakati katika vituo vya afya vya Serikali au binafsi na kujifungua kwa kituo wanachokiamini,” amesema
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Pharm Access, Dk Heri Marwa amesema wanashirikiana na ZHSF kuhakikisha mjamzito anapata huduma alipo bila kuangalia uwezo wake wa kifedha.
Amesema wamekuwa wakiwatambua wajawazito wasio na uwezo na kuwapa kadi za bima bure ili kupata huduma popote zinapopatikana.
Tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2025 katika wilaya mbili za Kaskazini B na Micheweni, Dk Marwa amesema tayari wamefikiwa wanawake 2,800 ambao kwa sasa wanapata huduma bure katika vituo vyote vya Serikali na binafsi.
“Kitu cha msingi mradi unaondoa fikra kumchukulia mjamzito kama kikundi, badala yake anachukuliwa yeye peke yake na zile taarifa zinapokusanywa anapokwenda kwenye huduma zinasaidia kumfuatilia,” amesema.
Amesema kila mwaka Zanzibar wanaojifungua ni 65,000 na kati ya hao asilimia 40 hawana uwezo wa kujilipia, hivyo wanataka ifikapo mwaka 2027 wanaojifungua katika visiwa hivyo wawe wamefikiwa na kupewa kadi za bima ya afya.
Amesema mradi huo umehakikisha mifumo inasomana ukiwemo wa Mfuko wa Afya Zanzibar, mfumo wa kupokea taarifa za wagonjwa na utambuzi wa matibabu yote hivyo inakuwa rahisi kufuatilia utoaji huduma.
Mkazi wa Mahonda ambaye ni mnufaika wa ZHSF Mother, Zaria Shah Mohamed, amesema kabla hapo alipoteza mtoto wake akiwa na ujauzito wa miezi saba kwa kushindwa kutumia dawa.
Mama huyo ambaye ana tatizo la shinikizo la damu (BP) alipata kifafa cha mimba kisha kikasababisha kupoteza mtoto wake.
“Huko nyuma nilipata ujauzito nilipofika miezi saba nikapata kifafa cha uzazi, kwa kuwa sikuwa na bima na sikupata elimu ya kutumia dawa za BP. Nilipofika kwenye jamii wakaniambia dawa ni mbaya nilimeza vidonge viwili nikaacha nikapata kifafa cha mimba yule mtoto alifariki.”
“Lakini sasa nina elimu na uhakika wa matibabu, pia wataalamu wanafuatilia afya yangu na mtoto hatua kwa hatua,”amesema.
