
Katibu Mkuu amesema azimio hilo linaweka wazi wajibu wa nchi wanachama kulinda wananchi wao dhidi ya kile alichokiita “ongezeko la mgogoro wa tabianchi”.
Azimio hilo lililoandaliwa na Vanuatu nchi ya visiwa vya Pasifiki iliyo mstari wa mbele kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na nchi nyingine, limepitishwa baada ya mjadala mkali uliohusisha marekebisho kadhaa yaliyopendekezwa.
Azimio hilo limepata kura 141 za kuunga mkono, 8 kupinga na 28 kujizuia kupiga kura.
Nchi zilizopiga kura za kupinga ni Belarus, Iran, Israel, Liberia, Urusi, Saudi Arabia, Marekani na Yemen.
Uamuzi wa ICJ umetajwa kama mafanikio makubwa
Wakati Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, chombo kikuu cha mahakama cha Umoja wa Mataifa ilipotoa uamuzi Julai 2025 kwamba mataifa yana wajibu wa kulinda mazingira dhidi ya uzalishaji wa gesi chafu (GHG), uamuzi huo ulipokelewa kama mafanikio makubwa. Katibu Mkuu aliueleza kwa kifupi kama “ushindi kwa sayari yetu”.
Wajibu wa kisheria
Mahakama pia iliamua kwamba iwapo mataifa yatakiuka wajibu huo, yatawajibika kisheria na yanaweza kutakiwa kusitisha vitendo hivyo visivyo halali, kutoa dhamana kwamba havitarudiwa, na kufanya fidia kamili kulingana na mazingira ya kesi husika.
Ingawa maoni ya ushauri ya ICJ hayalazimishi kisheria, yana uzito mkubwa wa kisheria na kimaadili yakisaidia kufafanua na kuendeleza sheria za kimataifa kwa kubainisha wajibu wa mataifa.
Uamuzi wa Baraza Kuu uliofuatia leo Jumatano unaashiria ujumbe mzito kwamba kukabiliana na janga la tabianchi ni wajibu wa kisheria chini ya sheria za kimataifa, si chaguo la kisiasa tu.
“Mahakama ya juu kabisa duniani imetoa kauli yake,” amesema Guterres. “Leo, Baraza Kuu limejibu.”
Yaliyomo kwenye azimio
Azimio linazitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua zote zinazowezekana kuzuia uharibifu mkubwa wa hali ya hewa na mazingira, ikiwemo uzalishaji unaotokana na ndani ya mipaka yao, na kutekeleza ahadi zao za tabianchi chini ya Mkataba wa Paris.
Serikali zimetakiwa kushirikiana kwa nia njema na kuratibu juhudi kwa kuendelea ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani, na kuhakikisha sera za tabianchi zinalinda haki ya kuishi, afya na kiwango cha maisha kinachokubalika.
Katika taarifa yake baada ya kura hiyo, Guterres alisema wale walio na mchango mdogo zaidi katika mabadiliko ya tabianchi ndio wanaolipa gharama kubwa zaidi, na kwamba njia ya haki ya tabianchi “inapitia katika mabadiliko ya haraka, ya haki na ya usawa kutoka nishati ya mafuta kuelekea nishati jadidifu au mbadala.”
Katibu Mkuu amebainisha kuwa nishati mbadala imethibitika kuwa ya bei nafuu zaidi na salama zaidi, na kwamba lengo la kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi joto 1.5 juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda bado linawezekana kufikiwa.
Mambo muhimu ya azimio
- Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) limepitisha azimio “Maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu wajibu wa Mataifa katika mabadiliko ya tabianchi”
- Azimio hilo, lililoandaliwa na Vanuatu na nchi nyingine, limepitishwa kwa kura 141 za ndio, 8 za hapana na 28 wamejizuia kupiga kura.
