
“Raia mmoja aliuawa kila takriban dakika 14 mwaka 2025” amesema Edem Wosornu, Mkurugenzi wa kitengo cha kukabiliana na dharura kwenye Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu na masuala ya misaada ya kibinadamu na hali za dharura OCHAmbele ya wajumbe wa Baraza hilo katika kikao kilichomulika ulinzi wa raia katika mizozo jijini New York Marekani.
Amebainisha kuwa takwimu hizo zinahusu tu vifo vilivyothibitishwa katika migogoro 20 ya silaha.
Amesema idadi halisi huenda ni kubwa zaidi, akitaja mizozo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sudan, Ukraine, Eneo linalokaliwa kimabavu na Israel la Palestina na maeneo mengine.
Raia walengwa majumbani, mashuleni na sokoni: UN
Bi. Wosornu ameeleza hali ya kutisha ya raia katika maeneo ya vita aliyoyatembelea.
“Mara nyingi hawawi tu madhara ya pembeni,” amesema. “Wanalengwa moja kwa moja.”
Amesema raia wanauawa “majumbani mwao, sokoni, kazini, shuleni, barabarani na hata wanapokimbia kutafuta usalama,” hali inayoonesha jinsi vurugu zilivyoingia katika maisha ya kila siku.
Mashambulizi dhidi ya huduma za afya yaendelea
Licha ya Baraza la Usalama kupitisha Azimio 2286 (2016) kuhusu ulinzi wa huduma za afya katika vita, hali imeendelea kuwa mbaya zaidi, amesema Wosornu.
Amesema unyanyasaji wa kingono bado umeenea, watoto wanatekwa na kuingizwa vitani, waandishi wa habari wanalengwa, na watu wenye ulemavu huachwa nyuma wakati mashambulizi yanapotokea.
“Haya yote ni matokeo ya maamuzi ya makusudi,” amesisitiza, akitoa wito kwa nchi wanachama kuheshimu Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa za kibinadamu bila ubaguzi.
Amezitaka pia nchi kuepuka matumizi ya silaha nzito katika maeneo yenye watu wengi na kusitisha uhamishaji wa silaha pale ambapo kuna hatari ya kutumika dhidi ya raia.
ICRC: Vita visivyo na sheria vinaharibu ubinadamu
Akizungumza katika kikao hicho, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Msalaba mwekundu ICRC, Mirjana Spoljaric Egger, ameonya kuwa vita vya kisasa vinazidi kupoteza ufuasi wa sheria za kimataifa.
“Vita vinavyoendeshwa bila sheria hubadilisha vita dhidi ya wapiganaji kuwa vita dhidi ya raia,” amesema.
Amesema mifumo ya ukatili wa vita imeenea katika maeneo mbalimbali, kutoka Mashariki ya Kati hadi Pembe ya Afrika na Ulaya ya Mashariki.
Hatuwezi tena kujifanya hatuoni
Bi. Spoljaric Egger ameonya kuwa lugha na vitendo vya kudhalilisha jamii nzima vinachochea uhalifu wa kivita na kuvunja misingi ya maadili ya binadamu.
“Hatuwezi tena kujifanya kuwa tunachokiona katika maeneo ya vita kinaendana na sheria,” amesema.
Ameongeza kuwa historia inaonesha kuwa kudhalilisha binadamu ni hatua ya awali ya mauaji makubwa ya halaiki.
“Hutufanya tuache kuona wengine kama binadamu sawa na sisi,” ameongeza, akisema hali hiyo hurahisisha uhalalishaji wa mauaji, mateso na ukatili.
Wito wa hatua za haraka kulinda raia
Mjadala huo umeonesha wasiwasi unaoongezeka ndani ya Baraza la Usalama kwamba mifumo ya ulinzi wa raia inashindwa kukabiliana na ukubwa wa migogoro ya sasa, huku viongozi wakitoa wito wa haraka wa hatua za kisiasa kurejesha heshima ya sheria za kimataifa na kuzuia maafa zaidi ya kibinadamu.
