Tanzania, Marekani zapanga mkataba mpya wa afya kuwa mfano AfrikaTanzania, Marekani zapanga mkataba mpya wa afya kuwa mfano Afrika

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Marekani zimeanza mazungumzo ya kuandaa mkataba mpya wa ushirikiano wa afya unaolenga kuwa mfano kwa nchi nyingine za Afrika, huku ukiahidi kuimarisha usalama wa afya, bima ya afya kwa wote na uzalishaji wa ndani wa bidhaa tiba.

Hatua hiyo imefikiwa leo Jumatatu, Mei 18, 2026 mjini Geneva nchini Uswisi, katika mkutano kati ya Waziri wa Afya wa Tanzania, Mohamed Omary Mchengerwa na Ofisa wa Marekani wa Shirika la Global Health, Brad Smith.

Katika mkutano huo, pande zote mbili zilikubaliana kuharakisha majadiliano kuhusu pendekezo la hati ya makubaliano ya ushirikiano wa afya ya kimataifa kati ya Tanzania na Marekani, huku zikisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuwa na manufaa kwa pande zote na kuzingatia sheria za kitaifa pamoja na wajibu wa kimataifa.

Smith anahudumu kama Mshauri wa Masuala ya Afya Kimataifa na Mshauri Mwandamizi katika Ofisi ya Usalama wa Afya ya Kimataifa na Diplomasia ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Mazungumzo hayo yalifungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa afya kati ya nchi hizo mbili, huku Tanzania ikiweka wazi dhamira yake ya kujenga mfumo imara zaidi wa afya unaojitegemea na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiafya za sasa na zijazo.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa (wa pili kulia) akiwa katika majadiliano na Ofisa wa Marekani wa Shirika la Global Health, Brad Smith mjini Geneva. Mchengerwa aliambatana na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa mjini Geneva, Abdallah Possi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mchengerwa amesema Tanzania ina matumaini makubwa kuhusu mazungumzo hayo na iko tayari kuanza ushirikiano wa kiufundi mara moja.

Amesema Tanzania inahitaji ushirikiano wenye uwiano unaosaidia kuimarisha mifumo ya afya, hususan katika eneo la bima ya afya kwa wote, uzalishaji wa ndani wa bidhaa tiba na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika huduma za afya.

“Tunataka mfumo wa ushirikiano ambao unaleta matokeo ya muda mrefu, unaosaidia wananchi kupata huduma bora na unaoijengea nchi uwezo wa kujitegemea zaidi katika sekta ya afya,” amesema Mchengerwa.

Katika mazungumzo hayo, suala la bima ya afya kwa wote lilijitokeza kama moja ya maeneo muhimu ya ushirikiano.

Tanzania inaendelea kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wengi zaidi, kupunguza malipo ya moja kwa moja kutoka mifukoni mwa wananchi na kuunganisha mifumo ya uchangiaji wa huduma za afya.

Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inatarajia kunufaika na uzoefu wa Marekani katika maeneo ya ubunifu wa mifumo ya ufadhili wa afya, usimamizi wa madai ya bima, udhibiti wa udanganyifu pamoja na uimara wa kifedha wa mifuko ya afya.

Aidha, pande zote mbili zimesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa vya uchunguzi na bidhaa nyingine za matibabu ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Mchengerwa amesema kuimarika kwa uzalishaji wa ndani kutasaidia kuongeza usalama wa afya wa kikanda, kuimarisha upatikanaji wa bidhaa tiba na kufungua fursa za uwekezaji kwa kampuni za Marekani nchini Tanzania.

Katika hilo, ametaja ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Kampuni ya Abbott katika kusaidia uzalishaji wa vifaa vya vipimo vya haraka vya VVU, kaswende na homa ya ini kuwa mfano wa ushirikiano unaoweza kupanuliwa zaidi.

Kwa zaidi ya miaka 20, Tanzania na Marekani zimekuwa zikishirikiana katika mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU na Ukimwi, kifua kikuu na malaria kupitia programu mbalimbali za afya ikiwemo PEPFAR.

Ushirikiano huo pia umechangia kuimarisha mifumo ya maabara, minyororo ya ugavi wa vifaa tiba pamoja na maendeleo ya wataalamu wa afya nchini.

Sasa, kupitia mkataba huo mpya unaopendekezwa, nchi hizo mbili zinatarajia kujenga mfumo wenye uhakika zaidi wa ushirikiano wa muda mrefu, unaolenga matokeo na unaoweza kuigwa na nchi nyingine za Afrika.

Katika mkutano huo, Mchengerwa aliambatana na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa mjini Geneva, Abdallah Possi.

Kwa upande wa Marekani, Smith aliambatana na Michael Behan, Mshauri wa Afya ya Umma katika Ujumbe wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *