Sauti ya mwanamke na haki zake vyawezekana Kilifi Kenya: Mbunge Martha KokiSauti ya mwanamke na haki zake vyawezekana Kilifi Kenya: Mbunge Martha Koki

Lakini katika Kaunti ya Kilifi, Mbunge Martha Koki anasema mabadiliko yanaanza kuonekana huku wanawake wakizidi kupewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya jamii na siasa.

Akizungumza katika mahojiano malum na Un News Kiswahili Martha Koki amesema moja ya changamoto kubwa inayowakabili wanawake ni suala la urithi wa ardhi na mali, ambapo wanawake wengi bado wananyimwa haki zao kwa misingi ya mila na desturi.

“Kwanza kabisa ile changamoto kubwa ambayo iko ni urithi wa mashamba. Mwanamke anaambiwa hawezi kurithi kwa sababu ataolewa na kwenda kwa mumewe,” amesema Koki.

Amesema hali hiyo huwafanya wanawake wengi kubaki bila usalama wa kiuchumi, hasa wanapopoteza waume zao au familia kuwakatalia haki yao ya kumiliki ardhi.

Wanawake bado wachache sana katika uongozi

Mbunge huyo amesema licha ya hatua zinazopigwa katika usawa wa kijinsia, wanawake bado hawapati nafasi sawa katika siasa na ajira.

Katika Bunge la Kaunti ya Kilifi lenye wadi 35, ni wanawake watatu pekee waliochaguliwa moja kwa moja, jambo ambalo amesema linaonesha safari bado ni ndefu.

“Sauti zetu zinaweza kusikika. Zile zama ambazo zilikuwa ni za kukaa jikoni, kuangalia watoto na kupika zimeisha. Ni wakati wetu kujitokeza kama kinamama,” amesema.

Hata hivyo, amepongeza uongozi wa kaunti hiyo kwa kutoa nafasi sawa kwa wanawake katika serikali ya kaunti, akieleza kuwa nusu ya mawaziri wa kaunti ni wanawake huku naibu gavana akiwa mwanamke pia.

Mapambano ya wajane kupata haki zao

Koki amesema tayari ameanzisha juhudi za kuwasaidia wajane zaidi ya 2,500 katika eneo lake kupitia msaada wa kisheria wa bure ili waweze kuelewa na kudai haki zao.

Kwa mujibu wake, wanawake wengi hushindwa kwenda mahakamani kwa sababu ya umaskini na kutofahamu sheria.

“Tuko na wanasheria ambao wanajitokeza kusaidia wamama wengi ambao wako katika hizi hali, kwa sababu wengi wao hawana hata fedha za kwenda mahakamani,” amesema.

Mbunge huyo ameongeza kuwa anapanga kupeleka mjadala bungeni utakaoimarisha sheria za kuwalinda wajane wanaonyang’anywa mali baada ya vifo vya waume zao.

Vita dhidi ya ndoa za mapema na mimba za utotoni

Katika maeneo ya pwani kama Mombasa, Kilifi na Malindi, ndoa za mapema na mimba za utotoni zimekuwa changamoto kubwa inayowazuia wasichana wengi kumaliza masomo yao.

Lakini Koki anasema juhudi za utoaji wa ufadhili wa masomo, kampeni za uhamasishaji na ushirikiano na mashirika mbalimbali zimeanza kuzaa matunda.

“Mtoto akibaki nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa karo, mzazi anaona bora aolewe apate mahari. Lakini sasa hivi zile namba za mimba za mapema na watoto kutokusoma zinashuka chini kabisa,” amesema.

Amesema wazazi wengi sasa wanaanza kuelewa umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike sawa na mtoto wa kiume.

“Tofauti ni jinsia tu, akili ziko sawa”

Kwa mujibu wa Koki, mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana bila kubadili mitazamo ya jamii kuhusu uwezo wa wanawake.

Anasema hata yeye alipowania uongozi, wengi walikuwa na mashaka kuhusu mwanamke kuongoza, lakini sasa jamii imeanza kuona uwezo wa viongozi wanawake.

“Wameanza kuona kumbe hata mama anaweza kuongoza zaidi kushinda yule aliyekuwa awali,” amesema.

Ametoa wito kwa jamii kuacha mila zinazowabagua wanawake na badala yake kutoa nafasi sawa kwa watoto wa kike.

“Tofauti ni jinsia tu, lakini akili zetu ziko sawa. Mawazo yetu yako sawa. Mtoto wa kike apewe nafasi sawa sawa kama mtoto wa kiume,” amesema.

Wito wa kuendelea kuhamasisha wanawake

Mbunge huyo amesema kongamano na mijadala ya haki za wanawake ni muhimu kwa kuwapa wanawake ujasiri wa kuzungumza na kushiriki katika maendeleo ya jamii zao.

Anasema mafanikio yake kisiasa yametokana na wanawake waliomwamini na kumpigia kura, na sasa anataka kuona wanawake wengi zaidi wakijitokeza katika uongozi, biashara, elimu na sekta ya afya.

“Mazungumzo kama haya yanampa mama nafasi ya kujua anaweza na anaweza kusikika,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *