Sura mbili bodaboda za mkopo, Serikali yatoa mwelekeoSura mbili bodaboda za mkopo, Serikali yatoa mwelekeo

Dar es Salaam. Huduma ya usafiri wa pikipiki maarufu bodaboda licha ya kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wengi nchini, mikataba ya kinyonyaji kwa madereva hao pamoja na wamiliki kutapeliwa vyombo hivyo vya moto, vimetajwa kama kero kwa watu waliojiajiri kwenye sekta hiyo.

Changamoto kwa madereva, imetajwa ni mkataba wa kulipa kidogo kidogo kwa pikipiki inayouzwa Sh3 milioni kutakiwa kulipia Sh6 milioni kwa mwaka mmoja au miaka miwili na baadaye kuwa mmiliki wa chombo hicho.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Mei 18, 2026, Dereva bodaboda James Peter, mkazi wa Dar es Salaam amesema kila wiki hutakiwa kuwasilisha kwa mmiliki Sh70,000 ambazo zitapelekwa kwa miezi 16, sawa na Sh4.48 milioni.

Kiasi hicho amesema hakilingani na bei halisi ya pikipiki dukani ambayo ni Sh2 milioni.

“Ukifanya kazi kwa muda huo, chombo kinakuwa kimechoka hata ukifika wakati wa wewe kukimiliki hakikupi faida tena.”

Katika hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, Albert Msando katika Kongamano la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Dar es Salaam, jana Mei 17, 2026, amesema amepiga marufuku mikataba hiyo, akidai imekuwa ikiwakandamiza madereva wa bodaboda kiuchumi.

Msando amesema baadhi ya madereva wamekuwa wakipewa pikipiki kwa makubaliano ya kulipa kwa awamu kiasi kinachozidi thamani halisi ya chombo hicho.

Amesema baadhi ya mikataba, pikipiki yenye thamani ya Sh3 milioni hulipiwa hadi Sh6 milioni, jambo alilolodai ni aina ya unyonyaji kwa vijana wanaotafuta kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande mwingine, wakopeshaji wanaeleza kupata hasara baada ya kukopesha vyombo hiyo vya moto kwa mikataba kwa kuwa, baadhi ya madereva hawafanyi marejesho kwa wakati, hutokomea na pikipiki na wengine huvitelekeza.

Willfred Mollel, mkazi wa Arusha na mmoja wa wamiliki wa bodaboda wanaokopesha pikipiki kwa mikataba, amesema mfumo huo si wa kinyonyaji kama baadhi ya watu wanavyofikiri, kwa kuwa wao pia huwekeza fedha nyingi wakitarajia kupata faida.

Amesema wanaponunua pikipiki mara nyingi hutumia mikopo yenye riba, hivyo hulazimika kuweka masharti yatakayowawezesha kurejesha fedha hizo pamoja na kupata faida ndani ya kipindi cha mwaka mmoja au miwili.

“Tunapompa mtu pikipiki kwa makubaliano ya kulipa kidogo kidogo kwa mwaka mmoja au miwili, hatumkandamizi.

 “Hizi pikipiki tunazinunua kwa fedha ambazo wakati mwingine tumekopa na zinahitaji kurejeshwa pamoja na riba, sisi pia tunahitaji kupata faida,” amesema.

Hata hivyo, amesema changamoto wanazokutana nazo ni nyingi, ikiwamo baadhi ya madereva kutoroka na pikipiki hizo.

“Wakati mwingine dereva anaweza kutoroka na pikipiki na usimpate tena, akikimbilia mkoani hata kumfuatilia unaweza kutumia gharama kubwa zaidi na kuingia hasara,” amesema.

Erick Lucas, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam, amesema aliwahi kukumbana na changamoto baada ya kijana aliyemkabidhi pikipiki ya mkopo kukimbia baada ya kupata ajali.

“Nilimpa mtu pikipiki, lakini baada ya mwezi mmoja alikamatwa na polisi kutokana na ajali, yeye hakupata madhara yoyote, lakini alikimbia na kuiacha pikipiki kituoni bila kuifuatilia, kwangu hilo ilikuwa hasara kubwa,” amesema.

Amesema licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kurejesha fedha kila wiki, baadhi ya wakopaji hushindwa kutekeleza masharti hayo, hali inayowalazimu baadhi ya wamiliki kuwapokonya pikipiki kutokana na usumbufu unaojitokeza.

Sheria inasemaje?

Wakili Ibrahim Bendera amesema mikataba inasimamiwa na sheria ya mikataba na kama upo udhaifu umebainika kwenye jamii kupitia mikataba hiyo Serikali inapaswa kuweka utaratibu.

“Sera itafutwe ya kuwalinda wakopaji wa namna hiyo kuwe na kima kisheria ambacho riba ya mkopo haipaswi kuzidi, tukisema tuzuie watu wasikope hilo haliwezekani kinachohitajika ni utaratibu kuzuia unyonyaji,” amesema.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mikataba ya mwaka 2002, hususani vifungu vya 10 hadi 19 vinavyohusu ridhaa, udanganyifu na mikataba kandamizi, mkataba unaweza kupingwa kisheria endapo mmoja wa wahusika aliingia bila ridhaa ya hiari au chini ya masharti ya unyonyaji.

Sheria hiyo inaweka msingi kwamba makubaliano yoyote lazima yawe ya haki na yenye uwiano wa nguvu kati ya pande zote, jambo linalozua mjadala katika mikataba ya bodaboda inayoitwa kausha damu, malipo ya awamu yanadaiwa kuzidi thamani halisi ya pikipiki.

 Pia, kifungu cha 23(1) cha Sheria ya Mikataba Sura ya 345 ya mwaka 2002; “Malipo yoyote au jambo lolote la kimkataba laweza kuwa halali isipokuwa, limekatazwa kisheria, ni la kughushi, litadhuru mtu au mali ya mtu fulani, au endapo Mahakama italiona kama liko kinyume na maadili au sera za Serikali.

Aidha, Sheria ya Ushindani na Haki za Mlaji ya mwaka 2003 kupitia vifungu vya 6, 8 na 9 inakataza vitendo vya biashara visivyo vya haki, ikiwamo udanganyifu kwa mlaji na masharti kandamizi ya kibiashara.

Kwa upande mwingine, Sheria ya Ukodishaji kwa Awamu ya mwaka 2010 pamoja na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, zinaweka msingi wa uwazi katika mikopo na mauziano ya bidhaa kwa malipo ya awamu.

Sheria hizo kupitia vifungu vyao mbalimbali zinataka kuwepo kwa uwazi wa bei, masharti ya mkopo na ulinzi wa mkopaji dhidi ya masharti yasiyo ya haki, jambo linaloibua hoja kwamba endapo pikipiki ya thamani ya Sh2 milioni inalipishwa hadi Sh4milioni au Sh6 milioni bila uwiano wa wazi, basi mfumo huo unaweza kuhitaji kuangaliwa upya kisheria na kikanuni ili kuondoa uwezekano wa unyonyaji.

 Kauli ya Serikali

Akizungumzi na Mwananchi jana, Mei 17, 2026 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amewataka vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali, ikiwamo mikopo nafuu, badala ya kuingia kwenye mikataba inayowaathiri kiuchumi.

Nanauka amesema uwepo wa fursa za mikopo rahisi ya Serikali ni kuwaondoa vijana katika mtego wa mikopo inayowaumiza.

“Kuna mikopo ya halmashauri ya asilimia 10, ipo fedha kwenye mabenki mfano kwenye maendeleo ya jamii kuna mikopo ya asilimia saba ambayo wanaweza kupata kupitia mabenki, hii yote ni mikakati ya Serikali kupambana na chagamoto wanazokutana nazo vijana,” amesema.

Uwepo wa fursa hizo, Waziri Nanauka amesema vijana wanapoamua kuziacha na kwenda kukopa kwa mikataba ambayo inalalamikiwa Serikali haiwezi kuwazuia kwa kuwa hayo ni makubaliano baina yao.

Amesema kazi ya Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri ya vijana kupata fursa.

 “Wapo vijana mkoani Mwanza tuliwakopesha guta na bajaji na kuwapa mkopo wa Sh100 milioni kikundi kinaitwa Buswelu tumewapa kwa asilimia tano na wapo pia mkoani Mtwara,”amesema na kuongeza.

“Vijana waangalie fursa zenye unafuu zaidi kwao kwa ajii ya kutumia fursa ambazo Serikali inawatengenezea,” amesema.

Fursa nyingine aliyoitaja Waziri Nanauka ni ile iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu, hutolewa mafunzo ambayo Serikali imeingia makubaliano na viwanda ili vijana wakafanye mazoezi kupata uzoefu.

Amesema vijana wanaopitia progamu hiyo Serikali inawalipa kila mwezi kwenda kushiriki na progamu hiyo ni ya muda mrefu.

Eneo lingine, ni kilimo, madini na uvuvi, Nanauka amesema kuna mitaji ikiwamo ya mradi wa Jenga kesho iliyobora (BBT) kwenye mifugo, kilimo na madini.

“Tuna Wizara ya Viwanda na Baishara kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) wataanza kutoa fedha na awamu ya kwanza watatoa Sh5 bilioni,”amesema.

Wachambuzi

Akitoa njia kuhusu changamoto hiyo, Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Rashid Aziz amesema mfumo huo wa ukopeshaji hauna kinga dhidi ya madhara kama ajali au magonjwa.

“Ikitokea kijana ameumia au kuugua, hana bima wala msaada wa dharura, lakini bado anapaswa kuendelea kulipa deni la mkataba,”amesema.

 Pamoja na changamoto hiyo, amesema bado vijana wanajitokeza kuchukua pikipiki hizo kwa kuwa mbinu hiyo ndio wameiona njia mbadala wa kutimiza matakwa yao.

“Hii ni kama kausha damu lakini watu wanaona inawasaidia, sasa jambo la kufanya ni kuwaelimisha watu fursa zingine za Serikali zilizopo ili wasinase kwenye mitego hii,” amesema.

Mbali na hilo amesema ni muhimu Serikali ikadhibiti bei ya vyombo hivyo vya moto ili kuondoa tatizo hilo akitolea mfano taasisi za fedha ambazo hukopesha lakini ipo kiwango cha riba anayopaswa kutozwa mteja.

Kwa upande wake Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi Oscar Mkude amesema mikopo hiyo inatolewa kwa namna hiyo kutokana na kutokuwepo njia ya kumtafuta mkopaji atakapotoweka.

“Mtu ukimkopesha akatoroka unaweza kutumia hela na muda mwingi kumtafuta na usimpate, sasa ili kuondokana na hali hii tuwe na mfumo wa kisasa wa kitaifa ambao mtu anaweza kujulikana alipo iunganishwe kwenye vitambulisho vyake vyote, chochote anachofanya mtu kama kumtafuta unaingia tu kwenye mfumo unamuona,”amesema.

Amesema kukiwa na jambo ambalo linawaumiza wananchi na wao bado wanalikimbilia pamoja na ubaya wake inatoa ishara kwamba watu hao hawana mbinu nyingine zaidi ya iliyopo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbopo Dar es Salaam, Suleiman Lieme amesema mara nyingi changamoto nyingi ya mikataba wanasuluhisha.

Amesema licha ya mikataba wanayopewa bodaboda hao ni migumu, hata ikiwa imebaki wiki mbili kumaliza mkataba kama hakurejesha rejesho analodaiwa hupokonywa pikipiki.

“Mikataba ni migumu lakini huwa tunawaombea wapo wanaonyang’anywa pikipiki hata wakiwa wamebakiza deni dogo, kwa hiyo tunawasaidia waepukane na shida hizo, tatizo wanashindwa kufuata makubaliano,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *